Kapteni Traore aivunja Tume Huru ya Uchaguzi Burkina Faso

Serikali ya kijeshi ya Burkina Faso imeivunja rasmi Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (CENI), ikieleza kuwa chombo hicho kimekuwa kikisababisha matumizi mabaya ya fedha za umma na kuruhusu ushawishi wa kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo.

Uamuzi huo umetangazwa kupitia televisheni ya taifa (RTB), ambapo ilielezwa kuwa majukumu ya tume hiyo yatahamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani, hatua inayolenga kupunguza gharama na kuongeza ufanisi katika maandalizi ya uchaguzi ujao.

Tangu waliposhika madaraka kwa mapinduzi ya kijeshi mnamo Septemba 2022, viongozi hao wakiongozwa na Kapteni Ibrahim Traoré wamekuwa wakifanya mageuzi makubwa ya kisiasa, yakiwemo ya kuahirisha uchaguzi mkuu uliotarajiwa kufanyika mwaka 2024.

Badala yake, serikali hiyo imeongeza muda wa mpito kuelekea demokrasia hadi Julai 2029, jambo linalomruhusu Kapteni Traoré kuendelea kuwa madarakani na pia kuwa huru kugombea urais katika uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia utakaoandaliwa na serikali hiyo ya kijeshi.

Waziri wa Utawala wa Wilaya, Emile Zerbo, amenukuliwa na Shirika la Habari la AFP akisema kuwa tume hiyo ya uchaguzi ilikuwa inagharimu serikali takribani dola 870,000 kwa mwaka (sawa na zaidi ya Sh2.2 bilioni za Tanzania), huku akisisitiza kuwa uamuzi wa kuivunja ni sehemu ya juhudi za “kuimarisha udhibiti wa kitaifa wa mchakato wa uchaguzi na kupunguza ushawishi wa kigeni.”