NIKWAMBIE MAMA: Dira, sera mpya ziwe mkombozi

Tumesikia mengi kutoka kwa vyama na wanasiasa hasa wakati huu tukielekea kwenye uchaguzi. Mengine sijui ni sera, mengine dira, kuna mpya na yapo marudio.

Wapo wanaofundisha kutokupiga kura bila mabadiliko ya sheria, wengine kwenda nyumbani baada ya kupiga kura, lakini kuna wale wa “Hakuna kulala”, hawa wanasisitiza kuzilinda kura zisiibwe kabla hazijahesabiwa na kutangazwa. Haondoki mtu hadi kieleweke.

Sijui, ila kuna hatari wapigakura watayaweka yote kwenye kapu moja. Wanaweza kujikuta wakishindwa kukumbuka wanachotarajia pindi watapokipa ridhaa chama kimojawapo.

Maneno yamekuwa mengi sana kama yanayosomwa kwenye daftari la Historia, tena la Shule ya Msingi. Vyama vinajiongeza kulingana na aina ya jukwaa wanalokutana nalo; Kigamboni wataambiwa hivi na Buza vile.

Hata hivyo maneno matupu hayavunji mfupa. Sera mpya hazibadilishi matakwa ya Watanzania. Wao kwa muda mrefu wamekuwa wakipambana na umaskini uliokithiri miongoni mwao.

Walitarajia viongozi wao wangekuja na sera zitakazowaondolea kadhia hiyo moja kwa moja. Badala yake wanapokea sera mpya katika kila awamu, na wamejikuta wakiingia kwenye kila awamu iliyofuatia wakiwa na hali ileile.

Hivi sasa kwenye makaratasi kiwango cha umasikini kinaonekana kushuka. Badala ya kila mtanzania kuishi kwa dola moja kwa siku, sasa masikini wa Bongo anaishi kwa dola tatu.

Kiwango hiki ni sawa na kutoka shilingi za Kitanzania Elfu Mbili Mia Tano na ushee hadi shilingi Elfu Saba Mia Nane na chenji inabaki.

Hii ni dalili kuwa sasa tumeuingia umasikini sugu. Sugu naweza kuifananisha na ganzi, yaani athari isiyobainiwa na milango ya fahamu. Masikini sugu hajui anaingiza kiasi gani, wala hajui matumizi yake ya siku.

Huku mtaani watu wasio na ajira ni wengi kuliko walioajiriwa na wale waliojiajiri. Hili unaweza kuliona kwa uchache wa ajira kwenye kila mwaka wahitimu wa vyuo wanavyoingia mtaani kutafuta kazi.

Wapangaji ni wengi kuliko wenye nyumba, nalo linaonekana kwa idadi ya nyumba za kupanga na idadi ya wapangaji kwenye nyumba moja moja.

Takwimu zinaonesha asilimia kubwa ya Watanzania ni wasio na kipato. Siku moja kituo cha Radio kinachoaminika sana na Watanzania kilifanya utafiti usio rasmi. Kiliendesha mahojiano na wakazi wa Dar es Salaam kikiwauliza bajeti zao za siku kwa wastani.

Kati ya kiasi cha watu kumi waliohojiwa, hakuna aliyetaja mahitaji yake ya kuwa chini ya Sh45,000 kila siku.

Awe anamudu au vinginevyo, hesabu hiyo ndiyo inayotosha chakula cha familia na mizunguko yake. Bila shaka hesabu iliyopigwa na kila mmoja wao ilianzia kulipokucha hadi kulipokuchwa, pale alipoinua kwato zake mpaka alipozirejesha nyumbani.

Ikumbukwe kuwa gharama za siku si chakula na nauli pekee, ni pamoja na masuala yasiyojitokeza kila siku. Kuna kodi ya nyumba na pengine ya ofisi au fremu ya biashara, mavazi, ankara za maji, simu na umeme, matibabu pamoja na dharura nyinginezo.

Kwa kuwa bajeti ya mtu inayosomeka ni ya chakula na nauli tu, gharama nyingine zote zinaangukia kwenye mikopo. Asilimia kubwa ya wafanyakazi wanaolipwa mshahara wa kima cha kati, huambulia kiasi kinachofanana na kima cha chini kwa sababu ya mikopo.

Mbaya zaidi, gharama zote za dharura huunganishwa na mikopo-umiza kama “kausha damu.” Huu ni umasikini wa kutisha kabisa.

Madhara ya umasikini huu yanaweza kutoonekana moja kwa moja. Lakini unaweza kuona mabadiliko katika maisha ya jamii tuliyomo.

Sisi ambao miaka ya nyuma tulikuwa tukiona changamoto za maradhi ya moyo, sukari, figo na msongo kuwa ni za watu wazima, hivi sasa tunaziona kwa vijana ambao ni nguvukazi ya Taifa. Vifo vya ghafla vimekuwa havistushi tena kwa kuwa vipo kila siku na kila mahala. Jukumu la viongozi wetu si kututangazia sera na dira mpya kila wakati. Bali waje na bunifu zitakazotuwezesha kukabiliana na majanga yetu.

Wachina walikuwa na dira ya muda mrefu ya kuongoza dunia kwa uchumi, na sasa ndoto zao zinatimia. Waliwekeza kuanzia kwa mtu mmoja mmoja, vikundi hadi kitaifa. Leo tunanunua bidhaa zilizotengenezwa na wajasiriamali wa Kichina kwa nembo ya Taifa lao.

Nilipita kwenye Maonyesho ya Sabasaba, vijana wa Chuo Kikuu Dar es Salaam wakanionesha ubunifu wao wa mtambo unaochenjua madini.

Jirani tu na nembo ya “Made in Tanzania” inapohamasishwa. Katika maongezi niligundua kuwa hawaijui hata hiyo nembo zaidi ya kuisikia tu. Sasa ikiwa hivyo kwa watu waliofanya maonesho chini ya paa moja, itakuwaje kwa wale walioko mbali vijijini.

Nembo iwatafute wajasiriamali, kama inasubiri wafanyabiashara ndio waitafute haitowapata. Nawaambia wazi kuwa wao hawajui watapata nini wakiitumia, na watakosa nini wakiipotezea. Inahitajika elimu maalum inayofanana na ya wahitaji maalum.

Fikiria iwapo watu wanabembelezwa kwenda kuishangilia timu yao ya Taifa, wasiohudhuria semina isiyowalipa, ni kipi kitawavuta kutumia nembo ya “Made in Tanzania”?

Hii ndiyo fursa ya wanasiasa na viongozi katika kuwatumikia wananchi. Kubuni njia mpya za kuwainua watu wao na si kubadili dira na sera ilhali watu wanazidi kuangamia.

Related Posts