Dodoma. Kiwanda cha kimkakati cha kutengeneza chaki kimeanza majaribio ya uzalishaji ambapo katoni za chaki 11,884 zenye thamani ya Sh19.4 milioni zimezalishwa na kuuzwa ndani na nje ya nchi.
Kiwanda hicho kimejengwa na Halmashauri ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu kwa gharama ya Sh8.09 bilioni.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha amebainisha hayo leo Julai 18, 2025 wakati akielezea mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita wa mkoa wake.
Amesema kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha chaki zaidi ya katoni 174,000 kwa mwaka.
“Kiwanda hiki kitakapoanza uzalishaji kamili kitazalisha ajira za moja kwa moja 140 na zisizo za moja kwa moja zaidi 200, hivyo kuchangia katika kuzalisha ajira katika mkoa,” amesema.
Amesema kiwanda hicho kitaongeza mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Maswa na kupunguza utegemezi wa ruzuku kutoka Serikali kuu.
Aidha, amesema kutokana na uanzishwaji wa viwanda hivyo, ajira zimeongezeka kutoka 3,701 hadi 7,037 katika sekta ya viwanda ambapo ajira za kudumu 2,408 na ajira za muda 4,629.
Macha amesema Mkoa wa Simiyu ni mzalishaji mkubwa wa zao la pamba (white gold) ambapo takribani asilimia 60 ya pamba yote inayozalishwa nchini huzalishwa katika mkoa wake.
“Uzalishaji wa mbegu za pamba umeongezeka kutoka tani 64,594 mwaka 2020 hadi tani 140,000 mwaka 2024,” amesema.
Amesema mkoa huo ndio pekee unaolima pamba hai nchini ambapo uzalishaji wa pamba hai umeongezeka kutoka tani 10,300 mwaka 2021/2022 hadi tani 12,285 mwaka 2022/2023.
Amesema kutokana na uzalishaji huo, Mkoa wa Simiyu ulishika nafasi ya saba na ya tano mtawalia katika uzalishaji wa pamba hai, ukitanguliwa na nchi za China, India, Uturuki na Tagekistan.
Kuhusu maji, Macha amesema Serikali utekelezaji wa Mradi wa maji wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi Simiyu (SCRP), Serikali inaendelea kutekeleza mradi unaogharimu Sh440 bilioni (Euro 171 milioni).
Amesema mradi huo ulianza Novemba 2023 na unatarajia kukamilika Machi 2026 na kuwa hadi sasa utekelezaji umefikia asilimia 69.
Aidha, amesema hali ya uchumi ya mkoa huo imeendelea kuimarika ambapo pato la mkoa limeongezeka kutoka Sh2.5 trilioni mwaka 2020 hadi Sh3.5 trilioni mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 42.
Pia, amesema pato la mtu mmoja mmoja limeongezeka kutoka Sh1.09 trilioni kwa mwaka 2020 hadi Sh1.53 trilioni mwaka 2024, ikiwa ni ongezeko la asilimia 40.
Kwa upande wake, mkazi wa Shinyanga, Stella Bernard ameshauri Serikali kuendelea na miradi ya kuimarisha upatikanaji wa maji hasa maeneo ya vijijini.
“Serikali ingeweka msisitizo katika miradi ya kusaidia upatikanaji wa maji kwa kuwa bado wanawake wanasumbuka kuyatafuta hasa wakati wa kiangazi,” amesema.
Kwa mujibu wa takwimu za mkoa huo, upatikanaji wa huduma ya maji vijijini umeongezeka kutoka asilimia 60.85 mwaka 2020 hadi asilimia 71.0 mwaka 2025.
Kwa upande wa upatikanaji wa maji mjini, umeongezeka kutoka asilimia 60.5 mwaka 2020 hadi asilimia 75.7 mwaka 2025.