TAKRIBANI siku 15 zimekatika tangu kufunguliwa kwa dirisha la usajili hapa nchini, mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara, Yanga SC wameshtukia jambo na kuamua kuchukua hatua za haraka.
Yanga ambayo msimu wa 2024-2025 ilibeba mataji matano, Kombe la Toyota, Ngao ya Jamii, Kombe la Muungano, Ligi Kuu Bara na Kombe la FA, inaendelea na hesabu za usajili huku siku zikizidi kukimbia kukaribia msimu ujao wa 2025-2026.
Katika kuimarisha kikosi chake, uongozi wa klabu hiyo umeshtukia kitu na kuweka mikakati ya kuitolea macho michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) itakayofanyika kuanzia Agosti 2 hadi 30 mwaka huu ikichezwa nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.
Kigogo mmoja wa Yanga aliliambia Mwanaspoti, kwa asilimia kubwa usajili umefanyika, lakini hawajamaliza, wakiacha nafasi ya kuangalia majembe zaidi kwenye michuano hiyo huku akibainisha shida kubwa ni kupata mastaa wenye ubora lakini suala la fedha si tatizo kwao.
Kwa mujibu wa bosi huyo, walichopanga ni kwa baadhi ya nafasi wanazotaka kuziboresha kwenye kikosi chao watakuwa na mkakati maalum wa kuangalia watu bora watakaopatikana kwenye fainali hizo.
Bosi huyo wa juu Yanga anayehusika kwenye usajili, alisema wachezaji wote wanaoshiriki fainali hizo, ni wale wanaocheza ligi za ndani Afrika, hivyo wanaona hakutakuwa na ugumu mkubwa kwao kuwapata.
“Hatuwezi kumaliza nafasi zote, tutakuwa na jicho letu kwenye hizi Fainali za CHAN, unajua shida yetu sisi ni watu bora tunaowataka, sio fedha,” alisema bosi huyo.
“Kama ingekuwa fedha tusingeingia sehemu ambazo kuna timu unaambiwa inazunguka na mchezaji ikiongea naye, tunataka watu sahihi kwa malengo yetu.
“Kuna wachezaji tutawatafuta kwenye fainali hizi, tumejipanga kwenda Uganda, Kenya na hapa nchini kufuatilia kwa kina wachezaji bora tunaowataka.”
Licha ya kwamba hadi sasa Yanga haijatangaza kumsajili mchezaji yoyote, lakini ilikuwa kwenye vita ya kuiwania saini ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Ivory Coast 2024-2025, Celestine Ecua aliyekuwa akiitumikia Asec Mimosas kwa mkopo akiwa mali ya Zoman na usajili wake unatajwa kukamilika kwa mujibu wa wakala wake.
Muda wowote kuanzia sasa, Yanga itamtangaza rasmi kocha mpya atakayeinoa timu hiyo kuelekea msimu ujao baada ya Miloud Hamdi mkataba wake kumalizika na kuondoka.
Awali Yanga ilikuwa inatajwa kuwa kwenye mazungumzo na makocha wawili ambao ni Rhulani Mokwena raia wa Afrika Kusini na Mfaransa Julien Chevalier, lakini inaelezwa kati yao hakuna anayetua kikosini hapo.
Wakati ikiwa hivyo, Romain Folz aliyewahi kuwa kocha msaidizi katika kikosi cha Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, ndiye anatajwa zaidi kwa sasa.
Kocha huyo raia wa Ufaransa, amejijengea jina barani Afrika baada ya kuifundisha Township Rollers ya Botswana, alihamia Afrika Kusini mwaka 2022 kujiunga na Marumo Gallants, ambapo alikua kocha mdogo zaidi katika Ligi Kuu wakati huo. Baadaye alihamia AmaZulu FC, kabla ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa klabu hiyo mwaka 2023.
Katika msimu wa 2024/25, alijiunga na Mamelodi Sundowns kama kocha msaidizi lakini aliacha kazi pamoja na kocha mkuu Manqoba Mngqithi, miezi michache baada ya msimu kuanza.
Rais wa Yanga, Hersi Said alisema suala la benchi la ufundi la timu hiyo kwa msimu ujao, wamezingatia uzoefu kwenye kutafuta kocha ambaye atawabeba kufikia mafanikio huku akitaja kuwa benchi hilo pia litakuwa sehemu ya wao kufanikiwa.
“Kocha anayekuja ana deni la kuhakikisha wanachama na mashabiki wanafurahia kutetea mataji yote lakini pia kimataifa tuweze kufanya vizuri kitu ambacho hakijafanyika msimu huu ulioisha, tusidanganye mashindano ya kimataifa yanahitaji uwekezaji mkubwa na uzoefu vitu ambavyo ndio tunavipambania.
“Yanga imefika fainali Kombe la Shirikisho huo ulikuwa ni uzoefu baada ya hapo kuna wachezaji waliondoka, msimu uliofuata tukiwa na sura mpya tulifika hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika bado kuna nyota waliondoka na msimu huu ulioisha tumeishia makundi tunapambana kuhakikisha tunabakiza nyota wengi muhimu kwasababu tuna kazi ya kufanya ili tuwe na muendelezo mzuri kimataifa ambapo kunahitaji uzoefu,” alisema Hersi.