Mwalimu adaiwa kujinyonga kisa wivu wa mapenzi

Tanga. Mwalimu Enock Peter (32) wa Shule ya Msingi Potwe wilayani Muheza mkoani Tanga, amedaiwa kujinyonga kwa kutumia shuka nyumbani kwake, huku wivu wa mapenzi ukitajwa kuwa chanzo cha tukio hilo.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu tukio hilo leo Jumatano Julai 16, 2025, Mratibu Elimu Kata ya Pongwe, Rajabu Msuya amesema alifika shuleni hapo kwa ajili ya kufanya kikao, walimu wote walikuwapo kasoro mwalimu Enock.

“Nilimtuma mwanafunzi aende nyumbani kwake akamuite, lakini aliporudi akasema amegonga lakini hakuitikiwa. Baadaye mwalimu mwingine alienda naye, wakagonga bila kuitikiwa, akaamua kuchungulia dirishani ndipo akamuona mwenzetu amejinyonga,” amesimulia Msuya.

Amesema baada ya kubaini hayo, walitoa taarifa polisi na askari walifika na  kuingia ndani na kukuta amejinyonga kwa kutumia shuka aliyoifunga kwenye mbao za juu ya paa la nyumba ya shule aliyokuwa akiishi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi amesema uchunguzi wa awali unaonesha chanzo cha kifo hicho ni wivu wa mapenzi.

“Katika uchunguzi wetu tumebaini marehemu alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mpenzi wake (jina limehifadhiwa). Waliwahi kugombana na alichana vyeti vya mwenza wake na kesi ilikuwa inaendelea mahakamani. Wakati kesi ikiendelea, ndiyo mwalimu huyo ameamua kujinyonga,” amesema.

Amesema Enock alishawahi kukamatwa na kufunguliwa kesi mahakamani akituhumiwa kwa uharibifu wa mali za mwenza wake na aliachiwa kwa dhamana huku kesi ikiendelea.

Shuhuda wa tukio hilo, Abdulrazaq Kikungo amedai siku mbili kabla ya kujinyonga, Enock aligombana na mwenza wake baada ya kudai kumkuta na ujumbe wa mapenzi kwenye simu. Alimtishia kumuua kwa kisu, jambo lililomfanya mwenza huyo kukimbia.

“Baada ya mpenzi wake kutoroka, Enock alichukua kisu na kukatakata baadhi ya vyombo, kuvunja kabati na kuchana vyeti vya chuo vya mwenza wake. Alishtakiwa polisi na alikamatwa, akaamriwa kulipa gharama za vyeti.”

Amesema wakati mvutano huo ukiendelea na kesi ikiwa mahakamani, jana ndipo waligundua mwalimu huyo amejinyonga, wakihisi chanzo ni wivu wa mapenzi.

“Baada ya ugomvi huo, Enock alikuwa hatoki nje. Mchana alikuwa anakaa ndani pekee yake, usiku kidogo ndio anaenda dukani kununua mikate au viazi. Hata, mahudhurio yake kazini hayakuwa mazuri,” ameongeza.

Mwili wa mwalimu huyo umeagwa leo katika viwanja vya Shule ya Msingi Potwe kabla ya kusafirishwa kwenda nyumbani kwao, Ngara mkoani Kagera, kwa ajili ya maziko.

Huyu ni mtumishi wa pili wa umma kudaiwa kujinyonga baada ya Julai 10, 2025, daktari bingwa wa watoto wa Hospitali Teule ya Kibosho Mkoani Kilimanjaro, Magreth Swai (30)  kujinyonga kwa kutumia waya wa antena alioufunga kwenye nondo ya mlango wa chumbani kwake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa ambaye alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, alidai kuwa chanzo ni msongo wa mawazo uliotokana na afya ya akili.

“Mnamo Julai 10, 2025 majira ya saa 3 usiku huko Longuo, Wilaya ya Moshi, Magreth Swai ambaye ni daktari amejiua kwa kutumia waya wa antena alioufunga kwenye nondo ya mlango wa chumbani katika nyumba anayoishi,” alisema Kamanda Maigwa.

Related Posts