Hivi karibuni, picha za wawakilishi wa Papua New Guinea wakiwa Umoja wa Mataifa (UN) au mikutano mingine ya kimataifa kama COP (Conference of the Parties) zimekuwa gumzo mitandaoni kwa namna ya mwonekano wao wa kiutamaduni katika uwakilishi wao kimataifa.
Papua New Guinea ni moja kati ya maeneo yenye urithi wa kipekee zaidi duniani. Kisiwa hicho kilichopo katika eneo la Pasifiki, makabila yao yanatahimi mila na desturi zakei huku ikikadiriwa kuwa na watu takribani milioni 10 kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa mwaka 2024.
Watu wa Papua New Guinea wanaishi maisha yanayoakisi mila zao, na wanajivunia zaidi kuenzi tamaduni hizo, kiasi cha kuvaa na mavazi yao ya asili hata wanapofanya uwakilishi katika majukwaa rasmi ya mikutano ya kimataifa jambo ambalo limekuwa likiwaacha wageni midomo wazi wanapowaona.

Mojawapo ya hatua kubwa ni namna ambayo watu wa Papua New Guinea wanaenzi utamaduni wao ni kupitia mavazi ya jadi. Mavazi hayo mara nyingi hutengenezwa kwa kutumia manyoya ya ndege wa asili, nywele, majani, ngozi za wanyama na mapambo ya asili.
Katika sherehe mbalimbali za jadi maarufu ‘sing-sing’ ni tamasha ambalo makabila hukutana na kuonyesha nyimbo, ngoma na mavazi yao.

Hii siyo tu njia ya kusherehekea utamaduni wao bali pia ni njia ya kuendeleza urithi wa mababu zao waliowaachia.
Kile kinachoishangaza zaidi ni namna ambavyo utamaduni wao umeendelea kuheshimiwa hata wakati wa uwakilishi wa kitaifa katika mikutano ya kimataifa kama vile Umoja wa Mataifa (UN).
Wawakilishi kutoka Papua New Guinea mara kadhaa wamehudhuria mikutano ya UN wakiwa wamevaa mavazi ya jadi badala ya suti za kisasa kama ilivyo kwa wengine.
Hili ni jambo la kipekee linaloonyesha uzito wanaoupa urithi wao wa kitamaduni. Kwao, kuvaa mavazi ya asili ni kutangaza asili yao, kuieleza dunia kuhusu utambulisho wao wa kiutamaduni, na kuonyesha kuwa maendeleo hayaondoi thamani ya mila.

Uwakilishi wao katika mikutano wamekuwa wamekuwa na mwonekano wakiwa wamepaka rangi usoni, wamevaa manyoya ya ndege wa rangi, na mapambo ya jadi, ujumbe wao ukiashiria kwamba “Hatuhitaji kuacha utamaduni wetu ili kuwa sehemu ya dunia ya kisasa.” Hii imewapa heshima kubwa kimataifa na kuchochea mataifa kujua kwa kina kuhusu asili yao.
Mbali na mavazi, lugha za asili bado zinazungumzwa kwa kiasi kikubwa nchini humo. Serikali ya Papua New Guinea inahamasisha matumizi ya lugha za asili katika elimu ya awali na pia kupitia vyombo vya habari vya kitaifa. Aidha, wasanii, wanamuziki, na wachoraji wa huko huunda kazi za sanaa zinazobeba maudhui ya kitamaduni, ambazo huuzwa hata nje ya nchi.
Papua New Guinea ni miongoni mwa mataifa machache duniani ambayo yameamua kukumbatia asili yake na utamudani wa nchi yao katika zama za utandawazi.
Wananchi wake wameonyesha kuwa maendeleo ya kiuchumi na ushiriki wa kimataifa haviwezi kuwa sababu ya kufuta asili ya jamii. Hivyo Papua New Guinea wanatumia kila fursa, hata majukwaa ya kimataifa, kutangaza urithi wao.