Mbeya. Mwanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) kutoka Mkoa wa Songwe, Nkunyutila Siwale, amechukua na kurejesha fomu ya kuomba kuteuliwa na chama hicho kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Zoezi hilo lilifungwa jana, Julai 15, likihitimishwa na wawaniaji wawili kutoka ukanda wa Nyanda za Juu Kusini na hivyo kufikisha jumla ya wagombea sita waliojitokeza kuwania nafasi hiyo kupitia CUF.
Siwale (70), mkazi wa Mbozi, amejiunga na watiania wengine watano ambao ni Rose Kahoji (Mbeya), Lutayosa Yemba (Mwanza), Gombo Samaditto (Geita), pamoja na Masoud Hamad Masoud na Habibu Mohamed Mnyaa wote kutoka Pemba.
Akizungumza leo Julai 16, Mwenyekiti wa chama hicho Nyanda za Juu Kusini, Yassin Mrotwa amesema idadi hiyo inaakisi kuwapo kwa demokrasia ndani chama na kutoa fursa kwa wanachama wake.
Amesema pamoja na idadi hiyo, kanda hiyo inajivunia zaidi kupata watiania wawili katika nafasi hiyo ya juu na kwamba matarajio yao ni kufanya vizuri katika uchaguzi mkuu mwaka huu.
“Hakuna kingine zaidi ya kukua kwa demokrasia ndani ya chama na uhuru kwa wanachama, katika idadi hiyo, kanda yangu imekuwa na wanachama wawili waliojitosa, hii ni hatua kubwa” amesema Mrotwa.
Kiongozi huyo ameongeza kuwa kwa sasa zoezi la uchukuaji na urejeshaji fomu limefungwa ambapo kwa upande wa Mkoa wa Mbeya majimbo yote yamepata watia nia sawa na nafasi za udiwani.
Amesema hatua iliyobaki ni kwa Baraza Kuu la Chama hicho Taifa kufanya mchujo na kuteua wagombea akibainisha kuwa matarajio ni kusimamisha wagombea wenye sifa na wenye kukubalika kwa wananchi.
“Tumefunga zoezi hilo jana Julai 15, muitikio ulikuwa mkubwa kwa wanachama, Jimbo la Uyole amechukua Mwanasheria Rafael Ngonda huku Mbeya Mjini nikiwa mimi, kiufupi majimbo yote yanao watia nia na madiwani wapo, ” amesema Mrotwa.