Wakati mamlaka za jiji zikisisitiza wafanyabiashara ndogondogo (wamachinga) kuondoka katika barabara zinazozunguka soko la Kariakoo, hali ya sitofahamu inaendelea kuhusu tarehe rasmi ya kufunguliwa kwa soko hilo lililoungua moto mwaka 2021.
Soko la Kariakoo limekuwa kwenye ukarabati tangu mwaka 2022, huku serikali ikitumia zaidi ya Sh28 bilioni kwa ukarabati na ujenzi wa soko dogo la ziada. Wafanyabiashara waliokuwa hapo awali walihamishiwa kwenye masoko ya Kisutu, Karume na Machinga Complex ili kupisha ukarabati.
Ingawa ujenzi umeelezwa kukamilika kwa asilimia kubwa kiasi cha kuanza kutumika, bado hakuna tarehe kamili iliyotangazwa ya ufunguzi rasmi.
Katika mahojiano na Mwananchi, Meneja wa Shirika la Masoko, Ashraph Abdulkarim, anasema mnada huo uliofanyika kwa njia ya mtandao na watu walipaswa kutuma maombi yao kuanzia Juni 5 hadi Juni 11, 2025.
Kwa mujibu wa Abdulkarim tayari waliopata nafasi wameanza kupatiwa mikataba kwa ajili ya taratibu zingine za kutambuliwa kama wapangaji halali wa shirika.
Hata hivyo pamoja na kufikiwa kwa hatua hizo bado kumekuwapo na danadana za kulifungua ambazo zilianza tangu Agosti, 2025 baada ya kumalizika kwa uhakiki wa kwanza wa wafanyabiashara waliopaswa kurejea sokoni hapo.
Mfanyabiashara Abdul Kombo, amesema wao hawaelewi ni lini hasa soko hilo litafunguliwa kwa kuwa kumekuwa na ahadi za mara kwa mara ambazo hazitekelezwi.
“Sisi tunawasubiria serikali watuambie lina haswa tunarudi kuanza biashara hapo sokoni, kwa kuwa kila siku tumesikia tukitajiwa tarehe tofauti za kufunguliwa, tuna imani wao ndio wanajua zaidi,” amesema Kombo.
Naye Mwenyekiti wa wafanyabiashara kitengo cha Shimoni, Ramadhani Kakandilo, amesema maandalizi ni kweli yanaendelea na kwa sasa kumekuwa na vikao vya mara kwa mara na uongozi wa soko kuhusu suala hilo.
Hata hivyo amesema shida inaonekana ipo kwenye kupata tarehe rasmi ambayo Rais Samia Suluhu anayetarajiwa kulizindua kuwa na nafasi ya kushiriki hilo.
Katika ushauri wao amesema wafanyabiashara wanapendekeza waanze kupangwa na kufanya biashara na Rais atakapokuja awakute tayari ndani ya soko.
“Huu ushauri pia tayari tumeufikisha pia kwa mamlaka husika na tunaamini kwa kuwa serikali yetu ni sikivu wataufanyia kazi,” anasema.
Kwa upande wake Katibu wa soko la wazi Kariakoo, Sudi Jongo, hakuwa mbali na Kakandilo na kueleza kuwa wakipangwa na kuanza kazi ni rahisi kuzibaini changamoto na pindi atakapokuja Rais waweze kuwasilisha kile walichoona ili ziweze kufanyiwa kazi.
“Mimi sijawahi kuona soko watu hawajui ndani linafananaje, hawajawahi kufanya biashara halafu linazinduliwa tu, tutazungumza nini hiyo siku kwa mgeni rasmi,” amesema Jongo.
Mmoja wa wananchi , Johari Kimambo, amesema ana wasiwasi kuendelea kuchelewa kufunguliwa kwa soko hilo, kutasababisha baadhi ya vifaa kuharibika.
“Kuna vifaa naamini vilivyofungwa mle vinahitaji uwepo wa watu kuviangalia au kuwashwa mara kwa mara, sasa kuendelea kuchelewa kulifungua, huenda serikali ikapata hasara kwa uwekezaji ulioufanya,” amesema Kimambo.
Mchambuzi wa masuala ya uchumi na kijamii, Oscar Mkude, amesema kuchelewa kufunguliwa kwa soko hilo kuna hasara kwa pande zote ikiwemo wakulima, wafanyabiashara na serikali.
“Kwa wafanyabiashara wapo ambao soko limeungua wameshindwa kufanya biashara au huko walipo haiwalipi kama walivyokuwa katika soko hilo. Lakini kuna wale wakulima ambao walikuwa wanategemea kuuza mazao yao hapo nao watakuwa wameathirika kwa namna moja au nyingine tangu soko limeungua hivyo kurejea kwake ingekuwa ahueni kwao.
“Wakati kwa upande wa serikali itashindwa kukusanya mapato yake ukizingatia tayari imeshaweka hela katika ujenzi wake, fedha ambazo ni kodi za wananchi wanaokamuliwa wanaponunua bidhaa au kupata huduma mbalimbali,” amesema Mkude.
Pia amesema soko hilo lina umuhimu mkubwa uchumi wa nchi na kubainisha hata biashara mbalimbali zinaofanyika leo maeneo ya Kariakoo soko hilo lina mchango wake.
