HENOCK Inonga aliondoka nchini mwaka jana kwenda Morocco kujiunga na AS FAR huku akiwa mchezaji ambaye hakuna klabu ya Tanzania haikutamani kuwa naye.
Simba ilimruhusu kishingo upande aende Morocco kwa vile alikuwa mchezaji muhimu katika kikosi chao lakini hata watani zao wa jadi Yanga bila shaka wasingeweza kuchezea fursa ya kutomsajili iwapo angeamua kujiunga nao.
Baada ya kucheza AS FAR kwa msimu mmoja, maisha yameenda kasi sana kwa Inonga ambaye hapa nchini licha ya kiwango bora ambacho alikuwa anakionyesha, alikonga nyoyo za wengi kutokana na mbwembwe zake awapo uwanjani.
Hii ni baada ya beki huyo aliyezaliwa mwaka 1993, kuwa mchezaji wa kwanza kutupiwa virago na AS FAR ambayo ni timu inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi la Nchi ya Kifalme ya Morocco.
Sababu isiyoacha shaka ni kiwango tu hakijavutia benchi la ufundi la AS FAR kuendelea naye na kuamua kumruhusu aende kwingine. Waarabu huwa sio wavumilivu na hawaogopi hasara kuvunja mkataba wa mchezaji pindi wasiporidhishwa naye.
Kwa jina ambalo Inonga amelitengeneza katika soka la Tanzania, ingekuwa zamani basi klabu zetu kubwa muda huu zingekuwa zinapigana vikumbo kuwania saini yake na usajili wake ungekuwa gumzo kubwa hapa nchini kama ambavyo imewahi kutokea kwa baadhi ya nyota hapo nyuma.
Lakini imekuwa tofauti kwani hapa kijiweni hatuoni pilika zozote kutoka katika hizo timu kubwa kuwania saini ya beki huyo na badala yake zipo katika harakati za kusaka wachezaji wengine wa kuimarisha nafasi mbalimbali zenye mapungufu.
Hili halitokei kwa bahati mbaya bali ni kukua kwa thamani ya ligi yetu kiasi ambacho leo hii klabu zetu kubwa hazikurupuki kuchukua mchezaji ambaye ametupiwa virago na klabu za nje hasa kama huko alipotoka huwa hapati nafasi ya kutosha ya kucheza.
Kingine ni klabu zetu kubwa sasa hivi zina jeuri ya fedha ambayo inazifanya ziwe na uwezo wa kuwadengulia wachezaji kwa vile zinakuwa na uhakika wa kuwapata wengine. Fikiria kama Yanga inaweza kumpata Anthony Tra Bi Tra kirahisi kwa nini ihangaike na Inonga?