Stars kutesti mitambo na Kenya, Uganda

Kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kinatarajiwa kushiriki mashindano ya CECAFA yaliyoandaliwa maalum kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN).

Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Shirikisho la Soka Ukanda wa Afrika Mashariki (CECAFA), yamepewa jina la CECAFA 4 Nations Tournament yatakayoshirikisha timu nne yakipangwa kufanyika kuanzia Julai 21 hadi 27, mwaka huu kwenye Uwanja wa Black Rhino Academy uliopo Karatu jijini Arusha.


Kwa mujibu wa taarifa kutoka CECAFA, mashindano hayo yatajumuisha mataifa ya Tanzania, Uganda, Kenya na Congo Brazzaville, lengo ni kuzipa maandalizi kabla ya mashindano ya CHAN 2024.

CECAFA imeamua kuziandaa timu za ukanda wake ambazo zinashiriki CHAN 2024 kabla ya mashindano kuanza Agosti 02 hadi 30, 2025 yakifanyika Tanzania, Kenya na Uganda.


Kwa sasa Taifa Stars ipo Misri ikiendelea na kambi iliyoanza Julai 7 mwaka huu jijini Dar es Salaam ikijiandaa na michuano ya CHAN itakayofanyika nchi tatu za Tanzania, Kenya na Uganda kuanzia Agosti 2 hadi 30, mwaka huu.

Michuano ya CHAN itashirikisha timu za taifa kutoka nchi 19, ambapo Kundi A mechi zake zitachezwa kwenye Uwanja wa Kasarani nchini Kenya, zikishirikisha Kenya, Morocco, Angola, DR Congo na Zambia, huku kundi B zikichezwa Dar es Salaam, zikiundwa na Tanzania, Madagascar, Mauritania, Burkina Faso na Jamhuri ya Afrika ya Kati.


Mechi za kundi C ambazo zitachezwa Uganda, zitashirikisha Uganda, Niger, Guinea, Afrika Kusini na Algeria, huku kundi D ambalo mechi zake zitapigwa kwenye Uwanja wa Amaan Complex visiwani Zanzibar, litashirikisha Senegal, Congo, Sudan na Nigeria.

Related Posts