Ajali za barabarani zaongezeka Zanzibar, 17 wafariki dunia Juni

Unguja. Idadi ya ajali za barabarani imeongezeka kwa asilimia 13.3 visiwani Zanzibar kwa Juni 2025 ambapo jumla ya watu 17 walifariki dunia ukilinganisha na watu 15 waliofariki mwezi uliotangulia, Mei 2025.

Hayo yamebainishwa leo Alhamisi Julai 17, 2025 na Mtakwimu kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu Zanzibar, Asha Mussa Mahfoudh, ambaye amesema katika ajali hizo, Wilaya ya Kaskazini A imeripotiwa kuwa na ajali zaidi ya nne, sawa na asilimia 16.7 ikilinganishwa na wilaya nyingine. 

Pia, amesema idadi ya ajali za barabarani zilizotokea Juni zimeongezeka kwa asilimia 71.4 na kufikia ajali 24 kutoka ajali 14 kwa mwezi Mei.

Asha amesema, kuwa mwezi huo Wilaya ya Kaskazini A Unguja imeripotiwa kuwa na ajali zaidi ya nne ambapo mwezi Mei Wilaya ya Kaskazini A, Kaskazini B na Magharibi ‘A’ zimeripotiwa kuwa na ajali tatu kila Wilaya.

“Idadi ya waathirika waliofariki Juni 2025 imeongezeka kwa asilimia 13.3 na kufikia waathirika 17 kutoka waathirika 15 kwa Mei, huku idadi ya juu ya waathirika waliofariki kwa miezi hiyo wameripotiwa kutoka Wilaya ya Kaskazini B, waathirika wanne ambapo Mei waliripotiwa zaidi kutoka Wilaya ya Kaskazini B,” amesema Asha. 

Amesema idadi kubwa ya waathirika waliofariki dunia kwa Juni 2025, wameripotiwa kutoka Wilaya ya Kati wakiwa na waathirika wanne na Juni 2024 ni kutoka Wilaya ya Kaskazini A, na Wete waathirika watatu kila wilaya.

Pia, amesema waathirika waliojeruhiwa Juni 2025 wameongezeka kwa asilimia 10.2 na kufikia 21 kutoka 19 kwa Mei, ambapo kwa Juni, Wilaya ya Kaskazini A na Magharibi B zilikuwa na idadi ya majeruhi sita na Wilaya ya Micheweni ilikuwa na waathirika tisa waliojeruhiwa.

Kwa upande wake, Inspekta wa Jeshi la Polisi Makao Makuu Zanzibar, Omar Hamad Omar amesema jitihada zaidi zinahitajika katika kupunguza ajali za barabarani husani kwa jamii yenyewe kwani ndio watumiaji wa barabara.

Amesema ajali nyingi zinazotokea huwa zinahusisha uzembe wa mwendokasi kwa madereva hasa wanaoendesha vyombo vya magurudumu mawili wakiwemo bodaboda. 

Dk Afua Mohamed kutoka Tume ya Mipango Zanzibar amesema licha ya kuanzisha mwongozo wa utumiaji wa vyombo vya usafiri kutoka serikalini, bado ajali za barabarani zinazidi kutokea, hivyo ni wajibu wa jamii na Jeshi la Polisi kushirikiana katika kupunguza ajali hizo.