YANGA ilikuwa na hesabu na makocha wawili raia wa Ufaransa, lakini mmoja amefunguka sababu zilizomfanya kurudi nyuma kukubaliana na dili hilo.
Kocha aliyefunguka hayo ni Julien Chevalier ambaye amemaliza msimu akiwa na ASEC Mimosas ya Ivory Coast, ambapo amekiri mbele ya Mwanaspoti kwamba alikuwa na hesabu za kutua Jangwani.
Chevalier alisema sio rahisi kuachana na ofa kubwa ya kuifundisha klabu kubwa kama ya Yanga, lakini kikao chake na uongozi wa juu wa timu hiyo ndio kimebadilisha akili yake.
Chevalier alifichua kwamba ndani ya msimu uliomalizika alipanga kuondoka Asec kutokana na kuandamwa na baadhi ya mashabiki wakiona kama mbinu zake zimefikia mwisho.
Kocha huyo ambaye ameoa kwa siri wiki moja iliyopita alisema anarejea Asec baada ya kuhakikishiwa imani na uongozi wa timu hiyo kwa hatua ya kusaini mkataba mpya.
“Nilikuwa na ofa nyingi, lakini kuna ofa moja kutoka Tanzania ilikuja, unajua niseme ukweli nilitaka kuondoka Ivory Coast, katikati ya msimu uliomalizika, kuna kelele zilielekezwa kwangu hazikunifurahisha,” alisema Chevalier.
“Asec ni timu inayotengeneza wachezaji wengi na kuwauza, hakuna msimu hatuuzi wachezaji, wapo baadhi ya mashabiki wao wanataka kuona tunachukua ubingwa wa Afrika na tunashinda mataji ya nyumbani.”
Kocha huyo aliongeza; “Miaka yote tumekuwa tunapambana kutimiza hilo lakini hapa kati tumeuza sana wachezaji wetu wenye vipaji vikubwa, wengine walikuja huko Tanzania, ilitufanya kupoteza ubora wetu kwenye mashindano.
“Haikunifurahisha niliamua kuandika barua ya kutaka kukaa pembeni lakini uongozi uliniambia bado una imani nami.”
“Hivyo nitarudi kuzungumza nao. Naipenda ASEC ni klabu inayobeba maono ya kile ninachotaka, napenda kufanya kazi na vijana, mara nyingi wanakuwa na njaa ya mafanikio.”
Kutokana na kocha huyo kuamua kurejesha majeshi Asec, Yanga mezani mwake imesaliwa na jina la Romain Folz (35) aliyewahi kupita Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, ikielezwa muda wowote huenda akatangazwa kama dili litakuwa limetiki kabla ya kutolewa kwa ‘Thank You’ kwa watakaoachwa.