Mwisho wa enzi Profesa Lipumba kuisaka Ikulu

Wakati mchakato wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu ukikamilika ndani ya Chama cha Wananchi (CUF), Mwananchi imethibitishiwa kwamba mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba hatogombea tena urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Tangu kuanza kwa chaguzi katika mfumo wa vyama vingi, Profesa Lipumba amegombea urais mara tano kuanzia mwaka 1995, 2000, 2005, 2010 na 2020. Hakugombea urais mwaka 2015 kwa sababu chama hicho kiliungana na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Katika matokeo ya uchaguzi miaka ya nyuma, Profesa Lipumba amekuwa akiingia kwenye nafasi tatu bora, hata hivyo katika uchaguzi wa mwaka 2020, aliporomoka hadi nafasi ya tano kati ya wagombea 17 waliopitishwa na Tume ya Uchaguzi.

Hadi sasa, makada wanne wamejitokeza kutia nia ya kuomba ridhaa ya chama hicho, kati yao kuna mwanamke mmoja na wanaume watatu. Wagombea hao ni Rose Kahoji, Kiwale Mkungutila, Chif Lutalosa Yemba na Gombo Samandito.

Akizungumzia ushiriki wa Profesa Lipumba kwenye uchaguzi wa Oktoba 2025, Makamu Mwenyekiti wa CUF Tanzania Bara, Omar Dunga anasema mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Lipumba hagombei tena nafasi hiyo katika uchaguzi ujao.

“Uamuzi wake wa kutokugombea tena urais, ameusema rasmi kwenye kikao cha kamati ya uongozi ya chama kilichofanyika Mei, mwaka huu, na tulianza mikakati ya kutafuta mgombea mwingine,” anasema.

Kwa mujibu wa Dunga, uamuzi huo wa Profesa Lipumba si kwa nafasi ya urais pekee bali hata nafasi ya uenyekiti anayoishika, akimaliza muda wake atakaa pembeni na kubaki mshauri wa chama.

“Mpango wetu ni kutafuta mgombea mwenye nguvu na mvuto, unajua Profesa Lipumba amekuwa mgombea wetu wa urais tangu mwaka 1995 hadi mwaka 2020, kasoro mwaka 2015 tu hakugombea kwa kuwa tulikuwa kwenye muungano wa Ukawa,” anasema. Dunga anasema Profesa Lipumba amenyosha mikono ya kutoutaka urais tena kwa sababu kulingana na mfumo wa Katiba iliyopo kwani hata akipambana hawezi kushinda wadhifa huo wa juu katika taifa. “Katiba na sheria zilizopo si rafiki na zinaonyesha kabisa upande gani unapaswa kutoa mshindi, sasa hiyo hali ametathmini na kuona kwamba asigombee tena, uwanja haujawa sawa,” anasema Dunga.

Dunga anaeleza kwamba siku Profesa Lipumba anawaeleza kuto kugombea katika kikao hicho, alitaja sababu mbili kubwa; kwanza, umri wake, anafikisha miaka 73, lakini kusumbuliwa na maradhi, hivyo anahitaji muda wa kupumzika. “Yeye hana tamaa na hivi vyeo, hata mara zote anataka watu wajitokeze kugombea lakini hawajitokezi ndiyo maana alikuwa anagombea. Sasa wakati ni ukuta, imefikia hatua hawezi kuendelea tena,” anasema Dunga.

Dunga anabainisha kwamba Profesa Lipumba aliyezaliwa Juni 6, 1952, eneo la Ilolangulu mkoani Tabora, anaona muda umefika na hawezi kushindana nao kwani anaweza kuumia akilazimisha na kuwaachia watu wengine kushika kijiti hicho.

Wakati akieleza hayo, Katibu Mkuu wa CUF, Husna Mohamed Abdallah amesema kati ya wagombea wanne waliojitokeza kuchukua fomu hadi sasa, Profesa Lipumba hajajitokeza kuwa miongoni mwao.

