Wizara yazindua mfumo wa eKilimo, wakulima milioni saba kusajiliwa

Dodoma. Wizara ya Kilimo imezindua mfumo wa kielektroniki uitwao eKilimo, utakaowawezesha wakulima kupata huduma za ugani kwa njia ya simu kutoka kwa maofisa ugani waliosajiliwa rasmi nchini huku lengo ni kuwasajili milioni saba.

Mfumo huo umetengenezwa ili kutatua changamoto ya uhaba wa maofisa ugani nchini, ambapo kwa mujibu wa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, kuna upungufu wa takriban maofisa ugani 13,000.

Akizindua mfumo huo pamoja na kampeni ya Mali Shambani leo Jumatano, Julai 16, 2025, katika Kata ya Mtanana, Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, Waziri Bashe alisema kila mkulima ataweza kutumia huduma hiyo kwa kutumia namba yake ya usajili.

Ameeleza kuwa mfumo huo umeunganishwa na teknolojia ya akili bandia, itakayomwezesha mkulima kuuliza maswali yanayohusu kilimo na kupokea majibu papo kwa papo. Tayari mfumo huo umeanza kufanya kazi.

“Sasa hivi mkulima hatahangaika tena kumfuata Ofisa ugani ofisini kwake bali ataingia kwenye mfumo na kumtafuta aliye karibu naye ili aje amhudumie shambani kwake na kutakuwa na fomu maalum ya kujaza ambayo mwisho wa mwaka atafanyiwa tathmini ya kazi aliyoifanya kwa kuhudumia wakulima.


‎”Huduma hii ni kwa maofisa ugani wa serikali na wale ambao hawajaajiriwa na serikali lakini wanatambulika kwa kufanya huduma za ugani, lengo ni kuwahudumia wakulima kwa wakati na kutatua changamoto zao.”

‎‎Amesema mfumo huo ni rahisi kutumia kwa sababu unatumia lugha ya Kiswahili ambayo inatumiwa na kueleweka na wakulima wengi nchini.

‎‎Bashe amesema mpaka sasa Serikali imeshasajili wakulima zaidi ya milioni nne kwenye mfumo huku lengo likiwa ni kuwasajili wakulima milioni saba ambao wanatambulika nchini.

‎‎Mbali na hilo Bashe amesema Wizara ya Kilimo inashirikiana na Chuo cha Kilimo (Sua), Chuo Kikuu cha Nelson Mandela na Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) kuwaandaa vijana wanaounda mifumo ya kilimo ili iweze kutumika na wakulima badala ya kuazima mifumo kutoka nje ya nchi.

‎Amesema mpaka sasa wameshawatambua vijana 15 ambao watawezeshwa kuboresha mifumo yao waliyoiunda kwa ajili ya kuboresha na kurahisisha huduma za kilimo nchini.

‎‎Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai amewataka wakazi wa Wilaya ya Kongwa kuchangamkia fursa ya uwepo wa ofisi za ghala la hifadhi ya chakula nchini (NFRA) kwenye wilaya hiyo ili waweze kuuza mazao yao.

‎‎Aidha, amewataka wawe walinzi wa miundombinu ya kituo hicho na wajiepushe na uharibifu wa miundombinu ya kituo hicho kwani ina manufaa kwao na kwa wakulima wote nchini

‎‎Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli amesema wizara hiyo itashirikiana na taasisi za kifedha nchini kuwawezesha vijana waliobuni teknolojia mbalimbali za kilimo ili kuziboresha kabla hazijaanza kutumika au kuuzwa nje ya nchi.

‎‎Amesema Wizara ya Kilimo imejenga kituo atamizi cha kilimo ambacho kitakuwa na soko la mazao ya kilimo, kiwanda cha kusindika mazao na kituo atamizi cha teknolojia ya mifumo mbalimbali ya kilimo inayobuniwa na vijana wa Kitanzania.

‎‎Uzinduzi wa kituo atamizi kilichopo kwenye Kata ya Mtanana wilayani Kongwa mkoani Dodoma ambapo ndipo zilipo ofisi za NFRA kitazinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwenye kilele cha maadhimisho ya Nanenane Agosti 8, 2025.