KAMISHINA wa ufundi na mashindano wa shirikisho la Mpira wa Kikapu nchini (TBF), Daniel Patrick amesema nidhamu ndiyo iliyombeba Miyasi Nyamoko achaguliwe kuwa kocha bora.
Patrick alisema hayo baada ya lawama za baadhi ya makocha, Nyamoko hakustaili kuwa kocha bora kutokana na timu yake kushika nafasi ya pili.
Alisema uteuzi wa kocha bora, uliangaliwa na vigezo vingi ikiwemo nidhamu, jinsi anavyosimamia benchi lake na mawasiliano mazuri na meza ya wasimamizi wa mchezo.
Katika mashindano ya Kombe la Taifa yaliyofanyika mwaka juzi mkoani Tanga, kocha bora alichaguliwa Daruweshi Shamuni kutoka timu iliyoshika nafasi ya pili ya Unguja.
Mkufunzi wa wahamuzi, Prosper Mushi alisema makocha wamekuwa wakikariri kocha bora ni yule aliyeipa ubingwa timu yake.
Akitolea mfano kocha anaweza akawa na wachezaji wazuri, kutokana na ubora wao amekuwa akishindwa kutoa hata maelekezo na timu yake ikawa bingwa.
“Ninachosema kocha bora ni yule aliyeitengeneza timu na kuipambania hadi kufika fainali,” alisema Mushi.
Nyamoko anafundisha pia Srelio katika Ligi ya kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) na ameifanya iwe moja ya timu tishio katika ligi hiyo.