UONGOZI wa klabu ya Simba ni kama umekubali ya ishe juu ya aliyekuwa nahodha wa timu hiyo, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ baada ya kukiri kushindwa kumuongezea mkataba mpya.
Ipo hivi. Simba kupitia Ofisa Habari, Ahmed Ally amesema uongozi ulianza kufanya mchakato wa mazungumzo kabla ya mkataba kumalizika, lakini hadi sasa makubaliano ya pande zote mbili hayajafikia mwisho.
Ahmed amesema walianza kufanya hivyo kutokana na kocha Fadlu Davids kuwaambia kuwa bado anahitaji huduma ya beki huyo wa kushoto kwa msimu ujao.
“Kabla ya mkataba kumalizika viongozi walianza mazungumzo naye kwa ajili ya kumuongeza mkataba mpya juhudi hizo zimeshafanyika, lakini hazikufikia mwisho kwa maana hawakufikia makubaliano ya pande zote mbili,” amesema Ahmed na kuongeza;
“Hadibmuda huu Tshabalala ni mchezaji huru anaweza kuamua chochote kwa maslahi yake binafsi kufuta au kubadilisha utambulisho wake kwenye mitandao ya kijamii.”
Ahmed amesema Tshabalala ni mchezaji ambaye wanayetamani kuendelea kuwa naye kwa sababu ya umuhimu alionao ndani ya Simba, huku akiweka wazi kuwa miaka 11 ndani ya timu hiyo sio jambo jepesi.
“Tshabalala ameitumikia Simba kwa moyo na mapenzi ya hali ya juu na amepambana kuhakikisha timu yetu inafika hapa ilipo sasa, mafanikio yote tunayojivunia yote yana mchango wa moja kwa moja na mchezaji huyo,” amesema Ahmed na kuongeza;
“Tungependa kubaki naye kwa sababu hata kocha Fadlu Devids alithibitisha ana mpango wa kuendelea na mchezaji huyo kutokana na mchango mkubwa aliouonyesha ndani ya Simba na ndio maana viongozi walianza mazungumzo naye kabla ya mkataba kuisha.”
Ahmed amesema mazungumzo bado hayajafika mwisho na walichoamua sasa uamuzi wowote utakaoamuliwa ni ya pande zote mbili wakiamua kwenda na Tshabalala ni kwa maslahi ya pande zote mbili mchezaji na Simba.
“Tukisema tunaachana na Tshabalala pia ni maslahi ya Simba na mchezaji mwenyewe na lazima wanasimba wakubali hilo kwamba unakuja na unaweza kuondoka hakuna mtu angetamani kuona nahodha wa timu anaondoka muda ukishaamua umeamua.”