Waziri Ndumbaro: Wakati wa uchaguzi Serikali haitakuwa likizo

Dodoma. Zimwi la kutoa vibali vya viwanja kwa watu zaidi ya mmoja limezidi kuwaandama maofisa ardhi na sasa wametakiwa kushitakiwa kwa makosa ya utapeli.

Mbali na maofisa ardhi, Serikali imeagiza watakaokiuka Sheria katika kipindi cha uchaguzi washitakiwe haraka mahakamani sawa na wanaodhurumu mali za mirathi kwani ni makosa yasiyopaswa kufumbiwa macho.

Agizo hilo limetolewa jana jioni Julai 15, 2025 na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro wakati akikabidhi magari 16 kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ambayo walipokea maofisa wa Wilaya.

Amesema tatizo la ardhi linachafua sura ya nchi na kuondoa imani kwa watumishi jambo ambalo wengi wanaona limefumbiwa macho lakini akasema ni wakati wa kuamka na kuwashughulikia.

“Tunahitaji haki,usawa na maendeleo sasa nchi ikikosa haki haiwezi kutawalika, ndiyo maana nasema msiwaonee watu bali shughulikeni na wavunja sheria na muwafikishe panapowafaa ili wapate stahiki yao,” amesema Dk Ndumbaro.

Waziri wa Katiba na Sheria Dk Damas Ndumbaro akimkabidhi mfano wa ufunguo Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini Anna Kileo mara baada ya kukabidhi magari 16 yanayokwenda Ofisi za mashitaka wilayani



Kwa mujibu wa Waziri, anataja maadui watatu ambao wanahitaji kushughuliwa kwa haraka ni watu wanaofoji na kupora mirathi, wanaouza ardhi kwa zaidi ya mtu mmoja na wote watakaokiuka sheria wakati wa uchaguzi ikiwemo kutukana wenzao.

Amesema kipindi cha kuelekea uchaguzi Mkuu kuna watu huwa wanajizima data wakidhani Serikali ipo likizo mwisho wake wanasababisha uvunjifu wa amani.

“Utafiti unaonyesha mambo mengi hutokea nyakati hizi za uchaguzi ikiwemo matusi majukwaani, hao watu kamata sweka ndani ili waheshimu wengine,” anasema.

Kuhusu magari yaliyotolewa amesema yanakwenda kusaidia kazi kubwa katika Ofisi za mashitaka wilayani ambako kumekuwa na kilio cha kutofikika kwa baadhi ya maeneo hivyo kushindwa kupata ushahidi wa ufunguaji wa kesi.

Hata hivyo, amesema idadi ya magari 16 yaliyotolewa yanafanya hadi sasa ofisi za wilaya kufikisha magari 109 na kubaki na uhitaji wa magari 38 ili Wilaya zote zipate usafiri.

Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, Anna Kileo amesema ofisi hiyo inafanya mageuzi makubwa katika kushirikiana na Polisi na Magereza ili kupunguza msongamano wa wafungwa na mahabusu uliopo sasa.

Kileo amesema magari waliyopewa yatasaidia sana kupunguza ukubwa wa mahitaji ingawa bado wana mahitaji zaidi ya vyombo vya usafiri.

Ametaja miongoni mwa wilaya zilizobahatika kwa awamu hii ni Momba, Nyang’wale, Kilosa, Uvinza, Ubungo, Kilwa, Iramba, Misenyi, Gairo, Kilolo na Kilombero.

Mwendesha mashitaka wa Wilaya ya Kilolo, Tito Mwakalinga amesema watakachoanza nacho ni suala la uuzaji wa viwanja kwa watu zaidi ya mmoja, kitendo alichosema ni kosa la kujipatia fedha kinyume na sheria.

Mwakalinga anasema kwenye mirathi kuna kuna tatizo zipo fojali nyingi ambazo zinafanywa kupora haki ya watoto na wajane  na sasa wanaondoka na maagizo ya waziri kwenda kushughulikia mpango huo.