Simba, Azam zachemka kwa Maxi, ishu nzima ipo hivi

KAMA kuna kitu ambacho mashabiki wa Yanga wanapaswa kukifurahia, basi ni uamuzi uliotolewa juu ya nyota wao, Maxi Nzengeli ambaye amekuwa akifukuziwa na wapinzani wao, Simba na Azam.

Ipo hivi; kuna kauli ambayo vigogo wa Maniema ya DR Congo wamewaambia viongozi wa klabu hizo kimyakimya siku chache zilizopita ambayo haijawafurahisha.

Siyo hao tu. Hata Kocha wa Ismailia ya Misri, Miloud Hamdi aliyeanza kazi rasmi hivi karibuni kuna kitu alijaribu kufanya kimafia Yanga akachemka na kuamua kurudi nyuma.

Timu hizo zote zinawinda saini ya Maxi Nzengeli ambaye mkataba wake na Yanga umemalizika hivi karibuni ambapo na wao wako kwenye harakati za kumbakisha kwa donge nono. 

Iko hivi, duru za usajili zinaeleza kwamba Simba na Azam zilisharusha karata kwa Maxi kwa nyakati tofauti hivi karibuni kupitia wakala wake pamoja na viongozi wa klabu yake ya Maniema lakini wakakutana na jibu la kuhuzunisha.

Maniema ambayo inammiliki Maxi kihalali, imewajibu kwamba kwa Tanzania hawezi kucheza nje ya Yanga anayoitumikia kwa mkopo kwani hawataki uhasama utakaoharibu kipaji cha mchezaji huyo. Habari zinasema kwamba Maniema imewaambia kama wanamtaka wasubiri aende nje ndipo arudi Tanzania kwa namna nyingine.

Kocha mpya wa Azam, Florent Ibenge ni swahiba mkubwa wa Maxi anayetajwa kumshawishi mara kadhaa lakini akakwama na kumfanya atafute mbadala mwingine DR Congo ambayo tayari ameshamalizana nao.

Miloud aliyeipa Yanga makombe matatu msimu uliopita akiinoa kwa takribani miezi sita pekee, aliwaambia viongozi wa Ismailia kwamba wafanye wafanyavyo wamletee mashine moja kutoka pale Yanga.

Kocha huyo amewaambia kwamba anamtaka kiraka Maxi Nzengeli kwenye kikosi chake cha msimu ujao ingawa vita ni kubwa.

Ameenda mbali zaidi kwa kuwahakikishia kwamba staa huyo bado hajasaini mkataba mpya Yanga ndipo mabosi hao wakawasiliana na Maniema ya DR Congo inayotajwa kummiliki staa huyo na kuwapa ofa ya dola 300,000 (zaidi ya Sh700).

Habari za uhakika zinasema Maniema na Ismailia wako kwenye mazungumzo ya wiki kadhaa sasa lakini wamepewa sharti moja ambalo limewawia gumu na ndilo ambalo linaweza kumbakiza Maxi Yanga.

Mabosi wa Maniema ambao walikuwa Dar es Salaam hivi karibuni, wamewaambia Ismailia kwamba wanataka dau lote la dola 300,000 na si kulipwa kwa mafungu matatu kama Waarabu hao wanavyoomba.

“Maxi hajasaini Yanga na Maniema wako tayari kumuuza Kwa Klabu yoyote ya nje ya Tanzania. Hamdi amewaambia Ismailia kwamba anamtaka na akawaelekeza wazungumze na Maniema.

“Viongozi wake wakapeleka ofa wakakubaliwa, changamoto ikaja kwenye mfumo wa malipo. Wameomba kulipa kwa mikupuo mitatu, Maniema wamekataa. Wamewaambia waweke fedha yote wamalize biashara kwa mkataba wa miaka mitatu,” kilisema chanzo cha kuaminika.

Habari zinasema kwamba Ismailia bado wanaendelea kubembeleza ingawa Yanga nao wamepiga simu Maniema wakiahidi kumpa staa huyo mkataba mpya muda wowote.

“Maniema wanaamini wakimuuza nje watapata fedha nyingi zaidi na hawataki kumuuza Kwa Simba wala Azam au Klabu yoyote ya Tanzania kutokana na siasa na uhasama ambao wanaamini upo baina ya timu hizo unaoweza kumaliza kiwango cha mchezaji huyo,” aliongeza.

Nzengeli msimu uliopita alimaliza na mabao sita na asisti kumi akicheza mechi 26 kwa dakika 1,806, huku ule wa 2023/23 alikuwa na mabao 11, asisti mbili akicheza kwa dakika 2090.

Related Posts