Dar es Salaam. Baraza la Mawaziri chini ya Rais Samia Suluhu Hassan linahitimisha safari yake ya utumishi wa miaka minne, huku likiacha kumbukumbu sita za pekee, ikiwemo teua tengua 15 na kuanza bila ya Makamu wa Rais.
Safari ya baraza hilo ilianza Machi 19, 2021, saa chache baada ya Rais Samia kuapishwa kuwa mkuu wa nchi, ikiwa ni siku mbili tangu alipofariki mtangulizi wake, Dk John Magufuli Machi 17, 2021, katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam, baada ya kuugua ugonjwa wa moyo.
Ilichukua wiki mbili kwa Samia kufanya mabadiliko katika baraza la mawaziri yaliyoingiza sura mpya, huku wengine wakihamishwa kutoka eneo moja kwenda lingine.
Wadau wa siasa na utawala wanasema upekee wa baraza hilo unatokana na historia yake ya mabadiliko ya mara kwa mara, umachachari wa mawaziri husika na mageuzi ya wizara.
Licha ya jana Jumatatu Julai 14, 2025, Rais Samia kufanya kikao cha mwisho cha Baraza la Mawaziri, Ikulu ya Chamwino, anaweza kuliitisha muda wowote au kufanya mabadiliko kwa mujibu wa Katiba.
Upekee wa baraza hilo unatokana na idadi kubwa ya mabadiliko yaliyofanywa. Ndani ya miaka minne, yamefanyika mabadiliko 15 yanayohusisha kuhamishwa kwa mawaziri, kutenguliwa na kuteuliwa wapya.
Ingawa Rais Samia amewahi kueleza kuwa sababu ya mabadiliko ya mara kwa mara katika baraza hilo ni kulinyoosha Taifa, wanazuoni wanasema hali hiyo inawaondolea wateule hali ya kujiamini na ubunifu.
Akizungumza katika kongamano la wanawake wa Kiislam visiwani Zanzibar, Julai 16, 2023, Rais Samia alisema anachokiangalia katika uamuzi huo ni kiongozi anayefanya vizuri na asiyefanya vema.
“Tustahimili kuumia kwa mwanao kuondoka, mdogo wako kuondoshwa, tustahimili kuumia ili Taifa linyooke. Vinginevyo tunyooshane tangu nyumbani ili anayepewa dhamana asiwe na mkono mkono.”
“Asifanye uzembe akaacha kazi, akatoka akaenda vijiweni. Sisi wakubwa huwa hatustahimili hayo, tuna mambo makubwa. Tumetoa ahadi ndani na kimataifa, tunataka wasaidizi wetu hawa watusaidie,” alisema.
Katika baraza hilo, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ndio wanaoshikilia rekodi ya kuhudumu katika wizara moja kwa kipindi chote cha miaka minne, tangu walipoteuliwa.
Dk Nchemba aliteuliwa Machi 31, 2021, katika mabadiliko ya awali ya baraza la mawaziri yaliyotangazwa na Rais Samia wiki mbili baada ya kuapishwa kushika wadhifa huo.
Kabla ya wadhifa huo, Dk Nchemba alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria katika baraza la mawaziri lililokuwa chini ya hayati Magufuli.
Uteuzi wa Dk Nchemba uliziba nafasi iliyoachwa wazi na Dk Philip Mpango aliyependekezwa na kupitishwa na Bunge kuwa Makamu wa Rais.
Kwa upande wa Aweso, ndiye waziri anayeshikilia rekodi ya kuiongoza wizara hiyo bila kiapo kutoka kwa Rais Samia. Waziri huyo aliteuliwa na Magufuli Desemba 5, 2020, na hajawahi kuondolewa hadi sasa.
Ingawa Rais Samia alifanya mabadiliko 15 katika baraza hilo, mawaziri hao hawakuwa sehemu ya walioguswa, ama kwa kuhamishwa au kutemwa kabisa.
Katika baraza hilo, wapo mawaziri waliohudumu katika wizara nyingi zaidi kutokana na kuhamishwa, akiwemo Mohamed Mchengerwa aliyehudumu wizara nne.
Mchengerwa aliingia katika baraza hilo akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi). Mwaka mmoja baadaye alibadilishwa kuwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Alidumu katika nafasi hiyo hadi Februari 2023, alipoteuliwa katika Wizara ya Maliasili na Utalii, alikotumikia kwa miezi kadhaa hadi Agosti mwaka huo huo, kisha akarudishwa tena Tamisemi mpaka sasa.
Mwingine ni Dk Pindi Chana, aliyeanza kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, kisha Februari 2023 akateuliwa kuwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Septemba mwaka huo, Dk Pindi aliteuliwa tena kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, kisha akahamishwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, wadhifa alionao hadi sasa.
Innocent Bashungwa naye anaingia katika anga hizo, akihudumu wizara nne kwa kipindi hicho cha miaka minne, sawa na wastani wa wizara moja kila mwaka.
Bashungwa aliingia katika baraza hilo la Rais Samia akiwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Oktoba 2022, akahamishiwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Septemba 2023, Bashungwa aliteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi, wadhifa aliodumu nao hadi Desemba 2024, kisha akahamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Anayefuatia ni Dk Damas Ndumbaro, ambaye amehudumu wizara tatu tofauti. Alianza kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Septemba 2021, kisha Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, na baadaye Wizara ya Katiba na Sheria.
