Sababu Tanzania kuagiza asilimia 60 ya dawa India

Tabora. Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imesema ongezeko la viwanda vya dawa nchini limechangia asilimia 30 ya matumizi ya nchi kupatikana ndani, huku ikitaja sababu ya asilimia 60 ya dawa zinazotumika kununuliwa India.

Tanzania imefikia hatua hiyo mwaka 2025 kutoka asilimia 10 hadi 20 mwaka 2020, hivyo kupunguza utegemezi wa uagizaji wa dawa kutoka nje ya nchi.

Hayo yamesemwa leo Jumatano, Julai 16, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo wakati wa kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari wa mikoa ya Dar es Salaam, Tabora, Kigoma na Katavi.

“Tunadhani labda tumesogea kufikia asilimia 30 ya matumizi yetu tunazalisha ndani, lakini bado tunakazi ya kufanya Kenya wanaongoza kwa uzalishaji wa ndani, Uganda inafuata sisi bado, sekta hii inahitaji uwekezaji zaidi ili kuongeza idadi ya viwanda ndani ya nchi,” amesema Fimbo.

Hata hivyo, kwa mwaka 2020 ni asilimia 10 mpaka 20 ya dawa ndizo zilizokuwa zinazalishwa katika viwanda vya ndani na mpaka kufikia 2025 imefikia asilimia 30.

Takwimu za awali zinaonesha Tanzania inategemea kuagiza dawa nje kwa asilimia 80 na katika mchanganuo asilimia 60 ya dawa zinazoagizwa nje zinatoka India, asilimia 19 China, asilimia 10.6 Ulaya, asilimia 9.2 Afrika na asilimia 0.83 zinatoka Amerika.

Alipoulizwa sababu za asilimia 60 ya dawa kuagizwa India, Fimbo amesema nchi hiyo ni ya kwanza duniani kwa kuwa ina viwanda vingi vya dawa za viambata hai.

“Viambata hai vinatengenezwa duniani na nchi tatu India, China na Ujerumani, viambata hai ndiyo vinaenda kutengeneza dawa ni kama malighafi ili uweze kutengeneza dawa, ukikuta kidonge cha ‘paracetamol’ kina vitu vingi lakini ile dawa yenyewe inatoka huko.

“Hii inawasaidia India kuwekeza sana kwenye sekta ya dawa na wamejenga maeneo mengi sana na sasa wanatafuta masoko ya nje na ndiyo maombi mengi tunayopokea, kaguzi nyingi zinafanyika India kwakuwa wameshawekeza sana kwenye sekta inauzwa hapa na kote duniani,” amesema Fimbo.

Mkurugenzi wa Dawa, TMDA Dk Hebron Yona amesema India anauza dawa zake kwa gharama nafuu kwa kuwa malighali anazo ikilinganishwa na nchi zingine ambazo zikitaka kuzalisha malighafi huagiza nje.

“India ana viwanda vya dawa zinazokubalika katika masoko mbalimbali na ndiyo sababu kubwa iwe tegemeo kubwa, kama nchi lazima tupunguze utegemezi ili kuokoa fedha za kigeni lakini pia majanga yakitokea viwanda vinaweza kutusaidia,” amesema.

Awali, akitoa mada kuhusu mchango wa TMDA katika kutekeleza sera ya viwanda nchini amesema  uanzishwaji wa viwanda vya dawa kutoka 13 mwaka 2020 mpaka 18 mwaka 2025 umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama ya kuagiza dawa nje ikiwemo majitiba.

Amesema wataendelea kuvilinda viwanda vya dawa vya ndani na kwa kuzingatia ubora kwani kiwanda chochote kilichokaguliwa na TMDA ni salama, bora na kina ufanisi.

“Tutashirikiana na wazalishaji kuhakikisha malighafi inaingizwa ina ubora na dawa zinavyozalishwa hatua zote tutakuwa na taarifa nazo, ikiwemo dawa za ARV zinazotarajiwa kuanza kuzalishwa nchini,” amesema Dk Yona.

Akielezea mafanikio amesema kumekuwa na ongezeko la idadi ya usajili wa dawa kutoka 722 mwaka 2020 hadi 990 mwaka 2025, viwanda vya tiba na vitendnaishi imesajiliwa kutoka bidhaa tano mpaka 22 mwaka 2025.

“Viwanda vimeanza kuzalisha na kuuza ndani na nje ya nchi. Kwa upande wa majitiba wameuza nje ya nchi Sh3.5 bilion na vidonge na dawa za maji na kupaka Sh2.8 bilioni.

Awali, akifungua mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha amesema mafanikio yaliyoonekana inaonyesha wazi taasisi inafanya kazi zake kama ambavyo inatakiwa akitolea mfano wa kutoa gawio la Sh23 bilioni kwa Serikali kwa mwaka 2025.

Amesema kwa kiasi kikubwa kwa mkoa wa Tabora wametoa matangazo kuhusu matumizi ya dawa kinyume na sheria.

“TMDA haiwezi kufanikisha majukumu yake bila uwepo wa vyombo vya habari ili kutoa elimu kwajamii namna ya kubaini dawa bandia, vita dhidi ya bidhaa bandia na zisizo na viwango hivyo kutokuwa salama kwa jamii, elimu zaidi inatakiwa kutolewa kwa jamii,” amesema Chacha.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora (RMO), Dk Honoratha Rutanisibwa amesema wamekuwa wakishirikiana na udhibiti uuzaji wa dawa holela na ambazo hazijasajiliwa na zisizo na ubora na panapokiwa na ukiukwaji hatua zimekuwa zinachukuliwa ili kulinda afya ya jamii.

“Pia, tunashirikiana na timu kuhakikisha tunatoa elimu kwa jamii kuhusu matumizi sahihi dawa, pia tumekuwa tukipita katika vituo vya afya na kuangalia vifaa vilivyokwisha muda wake ili viweze kuteketezwa na kutoa elimu ya utumiaji mzuri wa dawa wananchi kutumia kwa usahihi,” amesema.

Related Posts