“Naweza kusema kuchelewa kwake ninavyoona kunachangiwa pia na masuala ya kisiasa ambayo kwa namna moja au nyingine inafaidisha wachache kuliko walio wengi ambao ni watanzania wa kawaida,” anasema mchambuzi huyo.
Kwa nyakati tofauti viongozi wanaohusika kulisimamia soko hilo wamekuwa wakitoa ahadi ya kufunguliwa kwake bila utekelezaji ambapo Januari, 2025 Mwenyekiti wa bodi wa Shirika la Masoko Kariakoo, Hawa Ghasia alisema lingefunguliwa Februari 2025, baada ya kukamilisha kuwapanga wafanyabiashara.
Ghasia aliyasema hayo Januari 29, 2025, alipokuwa akielezea shughuli ya kumaliza kufanya uhakiki wa mara ya pili kwa wafanyabiashara wanaotakiwa kurejea sokoni hapo ambao ni wale walikuwapo kabla ya soko hilo kuungua.
Kabla ya hapo pia aliwahi kusema lingefunguliwa Agosti mwaka jana, lakini kutokana na vurugu zilizotokea kwenye uhakiki na wafanyabiashara kutoridhika baada ya baadhi kutokuwapo hilo halikuweza kutekelezeka.
Kama haitoshi kwa nyakati tofauti viongozi wa jiji la Dar es Salaam, akiwamo Mkuu wa Mkoa, na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, wamekuwa wakiwataka wafanyabiashara ndogondogo (wamachinga) ambao wapo katika barabara zinazoingia katika soko hilo kuondoka ikiwa ni maandalizi ya kuelekea kulifungua.
Mei 28, 2025, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya soko hilo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila alitoa wiki mbili kwa wafanyabiashara hao kuondoka ikiwa ni moja ya maandalizi ya kuelekea uzinduzi wake.
Katika mkutano huo Chalamila alisema tayari soko hilo limeshakamilika kwa asilimia 98 na kinachofuata ni maandalizi ya kulifungua japo hakuweka wazi tarehe rasmi.
“Mpaka sasa ninapozungumza soko limeshakamilika kwa asilimia 98 na kubakia matengenezo madogomadogo ikiwamo uzio. Baada ya hapo kinachosubiriwa ni Waziri mwenye dhamana wa Tamisemi kufanya ziara ya mwisho kukagua na kujidhihirisha ukamilifu wake kabla halijaja kuzinduliwa, uzinduzi unaotarajiwa kufanywa rasmi na Rais Samia Suluhu Hassan,” alisema Chalamila.
Hata hivyo ameleleza kuwa pindi soko hilo litakapofunguliwa kuna utaratibu umewekwa wa kuwapa baadhi ya maeneo wamachinga ambapo kuna maduka madogo watawekwa ili kupunguza adha hiyo ya wao kukaa barabarani.
Ukiachilia mbali Chalamila, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ambapo ndipo Wilaya lilipo soko hilo, alisisitiza tena kuondoka kwa wafanyabiashara hao katika barabara hizo.
Mpogolo alitoa msisitizo huo Juni 30, 2025 alipotembelea soko hilo kwa ajili ya maandalizi ya uzinduzi huo ikiwa na pamoja ya kutoa elimu kwa wafanyabiashara kutambua umuhimu wa kufungua barabara hizo.
“Ndugu zangu tunakaribia kuzindua soko letu hili ambalo awali lilipata majanga ya kuungua na Rais wetu mpendwa Dk Samia Suluhu Hassan kutoa fedha nyingi kuligharamia kulijenga upya hivyo tuwe tayari kulizindua na tufuate sheria stahiki bila shuruti kupisha uzinduzi huo,” alisisitiza Mpogolo.
Mkuu huyo wa Wilaya alisema moja ya barabara zinazotakiwa ziwe wazi ni pamoja na ile inayoingia sokoni shimoni iwe wazi kuelekea ufunguzi huo.
Alisema Soko la Kariakoo ni la Kimataifa na lina matumaini makubwa kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi wanaokuja kupata huduma katika soko hilo na kusisitiza hawatamvumilia yeyote atakayekaidi maagizo hayo kwa kuwa ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha Soko linakuwa na mazingira rafiki na litakaloingilika muda wowote
Hata hivyo naye alipoulizwa ni lini haswa linafunguliwa, hakuwa wazi kusema zaidi ya kusema hivi karibuni na kueleza kuwa maandalizi yanaendelea.
Makamu Mwenyekiti wa Wamachinga Tanzania na Mwenyekiti wa Soko la Kariakoo, Stephen Lusinde, anasema kazi kuwaondoa si kubwa kwao kwa kuwa hata wamachinga wenyewe wanajua maeneo hayo wameyavamia.
Lusinde anafafanua kuwa tangu awali wakati wanawapanga maeneo hayo ya Kariakoo, kuna barabara za mitaa walikubaliana waziache wazi na nyingi ndio hizo zinazoingia ambazo ni pamoja na ile ya Mtaa wa Nyamwezi -Mkunguni, Nyamwezi-Tandamti, Tandamti, Sikukuu -Mkunguni na Mkunguni –Congo (Big born).
“Katika maeneo hayo wafanyabiashara wanaelewa kuwa tulishakubaliana pawe wazi ila kwa wale wakaidi waliamua tu kuvamia na wengine maeneo wanayo walishapangiwa, hivyo ikifika muda tutafanya kazi yetu na hakutakuwa na wa kumlaumu,” anasema Lusinde.