Mahakama yaainisha yaliyozuiwa Chadema | Mwananchi

‎Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imetoa ufafanuzi wa amri ya zuio la kufanya shughuli za kisaisa ndani ya Chadema na kutumia mali za chama hicho mpaka kesi inayokikabili ya mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali itakapoamuliwa.

‎‎Ufafauzi huo umetolewa na naibu msajili wa mahakama kutokana na maombi yaliyowasilishwa na mawakili wa wadai katika kesi hiyo wakidai kuwapo upotoshaji kuhusu wanaoguswa na zuio hilo.

‎‎Katika barua ya Julai 14, 2025 kwenda kwa wadaawa ambayo Mwananchi imeiona nakala yake na kuthibitishwa na mawakili wa pande zote, naibu msajili amebainisha makundi 10, wakiwamo viongozi wote kuanzia ngazi ya juu ya kitaifa hadi wanachama wa kawaida.

‎‎Mahakama ilitoa amri ya zuio katika shauri la maombi madogo lililofunguliwa na wadai katika kesi ya msingi, baada ya kukubaliana na hoja zao.

‎‎Kesi ya msingi ya madai namba 8323 ya mwaka 2025 imefunguliwa na Said Issa Mohamed, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema Zanzibar na wenzake wawili, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu, ambao ni wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa chama hicho (Zanzibar).

‎Wadai walalamikia kuwapo mgawanyo wa rasilimali usio sawa baina ya Tanzania Bara na Zanzibar na kuwapo ubaguzi. Wadaiwa ni Bodi ya Wadhamini ya Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.

‎‎Wadai pia walifungua shauri la maombi madogo wakiomba mahakama itoe amri ya zuo la muda dhidi ya wadaiwa kutofanya shughuli za kisiasa na kutumia mali za chama hicho hadi kesi ya msingi itakapoamuliwa.

‎‎Shauri hilo lilisikilizwa na kuamuliwa Juni 10, 2025 na Jaji Hamidu Mwanga, aliyekubaliana na wadai na kutoa amri hizo baada ya kutupilia mbali pingamizi la wadaiwa dhidi ya kesi ya msingi na shauri la maombi ya zuio.

‎Amri hizo za zuio ziliibua tafsiri tofauti baina ya pande hizo mbili. Viongozi wa Chadema hususani Makamu Mwenyekiti (Bara), John Heche na Kaimu Katibu Mkuu, John Mnyika mara kadhaa wamenukuliwa na vyombo vya habari wakidai amri hizo zinawahusu wadaiwa pekee, yaani Bodi na Katibu Mkuu.

‎‎Wadai kwa upande wao  kupitia jopo la mawakili, Shaban Marijani, Gido Simfukwe na Alvan Fidelis  wamekuwa wakipinga tafsiri hiyo wakidai inawahusu viongozi na wanachama wote.

‎‎Ni kutokana na msigano huo wa tafsiri ya amri hizo, mawakili wa wadai walimwandikia barua msajili wa mahakama kuomba ufafanuzi wa wigo wa amri hizo.

‎‎Mmoja wa mawakili hao, Simfukwe amelieleza Mwananchi kuwa walimwandikia msajili barua kuomba tafsiri ya amri hizo Julai 2, 2025 kutokana na alichokiita upotoshaji wa uamuzi wa mahakama kuhusu amri hizo za zuio.

‎‎”Julai 2, 2025 tuliomba tasfri ya mkanganyiko unaotolewa wa uamuzi wa shauri hilo, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo Dar es Salaam ametoa ufafanuzi na kuainisha makundi 10 yaliyowekewa zuio tofauti na ilivyokuwa ikipotoshwa tangu uamuzi wa zuio umetolewa,” amesema.

‎Wakili wa Chadema, Dk Rugemeleza Nshala amekiri kupokea barua ya msajili, lakini amesema hawakubaliani na tafsiri hiyo na kwamba watachukua hatua za kisheria.

