Utata Sh87 bilioni za mwekezaji Simba

MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi na Rais wa Heshima wa Simba, Mohammed Dewji ‘MO’ usiku wa Julai 14, 2025, alitumia muda huo kuzungumza na Wanasimba na wapenda soka kwa jumla huku akitaja mambo mbalimbali yanayoendelea ndani ya klabu hiyo ikiwemo suala la uwekezaji wake.

Mo ambaye hii ni mara ya pili anafanya hivyo katika akaunti yake ya Instagram baada ya awali Juni 11, 2024 kuzungumza, alisema klabu hiyo itarudi kwa nguvu msimu ujao, huku akitangaza maboresho ya kikosi.

Akizungumzia mchango wake Simba, bilionea huyo alisema kuanzia mwaka 2018 hadi sasa ametumia kiasi cha Sh87 bilioni kwa matumizi mbalimbali ya klabu hiyo.

Katika mchanganuo wa fedha hizo, Mo alisema ametumia Sh45 bilioni kulipa mishahara, kufanikisha usajili, maandalizi ya timu na uendeshaji.

Tajiri huyo alisema pia ameweka Sh20 bilioni kama sehemu ya ununuzi wa hisa asilimia 49 za mwekezaji Simba. Pia ametumia Sh22 bilioni kuanzia 2017 hadi 2024 kwenye misaada mbalimbali pale ambapo imekuwa ikihitajika Simba.

“Kusema Mo hatoi fedha hiyo ni kauli ya kupotosha yenye mwelekeo wa chuki. Tuachane na fitina Wanasimba wenzangu, tuzibe panapovuja, tuzibe ufa,” alisema Mo.

“Msimu ujao tunarejea kwa nguvu mpya, kipaumbele chetu kikubwa kitakuwa kwenye usajili makini na wa kimkakati tukilenga kuleta wachezaji bora watakaoongeza ushindani bora na kina katika kikosi, sambamba na hilo tutaongeza nguvu kwenye benchi la ufundi ili kuhakikisha timu yetu inapata mwongozo sahihi wa kufikia mafanikio, nimetenga fedha za kutosha kuhakikisha timu yetu inakuwa bora zaidi,” alisema Mo.

Simba iliyomaliza nafasi ya pili kwenye ligi na Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kupoteza fainali mbele ya RS Berkane, malengo ya Mo ni kuona siku moja timu hiyo inakuwa bingwa wa Afrika.

“Msimu huu haukuwa rahisi, tumepitia changamoto nyingi lakini tumeonesha uimara mkubwa, leo hii Simba inashikilia nafasi ya tano kwenye viwango vya CAF huku bado tukiwa katika mchakato wa kujenga upya kikosi chetu, ni mafanikio ya kujivunia kwa klabu iliyokuwa nafasi ya 85 mwaka 2017/18 wakati uwekezaji ulianza, Simba imeendelea kuandika historia.

“Ni klabu pekee kutoka Tanzania kufika fainali ya CAF mara mbili ingawa hatukutimiza kila lengo tumeonesha dhamira tukipambana kwa heshima na moyo wa Simba, bado ndoto yangu ni ileile kuipa Simba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika.”

Wakati Mo akibainisha kutumia kiasi cha Sh87 bilioni ndani ya Simba kipindi hicho, kuna maswali kibao yamebaki vichwani mwa wadau wengi wa soka wakihoji bajeti, mikataba ya udhamini na fedha za mafanikio inazopata timu hiyo kwenye mashindano mbalimbali zinafanya kazi ipi.

Mbali na hilo, pia fedha za viingilio vya mlangoni ambavyo Simba imekuwa na rekodi nzuri ya kujaza viwanja ikiwemo Benjamin Mkapa, mapato yanakwenda wapi.

Swali lingine ambalo wengi wanajiuliza, kama Mo anatoa fedha za usajili kisha haoni mabadiliko huku akiahidi kuendelea kutoa, viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia usajili wanawajibikaje, kwa nini asiwawajibishe kwa kushindwa kufikisha malengo yake na klabu kwa jumla.

Ukiangalia msimu uliomalizika, Simba ilisajili wachezaji 14 wapya na hadi sasa kati ya hao wapya, imeachana nao watatu ambao ni Valentine Nouma, Augustine Okejepha na Kelvin Kijili, huku mmoja ikimtoa kwa mkopo Omary Omary.

Hata hivyo, inaelezwa haijaishia hapo, kuna wengine watakatwa kabla ya usajili kufungwa Septemba 7 mwaka huu.

Simba kuanzia 2018-2019, imecheza angalau robo fainali ya michuano ya CAF, huku msimu uliopita ikicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Katika kipindi chote hicho cha kufanya vizuri kwa Simba, timu hiyo imeingiza fedha kutoka CAF ikiwa ni kwa kiwango cha tofauti.

Mchanganuo wa fedha hizo upo hivi; msimu wa 2024/25 ambao imecheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ikimaliza nafasi ya pili, imepata Dola milioni 1 ambazo ni takribani Sh2.6 bilioni za Kitanzania.

Katika michuano hiyo pia msimu wa 2021/22, Simba iliishia robo fainali na kupata Dola 350,000 ambazo ni takribani Sh909 milioni.

Upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba imecheza robo fainali nne ambazo ni msimu wa 2018/19, 2020/21 na 2022/23 na 2023/24. Katika misimu hiyo, zile tatu za kwanza iliambulia Dola 650,000, takribani Sh1.7 bilioni kila msimu na 2023/24 ikachukua Dola 900,000 ambazo ni takribani Sh2.3 bilioni.

Kwa jumla, kupitia mafanikio ya michuano ya CAF, Simba imeingiza takribani Sh10.9 bilioni ndani ya kipindi cha kuanzia 2018 hadi 2025.

Kwa misimu sita kuanzia 2019/2020 hadi 2024/2025, Simba jumla ya bajeti yake ni Sh98.5 bilioni. Hiyo ni kwa mujibu wa bajeti ya kila mwaka inayotajwa katika mkutano mkuu wa klabu.

Kwa mujibu wa Simba, bajeti ya msimu hutokana na vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwemo udhamini kutoka kampuni mbalimbali.

Katika bajeti ya msimu uliopita ambayo ilipitishwa na wanachama ilionyesha Simba ilitarajiwa kupata Sh2.9 bilioni kutoka kwa mdhamini mkuu wa klabu hiyo ambaye ni Kampuni ya M-Bet, Sh1.5 bilioni kutoka kwa mdhamini wa jezi, Sh155 milioni mdhamini wa Ligi Kuu, Sh500 milioni Kampuni ya Serengeti, Sh250 milioni kutoka Kampuni ya A1 na Sh250 milioni kutoka vyanzo vingine

Mkuu wa Kitengo cha Fedha wa klabu hiyo, Suleiman Kaumbu mbele ya wanachama 700 waliohudhuria mkutano huo alisema katika bajeti ya Sh28.4 bilioni, Mo ametoa Sh7 bilioni ambazo zilianza kutumika kusajili mastaa wapya klabuni hapo.

Katika kila mkutano mkuu wa Simba wakati wa kutangaza bajeti ya msimu, hutaja mchango wa Mo kiasi cha fedha anachoweka ambapo msimu wa 2021/2022, bajeti ya klabu ilikuwa Sh12 bilioni huku Mo akitoa Sh2 bilioni.

Msimu wa 2022/2023 bajeti ilikuwa Sh15 bilioni na Mo alitoa Sh2.4 bilioni, huku msimu wa 2023/2024 bajeti ni Sh25 bilioni, Mo alitoa Sh3.9 bilioni.

Kwa jumla katika misimu hiyo minne ya karibuni, bajeti ya Simba jumla ni Sh80.4, huku Mo akitoa Sh15.3 bilioni.

Staa wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Zamoyoni Mogella, alisema kauli alizozitoa Mohamed ‘MO’ Dewji, zinategemea na ushirikishwaji nje na hapo atakuwa hajawatendea haki wengine.

“Kama hizo pesa alizokuwa anazitoa alikuwa anawashirikisha viongozi wengine wa Simba basi ana haki ya kutoka hadharani na kuyasema hayo, kama alikuwa anafanya kwa utashi wake kutoa pesa bila wengine kujua hilo halijakaa sawa,” alisema Mogella na kuongeza.

“Kitu pekee ninachoweza kushauri wanahitaji utulivu na vitu vifanyike kwa uwazi zaidi, nasisitiza kama pesa alizotoa Mo Dewji walishirikishwa basi ana haki kabisa kutoka hadharani.”

Katibu wa kundi la ushangiliaji la Simba la Ubungo Terminal, Joel Mwakitalima alisema:

“Kama kweli Mo Dewji anatoa pesa ndefu hivyo, basi amewafumbua macho watu, hadi anatoka hadharani kuzungumza huenda anaona zinatumika sivyo ndivyo.

“Kitu ninachoweza kuwashauri viongozi wa Simba wachangamke kama ilivyo kwa wenzao Yanga, wamepoa sana wakati hiyo ni klabu kubwa Afrika, jambo la msingi ambalo tajiri kalizungumza ni mshikamano wa kuhakikisha tunavuka tulipo.”

Mtaalamu wa uchumi wa magazeti ya Mwananchi, Ephrahim Bahemu amesema kwa ukubwa wa klabu kama Simba si ajabu kuwa imewezeshwa kiasi hicho cha pesa kilichotajwa kwa muda husika ikizingatiwa kuwa klabu zetu kubwa kwa sasa zinatumia kwenye usajili, mishahara ya wachezaji na utunzaji wa timu.

“Swali muhimu sasa pengine ni viongozi kuwaeleza wanachama juu ya vyanzo vingine vya mapato vinatumikaje maana kiasi kinachotajwa ni karibu thamani ya bajeti ya klabu hivyo pengine mapato mengine kama viingilio na malipo ya wadhamini mbalimbali yamehifadhiwa sehemu,”

Aliongeza kuwa kwa uwekezaji huo wa Mo bila shaka thamani ya klabu imongezeka muhimu ni kuwa na uwazi wa matumizi ya pesa hizo ili kuondoa utata kwa kuwa kiwango hicho kinanoneka kikubwa kuliko inavyoweza kufikirika.

Related Posts