Unguja. Vijana 70,000 wanatarajiwa kunufaika na mradi wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (TVET), utakaotolewa na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (Zeea) kwa kushirikiana na Jumuiya ya Mafunzo (Commonwealth of Learning) ya nchini Canada.
Mradi huo utadumu kwa miaka miwili na utagharimu Sh10 billioni, ambapo kila mwaka vijana 35,000 watapatiwa mafunzo hayo.
Hayo yameelezwa leo Ijumaa Julai 18, 2025 na Mkurugenzi wa Zeea, Juma Burhan Mohamed wakati akitoa taarifa ya uzinduzi wa mradi huo kwa waandishi wa habari, Mjini Unguja.
“Tutahakikisha kuwa katika kipindi cha miaka miwili tunawawezesha vijana 70,000 kwa kuwasomesha, kuwapa ajira na kuwafanya kuuzika nchi nyingine, Jumuiya hii ndio ambayo imetoa fedha hizo kwa ajili ya kuwawezesha vijana,” amesema Burhan.
Mkurugenzi Burhan amesema, mradi huo unalenga kuwapa vijana ujuzi na kuwarasimisha kwa kupata ithibati ya vyeti kwa mafunzo hayo ili kujiajiri na kuajirika katika Taasisi za ndani na nje ya Tanzania.
“Katika kufikia hilo wakala huo utashirikiana na Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Stadi na Vyuo vikuu, mabaraza ya vijana na wizara husika ili kuhakikisha dira ya Zanzibar na Tanzania ya 2050 inafikiwa kwa kuwajengea vijana mazingira bora,” amesema Burhan.
Pia, amewataka vijana hao kujiunga na mafunzo hayo kwani hawatozwi ada yeyote ili kupata mafunzo.
Burhan ametoa wito kwa vijana kuwa elimu ya ufundi stadi sio kwa watu waliofeli pekee badala yake hata wenye elimu zao za juu wanapaswa kuchangamkia fursa hiyo kwani itawasaidia kuongeza ujuzi.
Naye, Mshauri Ujuzi kutoka Jumuiya hiyo, Robert Okinda amesema mradi huo una mpango wa kuandaa mikakati itakayotekelezeka na kujumuisha vijana wote hasa ambao wanakabiliwa na vizuizi vya fursa zinapojitokeza.
Amesema, madhumuni ya mradi huo ni kuwapa vijana wa Zanzibar ujuzi unaofaa kwa sekta zinazokuwa kwa kasi ikiwemo uchumi wa kidijitali, uchumi wa kijani na Uchumi wa Buluu ambapo mbinu hizo zitasaidia kuvunja vizuizi vinavyohusiana na historia ya kitaaluma, eneo, umri, jinsia, au uwezo wa kimwili na kutoa nafasi ya kushiriki kwa kila mtu.
“Mafunzo hayo yatatolewa kwa njia ya mtandaoni, njia ya ana kwa ana, na kutambua uzoefu wa awali wa kujifunza kwa kufungua milango kwa wote, bila kujali asili au elimu ya awali,” amesema Okinda.
Mbali na hilo, amesema mafunzo hayo yatatolewa kwa kushirikiana na mashirika ya kimataifa kama vile Penang Skills Development Corporation nchini Malaysia, Elimu International, na Northern Lights College ya Canada, ili kuhakikisha ujuzi unaotolewa unakuwa na viwango vya kimataifa.