Simba yawaita mapema kina Ahoua, Camara

NYOTA wa Simba akiwamo Jean Charles Ahoua, Moussa Camara na wenzao wengine waitwa mapema kambini mwishoni mwa mwezi huu ili kujiandaa na maandalizi ya msimu mpya wa 2025-2026.

Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally, amesema wachezaji wote wapya na ambao wanatakiwa kuendelea na timu hiyo wote wanatakiwa kurejea mwisho wa mwezi huu.

Amesema mpango wao ni kuweka kambi nje ya Tanzania, hivyo nyota wote wa kikosi hicho watajumuika Dar es Salaam ambapo wataweka kambi ndogo ya muda kabla ya kusafiri.

“Tunanategemea hadi kufika Agosti tuwe tumemaliza mipango yote ya usajili na kukusanyika pamoja tayari kwa maandalizi ya safari,” amesena Ahmed na kuongeza;

“Usajili umefika hatua nzuri licha ya mashabiki kuwa na wasiwasi kwamba hatujaanza kusajili nawaomba wana Simba kuwa na amani mambo yanaendelea vizuri na tupo kwenye hatua nzuri.”

Mwanaspoti linafahamu kuwa, Simba ina mpango wa kuweka kambi Misri na Uturuki kama chaguo la kwanza kwa sababu ya mazingira yao bora ya maandalizi.

Misri ina klabu nyingi zinazoshiriki mashindano ya Afrika na zina miundombinu bora, wakati Uturuki inatoa hali ya hewa nzuri, viwanja vya kisasa na nafasi ya kucheza mechi za kirafiki na timu kutoka Ulaya Mashariki na Asia.

Katika kambi hiyo ya nje ya nchi, Simba inatarajiwa kucheza takribani mechi nne hadi tano za kirafiki dhidi ya timu kutoka ligi kubwa na zenye historia ya kimataifa, ambazo zitapangwa kwa kushirikiana na mawakala wa kimataifa wa michezo.