Geita. Jeshi la Uhamiaji mkoani Geita limewakamata wahamiaji haramu 719 waliovuka mipaka kwa njia za panya kuanzia Aprili hadi Julai 15, 2025, kinyume na sheria za nchi.
Akizungumza leo Jumatano Julai 16, Ofisa Uhamiaji wa mkoa huo, James Mwanjotile amesema idadi hiyo inajumuisha wahamiaji 126 waliokamatwa mwezi huu pekee, katika maeneo mbalimbali ya mjini Geita.
“Tuna operesheni inayoendelea kwa miezi mitatu sasa. Kuanzia Aprili hadi Juni 30 tulikamata wahamiaji 593. Mwezi huu hadi sasa tumeshikilia wengine 126, waliokutwa wakiishi bila makazi ya kudumu mjini Geita,” amesema Mwanjotile.

Amebainisha kuwa wahamiaji hao, wengi wao ni kutoka Burundi ambao huingia nchini kwa ajili ya shughuli za kilimo na uchimbaji madini, wakihusishwa na sifa ya uchapa kazi.
Hata hivyo, ameonya kuwa waajiri wa ndani wanapaswa kufuata taratibu za kisheria kwa kuwatafutia vibali vya kuishi nchini kisheria.
“Wengi huajiriwa kwa sababu wanaaminika ni wachapa kazi. Lakini ni lazima waajiri wao wawapatie vibali halali vya ukaazi. Kuwapitisha njia zisizo rasmi ni hatari kwa usalama wa nchi, kwani huenda wengine ni wahalifu,” amesema.
Mwanjotile amesema uhamiaji haramu ni changamoto kubwa kwa Mkoa wa Geita, lakini wanapambana nalo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama.
Ametoa wito kwa wananchi kushiriki kulinda usalama wa nchi kwa kutoa taarifa wanapobaini mtu asiye na vibali.
“Usalama si jukumu la vyombo vya dola pekee wala la Rais tu; ni la kila Mtanzania. Kuwafumbia macho watu wanaoishi nchini kinyume cha sheria ni kulisababishia taifa mzigo wa gharama ambazo zingetumika kwenye maendeleo,” aliongeza.

Amesema kwa sasa, mtu anayekutwa akiwa na mhamiaji haramu hulazimika kumrejesha nchini kwao kwa gharama zake mwenyewe.
Hata hivyo, alipoulizwa kama kuna Mtanzania anayeshikiliwa kwa kuwahifadhi raia hao wa kigeni, amesema waliokamatwa walikutwa wakizurura mtaani na hawakuwa kwenye makazi ya raia wa Tanzania.