“Lipumba hajachukua fomu na toka mwanzo hakuonyesha nia, ingawa tulitamani angeingia kwenye kinyang’anyiro lakini imekuwa tofauti,” anasema Husna.

Panda shuka kura za Lipumba

Matokeo ya Profesa Lipumba kwenye chaguzi zilizopita yamekuwa yakipanda na kushuka ingawa matokeo yake ya uchaguzi yanayotangazwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), katika uchaguzi wa mwaka 2020, yaliporomoka zaidi ukilinganisha na chaguzi zilizotangulia.

Katika uchaguzi huo (wa 2020), Profesa Lipumba alipata kura 72,885 zilizomfanya kushika nafasi ya tano, katika uchaguzi huo ambao mgombea wa CCM, John Magufuli aliongoza kwa kura 12,516,252. Alipogombea kwa mara ya kwanza mwaka 1995, alianza kwa kushika nafasi ya tatu, akipata asilimia 6.43 ya kura zote, mshindi alikuwa mgombea wa CCM, Benjamin Mkapa aliyepata jumla ya kura 4,026,422, sawa na asilimia 61.82 ya kura zote.

Uchaguzi wa mwaka 2000, Profesa Lipumba alipanda kwa kupata kura 1,329,077, sawa na asilimia 6.26 akimfuatia Mkapa aliyeshinda kwa kupata kura 5,863,201, sawa na asilimia 71.74 za kura zote za urais.

Uchaguzi uliofuata, mwaka 2005, Profesa Lipumba aliendelea kushika nafasi ya pili akipata kura 1,327,125 nyuma ya mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete aliyeshinda kwa kishindo, akijikusanyia kura 9,123, 952 sawa na asilimia 80.28.

Uchaguzi wa mwaka 2010, Profesa Lipumba alishushwa hadi nafasi ya tatu kwa kupata asilimia 8.28 huku aliyekuwa mgombea wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa akipata kura 2,271,941, sawa na asilimia 27.05 akimfuatia Kikwete aliyeshuka kwa kupata kura 5,276,827 sawa na asilimia 62.83.

Mwaka 2015, Profesa Lipumba hakugombea baada ya kutofautiana na viongozi wenzake ndani ya CUF, hususan aliyekuwa Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye baadaye alijiunga na ACT Wazalendo.

Chanzo cha mvutano huo ni hatua ya Maalim Seif kuunganisha nguvu na vyama vya Ukawa, na kukubaliana kumuunga mkono mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa aliyekuwa amehamia chama hicho kutokea CCM.

Profesa Lipumba alijiuzulu kwenye nafasi yake na kubaki kuwa mwanachama wa kawaida akijitenga na uamuzi uliochukuliwa na Maalim Seif. Hata hivyo, baadaye alirejea na kudai kwamba ametengua uamuzi wake wa kujiuzulu, hivyo akarejea kwenye nafasi yake.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Conrad Masabo anataja sababu mbili kubwa zilizomsukuma Profesa Lipumba kuchukua uamuzi huo; kwanza, ni kupungua kwa ushawishi wake ndani ya chama hicho.

Pili, anasema ni kupungua kwa mapato kwani unapokuwa mgombea urais mwenye ushawishi, chama kinauzika na mnapata kura nyingi za wabunge zinazoamua nafasi ya viti maalumu.

“Ukipata viti maalumu chama kinapata ruzuku inayosaidia hata kiongozi kuendesha shughuli za kichama, lakini kwa sasa hali ya kisiasa imebadilika, kuna matumizi makubwa ya nguvu, hata ukipigiwa kura zinaweza zisijulikane,” anasema.

Anasema uwezekano wa kuzipata hata kura ulizopigiwa hakuna lakini afya yake inawezekana inashida kama anavyodai anaweza akashindwa kuhimili vishindo vya uelekeo wa sasa.

Related Posts