Muheza. Zaidi ya kaya 700 ikiwemo maeneo ya biashara katika Kijiji cha Mlesa kilichopo Wilaya ya Muheza mkoani Tanga zimeunganishwa na teknolojia ya matumizi ya majiko banifu.
Majiko hayo yanayotumia kuni chache, yamewezesha wananchi wa kijiji hicho na vijiji vingine vya jirani wanaozunguka Hifadhi ya Mazingira Asili ya Amani, kulinda rasilimali za msitu kwa kupunguza uvunaji wa miti kwa ajili ya kuni.
Wakizungumza leo Ijumaa Julai 18, 2025 kijijini hapo wakati wa ziara ya Bodi ya Wadhamini wa Mfuko wa Uhifadhi wa Milima ya Tao la Mashariki (Eamcef) unaowezesha mradi huo, baadhi ya wanufaika wameeleza namna wamepunguza matumizi ya kuni.
Mmoja wa wanufaika hao, Sophia Khatibu ambaye ni mama lishe kijijini hapo, amesema kwa sasa jiko hilo limemuwezesha kutumia kuni chache tofauti na ilivyokuwa awali.
“Kama unavyoona, natumia kuni kubwa moja na ndogo moja, awali tulikuwa tunatumia jiko la kuni la kawaida la mafiga matatu ambalo lilikuwa linatumia kuni nyingi, kwa sasa hapa kwenye biashara linanisaidia kubana matumizi ya kuni,” amesema.
Amesema mbali na kutumia kuni chache, majiko hayo yanasaidia kupunguza athari za kiafya kutokana na moshi wake kutokuwa mkubwa, hivyo linapunguza athari za kiafya.
Mwenyekiti wa kikundi cha kutengeneza majiko hayo kijijini humo, Monika Joseph amesema hadi sasa wametengeneza majiko 703 majumbani na sehemu za biashara za wanakijiji wenzao na kuwa imesaidia kutunza mazingira na kupunguza watu kuingia msituni mara kwa mara.
“Kupitia mradi huu, tumeweza kutunza mazingira kwani idadi ya wanaoingia msituni imepungua, tunapata kipato, pia, kupitia shughuli hii japo kwa gharama ndogo ili kuwasaidia wanakijiji wenzetu waweze kumudu gharama na kutumia majiko haya,” amesema

Mmoja wa mamalishe kutoka Kijiji cha Mlesa,wilayani Muheza Mkoa wa Tanga, Sophia Khatibu, akizungumzia mradi wa majiko banifu.
“Awali watu wengi walikuwa wakiingia msituni jumatano na jumamosi kila wiki na kila wakiingia wanabeba mizigo mitatu ila kwa sasa kasi imepungua kwa wiki wanachukua mizigo miwili mara moja kwa wiki,” amesema.
Mwenyekiti huyo amesema asilimia kubwa wamehamasika na elimu ya upandaji miti hasa ya viungo ikiwemo mdalasini ambapo wakivuna wanatumia miti hiyo kama kuni, hivyo idadi ya wanaoingia msituni inazidi kupungua.
Kaimu Mhifadhi wa hifadhi hiyo ya Amani, Nanzia Charles amesema lengo la mradi ni kuwawezesha wananchi wanaopakana na hifadhi kutumia nishati salama na kulinda rasilimali za misiti kwa kupunguza uvunaji wa miti.
“Tunawashukuru Eamcef, wamesaidia wananchi kuwa na shughuli mbalimbali kupitia miradi na kupunguza kasi ya kuingia ndani ya hifadhi na kufanya uharibifu. Kwa sasa hifadhi iko katika hali salama uchimbaji wa madini umeisha, tunaendelea kuimarisha doria na mipaka,” amesema.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Jasper Makala amesema lengo la ziara hiyo ni kuona utekelezaji wa mfuko huo kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa na wananchi.
Amesema wanaiunga mkono juhudi za Serikali hususani kwenye matumizi ya nishati salama na kuwa matumizi ya majiko sanifu ni mojawapo ya uelekeo wa matumizi ya nishati safi na kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali katika nyanja mbalimbali.
Makala amesema wataendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu matumizi ya nishati salama ili kupunguza matumizi ya rasilimali misitu ambazo yana athari kiafya na kwenye mazingira kwa ujumla.
“Lengo la mfuko ni kushirikiana na Serikali katika kunyanyua kipato cha wana jamii tukiangalia hifadhi ya misitu, ndiyo maana tunaona kazi nyingi zinazofanyika zinahusiana na uhifadhi wa misitu, tumeona shughuli za ufugaji wa samaki, kilimo cha parachichi na majiko banifu,” amesema.
Mbali na mradi huo, mfuko huo unatekeleza miradi mingine ikiwemo ufugaji wa samaki na kilimo cha parachichi ambapo lengo ni kulinda misitu hiyo, miradi hiyo na mingine inayotekelezwa kwa vijiji 20 kutoka halmashauri tano zinazozunguka hifadhi hiyo.
Eamcef ilianzishwa kwa lengo la kutoa ruzuku kwa ajili ya kuanzisha miradi mbalimbali rafiki kwa wananchi wanaopakana na hifadhi tisa za mazingira asilia zilizopo kote nchini.