Iringa. Hali ya sintofahamu na ukata bado imewagubika wafanyabiashara wa soko la Mashine Tatu lililoko katika Manispaa ya Iringa, licha ya kazi ya usafi kukamilika katika eneo hilo lililoungua kwa moto hivi karibuni.
Ingawa hatua hiyo imeleta matumaini ya kurejea kwa biashara, bado wengi wao wameingiwa na hofu baada ya kuambiwa kuwa watapaswa kuchangia fedha kwa ajili ya ujenzi wa soko jipya.
Kwa mujibu wa uongozi wa soko hilo, wafanyabiashara waliokuwa ndani ya soko wanatakiwa kuchangia Sh500,000 kila mmoja, huku wale waliokuwa nje wakitakiwa kuchangia jumla ya Sh7 milioni.
Hata hivyo, imeelezwa kuwa fedha hizo zitarejeshwa kupitia makato ya kodi ya milango ya biashara baada ya kukamilika kwa ujenzi huo.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Alhamisi Julai 17, 2025, Mwenyekiti wa soko hilo, Jafari Sewando amesema licha ya ari waliyonayo wafanyabiashara ya kurejea kazini, uwezo wao kifedha na hususan mitaji ndilo tatizo kubwa. “Wana matumaini ya kurudi sokoni (wafanyabiashara), lakini hali ya ukwasi ni mbaya. Wengi hawana hata senti tano. Tunawaomba wadau, taasisi na kampuni wajitokeze kuwasaidia hawa wajasiriamali waliopata pigo kubwa kiuchumi,” amesema Sewando.
Aidha, amesisitiza kuwa yeyote anayetaka kusaidia anaweza kuwasiliana na Mkuu wa Wilaya, ambaye anaratibu mchakato mzima wa ujenzi wa soko hilo jipya.
Akizungumzia misaada waliyoanza kupokea amesema; “Mbunge wa Iringa Mjini anayemaliza muda wake, Jesca Msambatavangu, ameonyesha mfano kwa kuchangia zaidi ya Sh5 milioni, tunaomba na wengine sasa wajitokeze.”
Akizungumza na Mwananchi, Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) mkoani Iringa, Kibigili Said amekiri kuwapo kwa mpango wa kuchangia ujenzi wa soko jipya huku kisisitiza kuwa hakuna mfanyabiashara anayepaswa kuogopa.
Amesema fedha hizo zitakatwa kidogokidogo kupitia kodi ya milango baada ya soko kukamilika ujenzi wake.
“Hili ni jambo la mpito. Wakamilifu wa malipo hawatalazimishwa mara moja. Tutashirikiana kuhakikisha kila mmoja anarudi katika nafasi yake ya biashara,” amesema Kibigili.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta, kazi ya kusafisha eneo la soko imekamilika.
Amesema usafi huo umefanywa na Jeshi la Magereza pamoja na Jeshi la Akiba. Amesema jukumu la ujenzi wa soko hilo sasa limekabidhiwa rasmi kwa Bakwata ili kusimamia mchakato wa ujenzi wa miundombinu mipya kwa haraka.
“Tumeweka msingi mzuri kwa ajili ya ujenzi na mazingira tayari ni safi. Bakwata litakuwa msimamizi mkuu wa ujenzi huu wa kurejesha hadhi ya soko,” amesema Sitta.
Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara waliokumbwa na janga hilo wamelalamikia kutokuwa na uwezo wa kuchangia kiasi chochote cha fedha kwa sasa kutokana na hali mbaya waliyonayo.
“Hata hela ya chakula tunahangaika kupata. Tunauza kwa mikokoteni pembeni ya barabara. Hiyo laki tano tutaitoa wapi?” amesema mmoja wa wafanyabiashara hao aliyeomba hifadhi ya jina lake.
Kwa sasa, wafanyabiashara hao wanaendelea na shughuli katika maeneo yaliyotengwa kwa muda katika soko la Mlandege.