Kikao cha Fadlu, Mo Dewji Dubai kuleta mashine hizi!

MASHABIKI wa Simba bado wamepigwa na butwaa baada ya kuona sehemu ya mastaa waliosajiliwa msimu uliopita na kuiwezesha timu kufika fainali ya Kombe la Shirikisho wakipewa ‘Thank You’, lakini kocha mkuu wa timu hiyo, Fadlu Davids ametoa kauli moja ya kibabe akiwatuliza mapema.

Msimu uliopita Simba ilijinadi inajenga timu na kufanya maajabu ya kumaliza ya pili Ligi Kuu na kufika fainali ya CAF, lakini baada ya kumalizika kwa msimu tayari imeshawapa ‘Thank You’ mastaa kadhaa wakiwamo watatu wa kigeni, jambo lililowashtua Wanasimba.

Augustine Okejepha, Valentin Nouma, Fabrice Ngoma, ni kati ya wageni walioagwa Simba, huku wazawa wakiwa ni kipa Aishi Manula, Hussein Kazi, Kelvin Kijili na Omari Omari akitolewa kwa mkopo, lakini kocha Fadlu amewatuliza mashabiki kwa kuwaambia wanakuja wakali zaidi ya hao.

Kocha Fadlu ametoa kauli hiyo saa chache baada ya kufanya kikao kizito na Rais wa Heshima na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo, Mohammed ‘MO’ Dewji kilichofanyika Dubai na amewahakikisha wanachama na mashabiki wa Msimbazi kuna vyuma vitano vitashuka.

Ipo hivi. Kocha huyo kwa sasa ndiye mwenye jukumu kamili la kufanya usajili wa wachezaji wa kigeni wa timu hiyo kwa msimu ujao, baada ya kikao kizito kilichofanyika juzi kilichobeba mipango na mwelekeo kwa kikosi kipya na MO Dewji amemhakikisha usajili wa nyota watano.

Kwa mujibu wa taarifa inaelezwa Mo Dewji alionyesha imani kubwa kwa Fadlu na kumpa mamlaka yote katika kuchagua, kupendekeza na kusaini wachezaji wa kigeni.

Uamuzi huo ni sehemu ya mkakati wa klabu kujipanga upya kwa ajili ya msimu ujao na kuhakikisha inakuwa na kikosi cha ushindani zaidi kuanzia katika mashindano ya ndani hadi kimataifa.

Katika kikao hicho, Mo Dewji alieleza yuko tayari kuwekeza hadi Euro 200,000 kwa kila mchezaji wa kigeni atakayependekezwa na Fadlu, kiwango hicho ni zaidi ya Sh560 milioni. Simba inatarajia kusajili angalau wachezaji watano wa kigeni kwenye dirisha hili.

Fadlu ameweka wazi kwa Mo, anahitaji wachezaji wa kiwango cha juu katika maeneo sita muhimu ya uwanjani na wale atakaowaleta wataweza kushirikiana vizuri na wachezaji waliopo kama Ellie Mpanzu na Charles Jean Ahoua ili kuifanya Simba kuwa tishio zaidi kuliko msimu ulioisha.

Kocha huyo aliwasilisha ripoti ya maeneo anayoyahitaji na aina ya wachezaji anaowatafuta. Awali, Mwanaspoti liliandika kuhusu ripoti hiyo ni kiungo mmoja wa kati, mchezeshaji atakayemsaidia Ahoua, beki wa kati mwenye uwezo pia wa kucheza pembeni, winga mmoja na mshambuliaji wa kati.

Kupitia kikao hicho, Mo ameonyesha dhamira ya kuhakikisha Simba inarejesha ufalme wake kwenye mashindano ya ndani hasa baada ya kushuhudia timu hiyo ikiambilia patupu kwenye ligi ndani ya misimu minne mfululizo huku pia ikiwa na mipango ya kufanya vizuri zaidi kimataifa, ikumbukwe msimu uliopita timu hiyo ilifika fainali ya Kombe la Shirikisho.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, Mo aliandika ujumbe uliombatana na picha akiwa na Fadlu, uliosomeka: Nimefurahi kuwa na mazungumzo ya maana na kocha Fadlu (Davids) katika msimu wake wa kwanza, akiwa na kikosi kipya na benchi jipya la ufundi, ameiongoza Simba kufika fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF.”

“Chini ya Kocha Fadlu Davids, Simba imefika fainali ya CAF Confederation Cup, fainali ya pili ya kimataifa katika historia ya klabu. Msimu huu ulikuwa wa kujenga timu. Na bado tukafika fainali, licha ya upinzani mkali. Simba haitazuilika msimu ujao.”

Kwa Fadlu, huu ni mtihani mkubwa wa kuonyesha uelewa wake wa soko la wachezaji na namna ya kujenga kikosi imara. Tayari ametuma maombi ya wachezaji kutoka kwenye ligi kadhaa barani Afrika.

Anaamini kuwa mfumo wake wa uchezaji unahitaji wachezaji wenye kasi, nguvu na maarifa ya kiufundi.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha huyo alisema; “Tumekuwa na kikao kizuri chenye lengo moja tu la kujenga, sasa ni wakati wa kuboresha kikosi chetu kabla ya kuanza maandalizi ya msimu ujao.” 

Kamati ya usajili, licha ya kuendelea na jukumu la kusaka wachezaji wa ndani, itakuwa chini ya usimamizi wa karibu kutoka kwa Mo mwenyewe, hatua inayotafsiriwa kama njia ya kuongeza uwajibikaji na kuhakikisha kila mchezaji anayesajiliwa anakuwa na thamani kulingana na gharama inayotumika.

Mo alisisitiza hataki kuona fedha za klabu zikipotea kwa kusajili wachezaji wasiokuwa na mchango.

Kwa sasa, mazungumzo na mawakala wa baadhi ya wachezaji waliolengwa yameshaanza, huku Fadlu akitumia muda mwingi kufanya tathmini za kina kwa kila jina linalopendekezwa. Pia, amepanga kumaliza hekaheka hizo ndani ya wiki mbili zijazo kabla ya kuanza maandalizi ya msimu ujao.

Related Posts