Dar es Salaam. Mkoa wa Dar es Salaam umeweka wazi maeneo 88 yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji na uendelezaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi huku ikiwaita wawekezaji kuchangamkia fursa.
Maeneo hayo yanapatikana katika wilaya ya Ilala, Temeke, Kigamboni, Ubungo na Kinondoni huku kila wilaya ikijinadi aina ya uwekezaji unaohitajika na ukubwa wa eneo husika.
Maeneo yaliyo tayari kwa ajili ya uwekezaji Temeke ina maeneo 17, Kinondoni ina maeneo 29, Jiji la Dar es Salaam 9 Kigamboni 27 na Ubungo ina maeneo 16 yaliyogawiwa katika sekta 6.
Wakaifafanua aina ya uwekezaji wanaoutaka katika maeneo yaliyotengwa wawakilishi wa wilaya mbalimbali waliyanadi na kutaja sifa zake.
Kwa upande wa wilaya Temeke, Mchumi Dalton Mangowi amesema wanayo maeneo 17 ambayo yanaweza kutumika na wawekezaji katika kufanya uendelezaji za miradi mbalimbali ikiwemo michezo na biashara.
Maeneo hayo mengi yanapatikana Toangoma na Mtoni Kijichi huku baadhi ya maeneo yakifaa kwa ajili ya makazi, mabweni ya wanafunzi na shughuli za michezo.
Mchumi kutoka manispaa ya Ubungo, Andambike Kyomo aliainisha maeneo 16 ambayo yapo kwa ajili ya uwekezaji yakiwa yamegawanyika katika sekta 6 ikiwemo kilimo, biashara, michezo, usafirishaji.
Alipokuwa akielezea maeneo yaliyotengwa, aliwaita wawekezaji kuchangamkia fursa ya ujenzi wa kiwanja cha michezo wa Ubungo Sports Arena ambapo tayari eneo lenye ekari 43,268 imetengwa.
“Pia tuna fursa ya uwekezaji katika uwanja wa michezo Mburahati lenye mita za mraba 3500 linaloweza kutumika vizuri,” amesema.
Maeneo mengine ni ujenzi wa maegesho ya magari makubwa, ukusanyaji taka, ujenzi wa hoteli ya nyota tano, ukumbi wa mikutano ya kisasa ambapo eneo limetengwa Sinza Makaburini Simu2000 na Mbezi.
Pia sekta ya viwanda waliitwa wawekezaji eneo la Shekilango Complex pia katika ujenzi wa viwanda vidogo na vya kati katika eneo la Mbezi lenye ukubwa wa ekari 8.3.
Mchumi kutoka Wilaya ya Kigamboni, Rajabu Undumu amesema katika maeneo waliyoainisha pia wanavyo viwanja 80 vimetengwa kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda na kila kimoja kina ukubwa wa ekari tano ambayo inaweza kutumika kujenga kiwanda kikubwa au kidogo.
Amesema tayari baadhi ya viwanda vimeanza kuwekeza ikiwemo kile kinachozalisha vifaa vya umeme.
“Pia viwanja 40 kila kimoja kina ukubwa wa mita za mraba 1000 ambapo baadhi ya taasisi za kifedha zimewekeza. Pia tuna eneo mahususi kwa ajili ya shopping mall tuna ekari 10 ambazo zinaweza kutumika kuwekezwa ni rafiki na karibu na barabarani lipo Gezaulole,” amesema
Amesema kama wilaya ya Kigamboni wamekuwa wakishirikisha jamii wanayoihudumia inakuwa kiuchumi ikiwemo kuwapatia ujuzi kupitia elimu ya ujasiriamali na kibiashara imetolewa ili waweze kujiendesha na kutengeza mnyororo mzima wa viwanda.
Akizungumza mwakilishi wa Machinga mkoa wa Dar es Salaam, Yusuph Namoto aliomba uwekezaji unaofanyika uwe shirikishi ili nao wanufaike kwani wao hawana mitaji mikubwa.
“Kwenye maeneo yanayofanyiwa uwekezaji na watu wenye mitaji mkubwa Serikali iweke mpango wa kutenga maeneo ya machinga ndani yake ili tupate eneo la kufanyia shughuli zetu na kujipatia kipato,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tantrade, Latifa Khamis amesema mbali na kunadi maeneo ya biashara wamekuwa wakihakikisha wanawajengea uwezo wazalishaji wa bidhaa na huduma ili kuhakikisha kile wanachokifanya kinaweza kushindana katika masoko ya nje na ndani.
“Tunatamani kufanya vizuri zaidi na mkoa wa Dar es Salaam kuwa kitovu cha biashara tunaomba maafisa biashara waweze kutumika zaidi katika kufikia watu wengi zaidi,” amesema.
Naye Katibu Tawala mkoa wa Dar es Salaam, Abdul Mhite amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki ya ufanyaji biashara ili yaweze kugusa shughuli na kuhakikisha kila mwananchi anapata nafasi ya kufanya shughuli na kiuchumi na kutumia nafasi iliyopo.
Kuendelea kuheshimu sheria ya kanuni na biashara na kutumia fursa za maendeleo zinazopatikana ndani ya nchi na nje ya mipaka yake ili isaidie kusaidia kuongeza uwezo wa kiuchumi wa nchi.
“Kwa pamoja tutajenga Tanzania ya viwanda imara na uchumi wa kisasa unaogusa maisha ya Mtanzania na ya wana Dar es Salaam kwa ujumla,” amesema.