Wasichana wanaoacha vyuo waongezeka | Mwananchi

Dar es Salaam. Idadi ya wasichana wanaoacha vyuo imeongezeka kwa asilimia 44 kati ya mwaka 2020/21 hadi 2023/24, Ripoti ya wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) 2024 inaeleza.

Hali hii inafifisha juhudi za Taifa kufikia usawa wa kijinsia katika elimu, hasa ikizingatiwa elimu ya juu ni nguzo muhimu ya uwezeshaji wa wanawake na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Kukosekana kwa ajira, mabadiliko ya mfumo wa elimu, kukosa uangalizi wa karibu zikiwa sababu zinazotajwa kuwapo kwa ongezeko hili huku mabadiliko ya mila na mitazamo hasi ya kijinsia haikuachwa nyuma.

Hili linashuhudiwa wakati ambao Serikali na wadau mbalimbali wameendelea kuhamasisha usawa wa kijinsia kupitia sera na mikakati, hali halisi inaonesha bado kuna pengo kubwa linalohitaji kushughulikiwa kwa dharura.

Ripoti hiyo ya mwaka 2024 inaonesha wasichana walioacha masomo mwaka 2020/21 walikuwa 907, idadi iliyoongezeka hadi kufikia 1,313 mwaka 2023/24 huku wanaume wakitoka 1,537 hadi kufikia 1,712, mtawaliwa.

Licha ya idadi ya wanaume inaoneka kuwa kubwa kuliko wasichana lakini ukuaji wake ulikuwa ni asilimia 11.35 pekee.

Katika kipindi cha miaka minne, 2021/22 ndiyo ilirekodiwa idadi kubwa ya wanafunzi waliokacha masomo, wasichana walikuwa 1,444 na wavulana 2,196 waliacha masomo.

Idadi hiyo ilikuwa ni ongezeko la asilimia 59.2 kwa wasichana na asilimia 42.87 kwa wavulana ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.

Akizungumza Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Iringa, Valerius Haule amesema zipo sababu mbili zinazochangia hali hiyo ikiwamo mabadiliko ya kiusimamizi na aina ya mazingira.

Katika upande wa mabadiliko ya kiutawala, Haule amesema wasichana wengi wanaoingia vyuo huwa wametoka katika mifumo ya elimu ambayo husimamiwa kwa mujibu wa sheria tofauti na vyuoni wanapolazimika kujitegemea.

“Katika mabadiliko haya wasichana huwa huru kufanya kile wanachohitaji hali inayofanya wengi kuishia kutomaliza masomo kwa sababu hata ukiangalia kesi za walioacha vyuo kwa sababu ya kukosa ada ni chache ukilinganisha na sababu nyingine,” amesema Haule.

Upande wa mazingira amesema baadhi ya wasichana pia wanaoingia vyuo hutoka katika shule za jinsia moja hali inayowafanya washindwe kufanya vyema na kujiamini wanapokutana na watoto wa kiume vyuoni hali inayodumaza ufaulu wao.

Maneno yake yaliungwa mkono na Latifa Shauri, mkazi wa Ilala jijini Dar es Salaam akisema  kutokuwapo kwa ufuatiliaji wa wazazi ni moja ya jambo linalofanya watoto kuingia katika makundi yasiyofaa na mwisho kuacha shule.

“Wazazi wengine, mtoto akifika chuo anaona si jukumu lake tena, anaamini mtoto atapata mkopo, atalipiwa ada, atapewa hela ya kula na wakati mwingine wanamfanya kuwa tegemezi nyumbani, hii inasababisha baadhi ya wasichana kuingia katika mambo mabaya ili waweze kupata mahitaji yao,” amesema Latifa.

Amesema suala hilo hufanya hata baadhi ya wazazi kutojua mabinti zao wanafanya nini vyuoni kinachowafanya kupata fedha zinazomuwezesha kumudu mahitaji yake ya kila siku.

“Tusije kulalamika tu, mtoto wangu hajamaliza chuo, alikuwa anacheza, hasomi wakati hukuwa unafuatilia kujua anaishije., Serikali iangalie namna ya kuongeza mikopo zaidi kwa wanafunzi hasa wale wanaotoka mazingira magumu, hii ndiyo njia pekee inayoweza kufanya wengi wamalize masomo yao hasa wasichana ambao wanaweza kuangukia katika vishawishi,” amesema Latifa.

Kuhusu kuongezeka kwa mikopo, kwa mwaka wa masomo 2025/26  jumla ya  Sh916.7 bilioni zimetengwa kwa wanafunzi wa elimu ya juu 99,620 wa mwaka wa kwanza katika ngazi za diploma, shahada ya kwanza na shahada za uzamili.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Dk Bill Kiwia alipokuwa akitangaza kufunguliwa kwa dirisha la uombaji mikopo, amesema wanafunzi 88,000 wa shahada ya kwanza watapangiwa mikopo hiyo.

Amesema idadi hiyo ni ongezeko la wanufaika 8,000 ikilinganishwa na mwaka wa masomo 2024/25 wanufaika 80,000 walipangiwa mikopo.

Kwa upande wa wanafunzi wa diploma, amesema mwaka 2025/26  wa masomo wanufaika 10,000 watapata mikopo hiyo ikiwa ni ongezeko la wanufaika 3,000 ikilinganishwa na ilivyokuwa katika mwaka wa masomo uliopita.

Amesema fedha hizo zitatumika pia kwa wanafunzi 173,783 wanaoendelea na masomo.

“Tunazidi kuongeza wigo wa wanafunzi wanaopata mikopo, mwaka huu hata wanafunzi wa diploma idadi yao imeongezeka hapa lengo ni kuhakikisha kwamba wanapata elimu bila kujali hali zao,” amesema Kiwia.

Mdau mwingine wa elimu, Nicodemus Shauri amesema hili linaonekana sasa kutoka na kuwapo kwa ongezeko la wasichana wanaofika vyuo vikuu hasa baada ya utamaduni uliokuwa ukimjali zaidi mtoto wa kiume katika kupata elimu kuanza kuondoka.

Hiyo ni kutokana na wazazi kuelimika na kuona umuhimu wa kuwasomesha watoto, hivyo kadri idadi inavyokuwa kubwa hata wanapokacha masomo inakuwa rahisi kuonekana.

“Lakini kitu kingine ni kukosekana kwa ajira, watu wakaiona waliosoma hawana ajira wanaamua kuacha vyuo wakatafute hela, kwa wavulana ndiyo huwa zaidi kwa sababu wanakuwa na haraka ya kutafuta hela, wanaume wanaonekana kuwa na majukumu hata vyuoni kuna watu wanaishi kama mke na mme na anayehudumia ni mwanaume,” amesema Shauri.

Katika kukabiliana na hali hiyo, Haule anapendekeza kuwapo kwa elimu ya kujitambua kwa wanafunzi wa ngazi za chini ili wanapofika vyuo waweze kujua kusudi lao.

“Nadhani mabadiliko ya sera ya elimu yataweka mkazo katika kujitambua hasa kwa wasichana, kufanya hivi kutawasaidia waweze kujimudu kama watoto wa kike kwa sababu tunaamini akiwa na miaka 16 hadi 18 anaweza kujitambua na kujiongoza vyema,” amesema Haule.

Related Posts