LEGENDARI wa soka nchini aliyewahi kutamba na klabu za Simba na Yanga pamoja na timu ya taifa, Taifa Stars, Zamoyoni Mogella ‘Golden Boy’ ametoa mtazamo akisema ujanja iliyonao Yanga kiasi cha kuizidi Simba ni kitendo cha kusajili wachezaji wenye viwango vya juu, vilivyoipa klabu mafanikio.
Mshambuliaji huyo aliyewahi kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, ameeleza hayo alipozungumza na Mwanaspoti na kusema endapo Wanamsimbazi wakitaka kicheko msimu ujao ni lazima uongozi wa klabu hiyo usajili wachezaji wenye viwango vya juu watakaoiletea tija la sivyo watateseka zaidi.
“Ni kweli Simba ilicheza fainali za CAF, lakini kilichofanya isichukue taji ni ubora wa wachezaji kuwa chini ukilinganisha na wa timu ya RS Berkane na ukweli kama wanataka kutisha na kuwazidi hata watani wao ni lazima wasajili wachezaji wa aina hiyo watakaoleta mapinduzi,” alisema Mogella na kuongeza;
“Mechi ya mwisho ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga ambapo Simba ilipoteza kwa mabao 2-0 ndio iliyoonyesha ukweli na tofauti ya ubora wa wachezaji wa timu hizo na kocha Fadlu Davids aliweka wazi hilo. Nami nasisitiza ili Simba irejee kunyakua mataji inahitaji kufanya usajili wa nguvu, wachezaji wazuri wapo skauti isiwatafute wa bei chee.”
Mogella alisema kipindi ambacho Simba ilikuwa inanyakua mataji mfululizo (back to back), ilikuwa na kikosi imara kama Meddie Kagere aliyechukua kiatu cha mfungaji bora misimu miwili mfululizo (2018/19 mabao 23, 2019/20 mabao 22), kilikuwa na kina Emmanuel Okwi na wengineo.
“Kikosi cha Simba kilikuwa kipana na cha wachezaji wa viwango kama Jose Luis Miquissone hadi timu ya Al Ahly ikashawishika kumsajili, Clatous Chama hadi akasajiliwa na RS Berkane, John Bocco alikuwa wa moto, kifupi ilikuwa na wachezaji wa viwango.”
“Wakati huo Yanga ikawa inajipanga ikasajili kina Michael Sarpong, Fiston Abdulrazak, kabla ya kuja na Fiston Mayele, Joyce Lomalisa, Tuisila Kisinda wachezaji wa viwango hata walipoondoka wameleta mbadala wenye uwezo, kuna kina Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli, Stephane Aziz Ki ambaye kaondoka, Simba inahitaji utulivu kufanya hilo wachezaji wazuri wapo wengi,” alisema.