Vita ya Zitto, Nondo Kigoma Mjini ‘usipime’

Dar es Salaam. Hatua ya Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa ACT Wazalendo, Abdul Nondo kuchukua fomu ya kugombea ubunge wa Kigoma Mjini kupitia chama hicho, ni wazi kuwa atamkabili kiongozi wake mstaafu, Zitto Kabwe.

Vita ya wawili hao, inafananishwa na ile ya mzazi na mwana, kutokana na kinachoelezwa kuwa, Zitto ni kiongozi, lakini mlezi wa kisiasa wa Nondo ndani ya chama hicho, lakini kuna uwiano wa mizania ya kukubalika kwao ndani ya chama hicho.

Nondo alichukua fomu ya ubunge kwa chama hicho, Julai 15, 2025, miezi mitatu baada ya mshindani wake kufanya hivyo, Aprili mwaka huu.

Wawili hao wote ni wazaliwa na wakazi wa Kigoma na hii sio vita yao ya kwanza, waliwahi kuwania ubunge wa jimbo hilo pamoja, katika mchakato wa ndani wa chama hicho, kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Zitto ndiye mwasisi wa chama hicho, kilichopata usajili mwaka Mei mwaka 2014, huku Nondo akijiunga na chama hicho, mapema baada ya kuhitimu elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Ukiacha uasisi, Zitto amekuwa kiongozi wa chama hicho kwa miaka 10 kabla ya kung’atuka, huku Nondo akiiongoza ngome ya vijana kwa vipindi viwili mfululizo.

Alizungumzia uamzi wake katika mahojiano na Mwananchi, Jumatano Julai 16, 2025, Nondo amethibitisha nia yake hiyo huku akisema ametimiza wajibu wake wa kikatiba hivyo demokrasia ndani ya chama itaamua iwapo ni yeye au Zitto.

“Nikweli kabisa nimegombea, ACT tunadai demokrasia na demokrasia haipaswi kusemwa tu ndani ya chama chetu bali inatakiwa kuonekana ikitendeka pia,” amesema.

Amesema ni kiu yake ya muda mrefu kuwawakilisha wananchi wa Kigoma Mjini, hivyo alichokifanya ni kutimiza wajibu wake ili kupigania maendeleo ya jamii yake.

“Mimi ni mwana-Kigoma nimekuwa na mpango wa kuwakilisha jimbo hili kwa muda mrefu hivyo, sina jimbo lingine la kugombea isipokuwa nyumbani Kigoma mjini,” amesema.

Kuhusu kushindana na kiongozi wake, amesema ni demokrasia na haki ya kila mwanachama kugombea nafasi anayoona inafaa katika sehemu yoyote.

“Kugombea ni haki ya kila mwanachama na kila mmoja anasifa zake na fikra zake katika uongozi, hivyo ni chama ndicho kitaamua nani awe mgombea baada ya michakato ya kidemokrasia na kama nitashindwa na ikawa kwa haki mimi nitamuunga mkono Zitto na kumnadi, kikubwa iwe kwa haki,” amesisitiza.

Washindani hawa wanarejea katika ushindani huo mara ya pili baada ya kipindi cha miaka mitano kupita huku kila mmoja akiwa amejipanga kwa namna yake na kujijengea ushawishi wake katika jamii hali inayofanya mchuano wa awamu hii kuvaa sura mpya juu ya nani anaweza kuibuka kidedea katika msimu huu.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dk Revocatus Kabobe anasifu hatua hiyo, akisema ni ukomavu wa demokrasia katika chama hicho kichanga.

Amesema si rahisi katika siasa kwa vijana kuthubutu kugombea nafasi za uongozi na wanasiasa wakongwe licha ya demokrasia kuruhusu.

“ACT bado ni chama kichanga lakini kwa hatua hii ya kijana Abdul Nondo kuchuana na aliyekuwa kiongozi wake mkuu inaonesha ukomavu wa demokrasia ndanio ya cham hicho,” amesema.

Dk Kabobe amesema Zitto ni kiongozi mkongwe katika siasa za Kigoma lakini huenda amekuwa akichaguliwa ndani ya chama kwa kukosa upinzani thabiti na huenda Nondo kwa nafasi aliyonayo na ushawishi wake akawa mpinzani sahihi na mkubwa.

“Zitto Kabwe amekua mwanasiasa mwenye ushawishi sana na bado anayo nafasi hiyo lakini huenda amekuwa akionekana hivyo kwa kukosa ushindani kutoka kwa watu makini, uamuzi wa Adbduk Nondo ni kukuwa kwa demokrasia na huenda akawa mshindani mkubwa kwa Zitto,” amesema.