Machinga akamatwa kwa kuchapisha, kukutwa na noti bandia za Sh36 milioni

Mwanza. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia Richard Sinkala (38), mkazi wa Rwanima Nyamagana, kwa tuhuma za kupatikana na kiasi kikubwa cha noti bandia za Kitanzania na za kigeni zenye tarakimu zinazoonyesha zaidi ya Sh36 milioni.

Sinkala, anayejishughulisha na biashara ndogondogo (machinga), alikamatwa usiku wa kuamkia Julai 18, 2025 saa 8 usiku katika mtaa wa Kageye jijini Mwanza baada ya wananchi wema kutoa taarifa za uwepo wa mtu anayemiliki fedha nyingi bandia.

Akithibitisha tukio hilo leo Julai 18, 2025 katika mkutano na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amesema baada ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi, jeshi hilo liliweka mipango ya kumkamata na kufanikiwa kumkuta na noti bandia mbalimbali na vifaa vya kutengeneza fedha hizo zikiwemo za Tanzania, Msumbiji, Marekani na Zambia.

Mutafungwa amesema katika upekuzi huo Sinkala alikuwa na kiasi kikubwa cha noti bandia zilizofikia 2,691 zenye jumla ya tarakimu za Sh36.24, zikiwemo za Sh10,000 zipatazo 646 za Sh6.4 milioni na zingine ambazo hazijakamilika kuchapishwa zenye tarakimu ya jumla ya Sh3.1 milioni.

“Pia, zilikamatwa noti 490 ambazo bado hazijakatwa zenye za Sh2.4 milioni, noti 96 za Sh2,000 zenye thamani ya Sh192,000 na noti moja ya Sh1,000,” amesema Mutafungwa.


Ameongeza kuwa; “Amekutwa na dola 34 bandia za Marekani zenye thamani ya Dola 3,400 kama zingekuwa halali, Kwacha 28 za Zambia zenye thamani ya Kwacha 560 na noti 135 za Sh500 za Msumbiji sawa na Meticais 66,500 huku zingine zikiwa bado hazijakamilika kuchapishwa zenye thamani ya zaidi ya meticais 300,000.”

Mutafungwa amesema mbali na fedha hizo, wamekamata vifaa vinavyodaiwa kutumika kwenye utengenezaji wa noti bandia ikiwemo Printa, mashine ya kuchapisha noti, pasi ya kunyooshea nguo ambayo mtuhumiwa alidai ni ya Kijerumani na amekuwa akiitumia kwenye shughuli za kitapeli.

“Amekutwa pia na dawa za rangi mbalimbali zinazotumika kuchanganya wino wa kuchapisha pamoja na Kompyuta mpakato (laptop) moja na laini nyingi za simu za mitandao tofauti ambazo zinaendelea kuhesabiwa,” amesema Mutafungwa.

Ameongeza kwamba mtuhumiwa huyo anaendelea kuhojiwa na uchunguzi ukikamilika atafikishwa kwenye vyombo vya sheria, ambapo kwa sasa jeshi hilo linashirikiana na taasisi nyingine za Serikali kubaini mtandao mzima wa watu wanaoshirikiana na mtuhumiwa huyo.

“Wizi na utapeli wa namna hii ni adui wa maendeleo, tunapaswa kushirikiana kuhakikisha wahusika wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria,” amesema Mutafungwa.