Rungwe yabuni mkakati kukomesha lumbesa

Rungwe. Kutokana na malalamiko ya wakulima wa viazi mviringo katika vijiji vya Ndato na Isongole wilayani Rungwe wakilalamikia wanunuzi kutumia vifungashio vikubwa vinavyojulikana kama ‘lumbesa,’ Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya imeonya na kuweka mikakati ya kudhibiti tatizo hilo.

Miongoni mwa hatua zilizopangwa ni agizo la matumizi ya vifungashio maalumu vyenye ujazo wa kilo 100, ambavyo vitatumika kupimia mazao shambani kabla ya kuingizwa sokoni.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Renartus Mchau ameyasema hayo leo Jumatano, Julai 16, 2025, wakati akizungumza na Mwananchi Digital kufuatia ongezeko la malalamiko kutoka kwa wakulima licha ya Serikali kuwa tayari imeshapiga marufuku matumizi ya ‘lumbesa.’

Mchau amesema hivi karibuni wamepokea malalamiko kuhusu wanunuzi wanaoingia shambani wakiwa na magunia yenye ujazo mkubwa, maarufu lumbesa, hali iliyowalazimu viongozi wa halmashauri kufika na kufanya mikutano ya hadhara katika vijiji vinavyozalisha zao hilo ili kueleza mikakati ya Serikali.

“Sasa ni msimu wa mavuno ya viazi mviringo. Tuliwaeleza wakulima na wanunuzi kuhusu malengo ya Serikali na suluhisho la kuanza kutumia vifungashio maalum vya ujazo wa kilo 100, ambavyo vitatumika rasmi,” amesema Mchau.

Mkurugenzi  Halmashauri  ya Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya, Renatus  Mchau  akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Jumatano Julai 16,2025. Picha na Hawa Mathias.



Amefafanua kuwa katika kutekeleza mpango huo, tayari wamehusisha Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) kwa lengo la kuondoa migongano na malalamiko kati ya wakulima, wanunuzi na wafanyabiashara.

Sikujua Amos, mkulima kutoka Kijiji cha Isongole, amesema changamoto kubwa ni upungufu wa wanunuzi wakati wa msimu wa mavuno, hali inayowapa nguvu kutumia mbinu za kuwakandamiza wakulima.

“Tunagombana sana na wanunuzi mashambani. Wanakuja na mifuko mikubwa na kuongeza juu plastiki tatu za kilo 20 kwa mtindo wa lumbesa, jambo linalotuumiza sana,” amesema Amos.

Ameomba Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe aendelee kusisitiza marufuku ya ununuzi wa viazi mviringo kwa mfumo huo na kuwe na ukaguzi wa magari yanayosafirisha mazao hayo.

“Tuna imani na Waziri wetu wa Kilimo. Sisi wakulima tunateseka sana. Tunatumia gharama kubwa kuzalisha lakini mwisho wa siku faida inachukuliwa na madalali,” amesema.

Naye Daniel Naftari amesema changamoto nyingine ni wanunuzi kutumia madalali ambao huwanyima wakulima fursa ya kupata bei yenye haki, kwa kuwa wanapanga bei bila kuzingatia gharama za uzalishaji.

Historia ya marufuku ya lumbesa

Serikali ilipitisha rasmi marufuku ya matumizi ya vifungashio vya ujazo au uzito mkubwa vikiwamo vya lumbesa, tangu mwaka 2016. Sheria ya Vipimo Sura Na. 320 inakataza mbinu hiyo katika bidhaa kama dagaa, viazi na vitunguu.

Sheria hii inalenga kudhibiti vitendo vya udanganyifu vinavyofanywa na baadhi ya wafanyabiashara na taasisi dhidi ya wakulima na wazalishaji wa bidhaa hizo, kwa kuhakikisha mizani na vipimo sahihi vinatumika katika biashara.

Related Posts