Mtanda akazia Sh34 bilioni kupelekwa Malya

Dodoma. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amezungumzia mvutano wa Sh34 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi na upanuzi wa Kituo cha Michezo cha Malya, akieleza kuwa mvurugano huo umetokana na wanasiasa kuchanganya mambo.

Akizungumza leo Jumatano Julai 16, 2025 jijini Dodoma wakati wa kuelezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika utekelezaji wa miradi mikubwa mkoani Mwanza, Mtanda amefunguka kuhusu mvutano wa fedha hizo.

Pia, amesema Serikali imetumia jumla ya Sh5.5 trilioni katika kipindi cha miaka minne iliyopita.

Kauli ya Mtanda kuhusu Sh34 bilioni imekuja baada ya kuulizwa kuhusu mvutano wa fedha hizo na mahali zilipokusudiwa kuelekezwa, suala ambalo limeibua kauli zinazokinzana miongoni mwa viongozi wa kisiasa.

“Wapi kituo kinajengwa zile zilikuwa ni kauli za wanasiasa, sisi tunajenga kituo mahali ambapo kuna kituo kwa hiyo tunafanya maboresho tu na mkumbuke Sumve na Malya zote zipo wilaya moja ya Kwimba sasa tatizo lipo wapi,” amesema Mtanda.

Fedha hizo ziliwahi kuzua malalamiko bungeni kutoka kwa Mbunge wa Sumve anayemaliza muda wake, Kasalali Mageni, aliyedai kuwa zilikuwa zimepangwa kujenga kituo cha michezo katika eneo la Sumve.

Hata hivyo, Mageni alieleza kushtushwa na taarifa kwamba matumizi ya fedha hizo yamebadilishwa ghafla, akidai kuwa hatua hiyo ni sehemu ya njama za baadhi ya watu wanaolenga kumhujumu kisiasa.

Mageni alidai kuwa baadhi ya viongozi walihusika kuhamisha fedha hizo kwenda Malya, eneo ambalo tayari lina kituo cha michezo, jambo aliloliona si sahihi kwa kuwa haikuwa busara kuendeleza miradi yote katika eneo moja.

Kauli hiyo ilimfanya Waziri wa Habari, Profesa Palamagamba Kabudi, kuingilia kati na kuahidi kufuatilia suala hilo kwa kina.

Hata hivyo, Mageni hakuchukua fomu ya kuomba uteuzi kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi ujao.

Akizungumza kuhusu maendeleo ya jumla mkoani Mwanza, Mkuu wa Mkoa Mtanda amesema sekta ya maji imepiga hatua kubwa, huku huduma ya umeme ikiwa imefika katika vijiji vyote vilivyoko maeneo ya bara.

Mtanda amesema vijiji 23 vilivyopo kwenye visiwa tayari vimepatiwa wakandarasi wanaoanza kufunga umeme wa jua, ili kuhakikisha huduma hiyo inawafikia wananchi wote.

Amesema lengo la mkoa ni kuhakikisha Mwanza inakuwa miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa kuchangia pato la Taifa.

Mtanda ameeleza kuwa maeneo mengi ya mkoa huo yana rasilimali za madini, na kwamba shughuli za uchimbaji zimeanza kushamiri, hususan katika Wilaya ya Misungwi.

Related Posts