Dodoma. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameendelea na mkakati wake wa kuimarisha utendaji serikalini baada ya kufanya uteuzi wa viongozi mbalimbali katika taasisi na mamlaka za umma.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa usiku wa leo Jumatano Julai 16, 2025 na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu kupitia Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka imewataja viongozi walioteuliwa katika nafasi mbalimbali ndani ya Serikali na taasisi zake.
Katika mabadiliko hayo, Omari Juma Mkangama ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Ludewa huku Juma Abdallah Njeru akiteuliwa kushika nafasi hiyo hiyo katika Wilaya ya Mpanda.
Kwa upande wa wakurugenzi wa halmashauri, Hellen Mwambeta ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, wakati Francis Kafuku akiteuliwa kushika nafasi hiyo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu.
Katika sekta ya elimu, Dk Adam Omar Karia ameteuliwa kuwa Mkuu wa Chuo cha Maji kwa kipindi cha pili. Viongozi wengine waliopata nafasi ni Balozi Aziz Mlima ambaye amekuwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Uwekezaji Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (Tiseza).
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Sharifa Nyanga, Rais Samia amemteua Mkuu wa Majeshi (CDF) mstaafu, Jenerali Venance Mabeyo kuendelea kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCCA).
Katika sekta ya afya, Dk Harrison Mwakyembe amepata nafasi ya kuendelea kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kwa kipindi cha pili.
Kwa upande wa sekta ya viwanda na biashara, Filbert Mponzi ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Sukari Tanzania kwa kipindi cha pili. Mponzi ni Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wakubwa wa Benki ya NMB.
Dk Leonada Mwagike akiteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa kipindi cha pili pia.