KUELEKEA msimu ujao wa mashindano ya Ligi Kuu ya Wanawake, JKT Queens inaendelea kujiimarisha na sasa inadaiwa kumsajili kocha wa timu za vijana za Simba, Mohamed Mrishona ‘Xavi’, akichukua mikoba ya Esther Chabruma ‘Lunyamila’.
Licha ya kuipa ubingwa wa Ligi Kuu msimu uliopita, JKT imempa mkono wa kwaheri baada ya kumaliza mkataba na Wanajeshi hao wa kike.
Kocha huyo aliyehudumu kwa misimu miwili mfululizo tangu 2023, akichukua nafasi ya Ally Ally, ndiye aliyeipa ubingwa msimu huu mbele ya Simba Queens.
Mmoja wa watu wa karibu wa timu hiyo alieleza kuwa Xavi huenda akaiongoza JKT msimu ujao, akianza na mashindano ya CECAFA ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake, yatakayoanza mwezi ujao nchini Tanzania.
Aliongeza kuwa JKT imemuwekea ofa kubwa na mshahara mara mbili zaidi ya aliyokuwa analipwa kwenye kikosi cha Simba ya vijana.
“Kule kuna fursa nyingi mbali na mshahara atakaolipwa, lakini pia atapata fursa jeshini. Kila kitu kimekamilika na huenda muda si mrefu akatambulishwa JKT kuanza maandalizi ya msimu mpya,” alisema mtu huyo.
Kocha huyo ambaye pia aliwahi kuichezea Jang’ombe ya Zanzibar ambayo hakucheza sana baada ya kupata majeraha, amekuwa akipata nafasi ya kuzinoa timu za taifa za vijana na Taifa Stars.
Mbali na kupata nafasi kwenye timu za taifa, pia anafundisha mazoezi binafsi ya wachezaji mbalimbali akiwemo winga wa Simba, Elie Mpanzu, Maxi Nzengeli na Simon Msuva.