Vodacom M-Pesa, Vivo Energy Tanzania Washirikiana Kuchochea Malipo ya Kidijitali

Kampuni ya Vodacom Tanzania, inayoadhimisha miaka 25 ya kuwahudumia Watanzania, imetangaza ushirikiano rasmi na kampuni ya mafuta ya Vivo Energy Tanzania katika jitihada za kukuza na kuongeza matumizi ya malipo ya kidijitali kwa wateja wanaonunua mafuta katika vituo vyake vya Engen kote nchini Tanzania. Uzinduzi huu uliofanyika katika kituo cha mafuta cha Engen kilichopo Mikocheni, Dar es Salaam ulihudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka sekta ya mafuta, watoa huduma za usafirishaji na wateja wa M-Pesa.

Ushirikiano huu unalenga kuimarisha mfumo wa Lipa kwa Simu, kutoa mikopo ya Chomoka inayotoa mafuta kwa madereva wa magari binafsi, daladala, bajaji na bodaboda. Pia wateja wa Engen watapa fursa ya kukopa simu janja kutoka Vodacom na kulipa mdogo mdogo ikiwa ni sehemu ya kuongeza wigo wa matumizi ya huduma za kidijitali nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa M-Pesa Vodacom Tanzania, Bw. Epimack Mbeteni, alisema, “Tunajivunia kushirikiana na Vivo Energy Tanzania, kampuni inayoamini katika uvumbuzi na maendeleo ya jamii. Ushirikiano huu si tu unarahisisha maisha ya wateja wetu, bali pia unatoa fursa ya kukuza kipato kupitia huduma salama, rahisi na za kisasa.”

Mbeteni aliongeza kuwa, “Kupitia Lipa kwa Simu, Vodacom Tanzania tunawapatia wateja wetu njia bora ya kufanya malipo bila kutumia fedha taslimu, huku tukipanua huduma za kifedha kama mikopo ya mafuta kupitia Chomoka na fursa za kukopa simu janja kwa madereva.”

Pamoja na uzinduzi huu, wateja wa Engen watafurahia ofa maalum ambapo Vodacom na Engen watawazawadia lita moja ya mafuta BURE kwa siku za jumamosi na jumapili kila watakaponunua mafuta na kulipa kwa simu. Ofa hii itapatikana kwenye vituo vyote vya Engen nchini kuanzia jumamosi tarehe 19 Julai 2025.

Takwimu zinaonesha kuwa Vodacom Tanzania inaongoza soko ikiwa na laini milioni 28, huku M-Pesa ikichukua zaidi ya asilimia 40 ya soko la huduma za kifedha kwa simu, ikifuatiwa na kampuni nyingine za simu. Vilevile, idadi ya miamala imeongezeka kwa kasi kubwa ikionesha jinsi Watanzania wanavyozidi kutegemea huduma za fedha kwa njia ya simu katika shughuli zao za kila siku.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Vivo Energy Tanzania, Bw. Mohamed Bougriba, aliongeza, “Tumejipanga kuhakikisha wateja wetu wanapata huduma bora zaidi katika kulipia mafuta na bidhaa zetu. Kwa kushirikiana na Vodacom kupitia M-Pesa, tunaamini tunaongeza thamani kwa kila mteja anayefika katika vituo vyetu vya Engen popote nchini, huku tukichochea mabadiliko ya kidijitali kwenye sekta ya mafuta.”

Hivyo Vodacom Tanzania na Vivo Energy Tanzania inawakaribisha madereva wa vyombo vya usafiri vya moto kama vile magari, bajaj, bodaboda aidha binafsi au wafanyabiashara. Kila Jumamosi na Jumapili, faidika na ofa ya lita moja ya mafuta bure kwa kununua mafuta kuanzia kiasi cha shs 10,000 TZS kwa kufanya malipo kwa kutumia M-Pesa.

Mkurugenzi Wa M-Pesa Vodacom Tanzania Epimack Mbeteni ( kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Vivo Energy Mohamed Bougriba wakisaini hati ya makubaliano ya kukuza na kuongeza matumizi ya malipo ya kidijitali kwa wateja, wanaonunua mafuta katika vituo vyake vya Engen kupitia Lipa kwa Simu hapa nchini. Hafla hii imefanyika tarehe 15 Julai 2025 jijini Dar es Salaam katika kituo cha mafuta cha Engen Mikocheni.


Related Posts