‎‎”Kweli tumepokea barua ya naibu msajili ikiainisha makundi 10 yaliyowekewa zuio, lakini amepotosha. Zuio lipo kwa makundi mawili tu, bodi ya wadhamini na katibu mkuu. Kwa hiyo, chama kitachukua hatua za kisheria,” amesema.

Katika barua, naibu msajili amesema zuio hilo linawahusu Bodi ya Wadhamini Chadema na Katibu Mkuu ambao ni wadaiwa katika kesi hiyo au Kaimu Katibu Mkuu.

‎‎Wengine waliotajwa katika barua kuhusu zuio hilo ni Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Kaimu Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, makamu mwenyekiti Bara au Kaimu Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara na Makamu mwenyekiti Zanzibar au Kaimu Makamu Mwenyekiti Zanzibar.

‎‎Vilevile naibu makatibu wakuu au kaimu naibu makatibu wakuu Bara na Zanzibar.

‎‎Kundi jingine ni la viongozi wote katika ngazi zote iwe ni viongozi walioteuliwa moja kwa moja katika nafasi zao za kiuongozi au wanaokaimu.

‎‎Kundi la 10 ni la mfanyakazi au wakala au mtu yeyote anayefanya kazi hizo kwa niaba ya Chadema, atakayefanya kazi za kisiasa kwa kutokea taifa, mkoa, wilaya, halmashauri, tarafa na maeneo yote nchini kwa Zanzibar na Bara.

‎‎Wakili Dk Nshala amedai makundi mengine yaliyotajwa na naibu msajili ni upotoshaji, akidai zuio hilo linagusa makundi mawili pekee, yaani wadaiwa waliotajwa katika kesi hiyo ambao ni bodi ya wadhamini na katibu mkuu.

‎Amesema Chadema kitachukua hatua za kisheria kupinga makundi mengine manane ambayo yaliyotajwa.

Wakili Simfukwe amesema mtu yeyote katika makundi hayo akifanya kinyume cha amri ya mahakama ni kosa kisheria.

‎‎Amesema wote waliotajwa katika barua hiyo kufanya mikutano au mahojiano na vyombo vya habari yanayoihusu Chadema ni kosa.

‎‎”Kama waliotajwa watafanya mahojiano kuwahusu wao binafsi na si Chadema hilo si kosa, lakini chochote kile kwenye makundi hayo 10 yaliyotajwa kikifanyika kuhusu chama ni kosa kisheria,” amesema.

‎Katika kesi ya msingi wadai wanaiomba mahakama itamke na kuamuru kuwa wadaiwa wamekiuka sheria zinazohusu vyama vya siasa na katiba ya chama hicho.

‎‎Wanaomba hayo wakidai kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Zanzibar na Tanzania Bara.‎

‎Pia wanadai kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga Muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

‎‎Hivyo, wanaomba mahakama itoe hukumu na amri dhidi ya wadaiwa kwamba wamekiuka kifungu cha 6A (1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 Marejeo ya mwaka 2019.

‎‎Pia wanaiomba mahakama itamke kwamba, ugawaji wa fedha, mali na rasilimali kwa ajili ya shughuli za kisiasa na kiutawala kati ya Tanzania Bara na Zanzibar unaofanywa na wadaiwa ni kinyume cha sheria na ni batili.

‎‎Vilevile wanaiomba mahakama itamke na kuwaelekeza wadaiwa kuzingatia kifungu cha 6A (1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 Marejeo ya mwaka 2019.

‎‎Wadaiwa katika kesi hiyo waliandika barua kumtaka Jaji Mwanga ajiondoe kusikiliza kesi hiyo kwa madai kuwa hawana imani naye.

Jaji Mwanga alisikiliza madai hayo Julai 14 na amepanga kutoa uamuzi wa ama kujitoa au kuendelea na kesi Julai 28, 2025.