Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, leo tena anapanda kizimbani, Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, kwa ajili ya shauri lake la maombi ya jinai alilolifungua mahakamani hapo.
Lissu anakabiliwa na kesi ya kuchapisha taarifa za uwongo katika mtandao wa YouTube, kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 14 ya mwaka 2015.
Kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mhini imeshaanza kusikilizwa ushahidi wa upande wa mashtaka ambapo tayari shahidi mmoja ameshatoa ushahidi wake.
Kabla ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa ushahidi, upande wa mashtaka ulifungua maombi mahakamani hapo (Kisutu) ukiomba mahakama hiyo iamuru baadhi ya mashahidi wake kutokuwekwa wazi wakati wakitoa ushahidi kwenye kesi hiyo wala taarifa za utambulisho wake kuwekwa wazi.
Lissu kupitia mawakili wake wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo ya Jamhuri waliyapinga pamoja na mambo mengine wakidai kuwa upande wa mashtaka haukutoa sababu za msingi za kuomba mashahidi wake wasiwekwe wazi.
Hata hivyo, mahakama hiyo katika uamuzi wake ilikubaliana na hoja za Jamhuri na kuruhusu mashahidi hao waliobainishwa kutoa ushahidi wao katika hali ya uficho, uamuzi ambao Lissu hakuridhika nao ndipo akafungua shauri hilo la mapitio ya Mahakama.
Katika shauri hilo linalosikilizwa na Jaji Elizabeth Mkwizu, Lissu anaiomba mahakama hiyo iitishe jalada la kesi hiyo kuchunguza mwenendo na uamuzi huo kujiridhisha na uhalali na usahihi wake na hatimaye iutengue.
Shauri hilo lilitajwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Juni 27, 2025, ambapo mahakama ilitoa muda wa siku 14 kwa mjibu maombi (Jamhuri) kuwasilisha majibu yake yake ya utetezi dhidi ya maombi hayo, ambapo aliitaka kuwasilisha majibu hayo Julai 8, 2025.
Pia Jaji Mkwizu alielekeza upande wa mwombaji kuwasilisha majibu ya hoja za mjibu maombi jana, Julai 15, na akapanga shauri hilo litajwe leo kwa ajili maelekezo muhimu, kuhusiana na usikilizwaji.
Katika kesi hiyo Lissu anakabiliwa na mashtaka matatu. Katika mashtaka hayo Lissu anadaiwa kumhusisha Rais wa Jamhuri ya Muungamo wa Tanzania na kutenguliwa kwa wagombea chama chake katika maeneo mbalimbali wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, 2024.
Pia, anadaiwa kuwatuhumu askari Polisi kuhusika katika wizi wa kura kupitia vibegi na majaji kutokutenda haki kwa madai ya kutaka wapate uteuzi wa Rais kuwa majaji wa Mahakama ya Rufani.
Anadaiwa kutenda makosa hayo Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam, kwa nia ya kulaghai umma.
Alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Kisutu kwa mara ya kwanza na kusomewa mashtaka hayo Aprili 10, 2025.