Utiririshaji wa maji taka migodi midogo bado changamoto

Dodoma. Wizara ya Maji imesema bado migodi midogo inakabiliwa na changamoto ya utiririshaji wa maji taka na hivyo kusababisha athari kwenye vyanzo vya maji.

Hayo yamesema leo Jumatano Julai 16, 2025 na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Diana Kimario wakati akielezea juu ya mkutano wa mwaka wa usalama wa mabwawa utakaofanyika jijini Mwanza kuanzia Novemba 19-21, mwaka huu.

Amesema mkutano huo umeandaliwa na Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Taasisi ya Chemba ya migodi Tanzania (TCM) pamoja na Kampuni ya City Engineering.

Kimario amesema mikutano hiyo inayofanyika kwa miaka mitatu mfululizo sasa imekuwa ikijikita pia katika kutoa mafunzo kuhusu usalama wa mabwawa ya maji na tope sumu.

“Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zimeshuhudia majanga yatokanayo na mabwawa ya maji na tope sumu yanapobomoka, hili si jambo geni kwani pia limekuwa likiripotiwa na vyombo vya habari katika nchi za wenzetu ambao wamekumbwa na majanga makubwa zaidi yatokanayo na kubomoka kwa mabwawa hususan ya tope sumu,” amesema.

Amesema Serikali itahakikisha wanalinda usalama wa wananchi na mali zao na kujenga uelewa wa pamoja kuhusu hatua za dharura za kuchukua zinapotokea ajali za kubomoka kwa mabwawa hayo ili kuokoa maisha ya watu na mali.

“Mabwawa pamoja na kuwa ni miundombinu muhimu kwa ajili ya kuhifadhi maji kwa shughuli za kiuchumi na kuhifadhi tope sumu litokanalo na shughuli za uchenjuaji wa madini yasipohifadhiwa vizuri na ni hatarishi kwa mazingira, vyanzo vya maji, mali za jamii na hata vifo,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji wa Wizara hiyo, Dk George Lugomela amesema bado migodi mingi midogo inatiririsha majitaka na kuharibu vyanzo vya maji tofauti na mikubwa na ya kati.

Amesema udhibiti wa mafuriko pia ni changamoto nchini lakini mabwawa yakivuja yanakuwa na athari zaidi.

Amesema kaulimbiu ya mkutano huo inasema tahadhari za dharura za kukabiliana na majanga ya mabwawa ya maji na tope sumu imekuja wakati mwafaka ili kukabiliana na changamoto hiyo.

“Tumeona bwawa la Mwalimu Nyerere mwaka jana lilikumbwa na maji mengi ikawa ni changamoto kudhibiti yale maji baada ya mageti kufunguliwa na kusababisha mafuriko, hivyo tahadhari na kujiandaa ni muhimu kwenye mabwawa ya tope sumu na mabwawa ya maji masafi pia,” amesema.

Awali, Mtendaji Mkuu wa Chemba ya Migodi Tanzania (TCM), Benjamin Mchwampaka ambao ni waasisi wa mafunzo hayo, amesema wanaendelea kushirikiana na wataalam kutoka nje kwa kushirikiana na wizara kuwapa ujuzi watanzania katika kuhakikisha mabwawa ya maji na ya tope sumu yanakuwa salama wakati wote.

“Nawaomba wamiliki wa kampuni za uchimbaji mkubwa na wa kati wa madini ambao ni wanachama wa TCM na ambao siyo wanachama kushirikiwa kwa wingi ili kufanikisha mkutano huu muhimu,” amesema.

Mei, 2019, Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) liliwahi kuupiga faini ya Sh5.6 bilioni Mgodi wa Dhahabu wa Acacia North Mara uliopo Tarime mkoani Mara kwa kushindwa kudhibiti utiririshaji wa maji yenye kemikali.

Mgodi huo ulikumbana na adhabu hiyo baada ya kushindwa kudhibiti maji hayo kutoka katika bwawa la Kuhifadhia tope sumu na kwenda kwenye mazingira ya makazi ya watu na hivyo kuhatarisha afya za wakazi wanaozunguka mgodi huo.

Related Posts