Wapo wanasiasa waliojikuta si sehemu ya wanaohitimisha safari ya miaka minne ya baraza hilo, akiwemo Ummy Mwalimu, January Makamba na Nape Nnauye.
Uwaziri wa Makamba ulikoma Julai 21, 2024, akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, nafasi yake ilirithiwa na Mahmoud Thabit Kombo.
Siku hiyo hiyo, Nape aliyekuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari naye aliondolewa.
Kwa upande wa Ummy, wadhifa wake ulikoma Agosti 15, 2024, akiwa Waziri wa Afya, nafasi hiyo aliteuliwa Jenista Mhagama anayehudumu hadi sasa.
Balozi Liberata Mulamula ni waziri mwingine aliyeishia njiani, aliteuliwa kuwa mbunge na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, wadhifa uliokoma Oktoba 3, 2022.
Wizara mpya, zilizobadilishwa majina
Katika kipindi cha miaka minne, Rais Samia alianzisha Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu Januari 11, 2022, na Dk Dorothy Gwajima kuwa waziri wake wa kwanza.
Agosti 30, 2023, Rais Samia alianzisha nafasi ya Naibu Waziri Mkuu na kumteua Dk Doto Biteko kushika nafasi hiyo, huku akiendelea kuwa Waziri wa Nishati.
Desemba 8, 2024, Rais Samia alihamisha majukumu ya sekta ya habari kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwenda Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, na Profesa Kabudi kuwa waziri wake.
Baraza bila Makamu wa Rais
Rais Samia alifanya kikao cha kwanza cha baraza la mawaziri Machi 19, 2021, saa chache baada ya kula kiapo, likiwa halina Makamu wa Rais.
Hiyo ni kutokana na kuwa ndiye aliyekuwa na wadhifa huo kabla ya kuapishwa kuwa Rais, hivyo ilimpasa kupendekeza jina la atakayemrithi kwa ajili ya kupigiwa kura bungeni.
Katika mchakato huo, jina la aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango, lilichomoza na kupitishwa na Bunge, kisha kuapishwa kuwa Makamu wa Rais, Machi 21, 2021.
Akizungumzia baraza hilo, Mhadhiri wa Rasilimali Watu na Utawala wa Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (Tudarco), Dk Lazaro Swai anasema upekee wa baraza hilo unatokana na tengua tengua zilizokithiri.
Ingawa tengua hizo zilionekana kuathiri kujiamini kwa wateule, anasema kwa upande mwingine zilijenga msingi wa kujisimamia, nidhamu na uwajibikaji.
“Ni baraza lililokuwa na tengua tengua nyingi. Nakumbuka lililopita lilikuwa na mambo ya kutumbuana hadharani, lakini hili ilikuwa kimyakimya, mnakutana na mkeka tu. Yote ni kuwajibishana,” anasema.
Anaongeza kuwa katika kipindi cha baraza hilo, kulishuhudiwa mabadiliko ya baadhi ya miundo ya wizara, ikiwemo ya Afya na Ujenzi, jambo alilosema lina tija katika kuongeza ufanisi wa kiutendaji.
Anasema ilitarajiwa kwamba ni mawaziri wachache tu ndio wangetoboa kuitumikia wizara moja kwa miaka yote minne.
Sura ya baraza linalomaliza
Ukiacha Rais Samia, Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi, Makamu wa Rais Dk Mpango na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, baraza hilo linahitimisha safari yake likiwa na sura mpya na za zamani.
Baraza hilo linajumuisha Dk Doto Biteko (Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati), Kapteni George Mkuchika (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu) na George Simbachawene (Waziri wa Nchi, Utumishi na Utawala Bora)
Pia wamo, Profesa Kitila Mkumbo (Waziri wa Mipango na Uwekezaji), Profesa Palamagamba Kabudi (Waziri wa Habari, Sanaa na Utamaduni), na Ridhiwani Kikwete (Waziri wa Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu).
Pamoja na hao, pia huyo, Dk Selemani Jafo (Waziri wa Viwanda na Biashara), Balozi Mahmoud Kombo (Waziri wa Mambo ya Nje ba Ushirikiano wa Afrika Mashariki), Profesa Makame Mbarawa (Waziri wa Uchukuzi), Innocent Bashungwa (Waziri wa Mambo ya Ndani), Dk Mwigulu Nchemba (Waziri wa Fedha), Hamad Masauni (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira) na Jenista Mhagama (Waziri wa Afya).
Yumo pia Dk Stergomena Tax (Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), Hussein Bashe (Waziri wa Kilimo), Abdallah Ulega (Waziri wa Ujenzi), Profesa Adolf Mkenda (Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia), William Lukuvi (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu), Jerry Silaa (Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari), na Dk Damas Ndumbaro (Waziri wa Katiba na Sheria)
Wengine ni Dk Dorothy Gwajima (Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu), Dk Ashatu Kijaji (Waziri wa Mifugo na Uvuvi), Jumaa Aweso (Waziri wa Maji), Dk Pindi Chana (Waziri wa Maliasili na Utalii), Mohamed Mchengerwa (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa) na Anthony Mavunde (Waziri wa Madini).