Dodoma. Wadau wamepongeza hatua ya ushirikishaji wa rika zote katika maandalizi ya Dira 2050 huku Mwenyekiti wa zamani wa Chadema, Freeman Mbowe akieleza kusikitishwa na sehemu ya dira hiyo.
Wadau wametoa maoni yao leo Alhamisi Julai 17, 2025 baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuzindua dira hiyo itakayoanza kutekelezwa Julai Mosi, 2026.
Akizungumza nje ya Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Mbowe amesema alipata mwaliko wa kuhudhuria uzinduzi huo kutoka kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwezeshaji, Profesa Kitila Mkumbo.
Amesema timu ya maandalizi ya dira imefanya jambo jema kufikia makundi mbalimbali kwenye maandalizi ya dira hiyo.
Hata hivyo, amesema iwapo Watanzania wanataka kutengeneza Taifa la kesho lililobora lazima kuwaza, kutenda na kufikiri nje ya mipaka ya kimakundi.
“Tuanze kumaliza tofauti zetu za kisiasa, kijinsia, kidini na tuanze kufikiria katika umoja wetu, badala ya vikundi vyetu na pale ambapo tulifanyiana makosa ni lazima pawepo na kukiri kwa wale ambao wanafanya makosa,” amesema.
“Na kukiri kuwa haya makosa hatutayarudia na tunavyokwenda huko mbele, tutaenda kusimamia mambo yote ambayo yanaleta mpasuko,” amesema.
Mbowe amesema utashi wa kisiasa hasa kwa viongozi ni jambo la msingi katika kufikia Tanzania iliyobora.
Mbowe amesema amesoma kwa haraka haraka dira hiyo na kusikitishwa na kile katika sehemu mojawapo ya mpango huo.
“Tume inaandika kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuboresha demokrasia na utawala bora, maboresho muhimu yaliyofanyika ni pamoja na kuboresha uhuru wa mahakama, kukuza mfumo wa vyama vingi kwa kuwepo kwa chaguzi zilizowazi na huru,” amenukuu sehemu ya dira hiyo.
Amesema kwa sehemu hiyo ukimweleza mtu yoyote ambaye yuko makini katika vyama vya siasa, ataona kwamba haipo sawa.
Mbowe amesema kusema kuwa kumefanyika maboresho kunaharibu ladha ya kazi njema inayotegemewa kufanyika huko mbele kupitia dira hiyo.
“Tunapokwenda kwenye dira mpya lazima tukiri maeneo tuliyofanya makosa na tuyarekebishe na tujenge imani kwa Watanzania wote. Lakini kwa utamaduni huu tayari tumeshaweka doa katika mambo ya msingi. Tuliyopaswa kuyarekebisha ili kutengeneza kesho ambayo ina umoja zaidi katika Taifa letu,” amesema.
Amesema wataendelea kufanya mashauriano na wanaohusika kwa namna moja ama nyingine ili kufikia makundi mbalimbali.
Mbowe amesema lengo ni kusisitiza njia bora ya kwenda vizuri kwa viongozi waandamizi Serikali kwa kukiri ukweli pale ambapo wamefanya mambo ambayo hayawapendezi wengine.
Amesema kwa kufanya hivyo kutarejesha imani katika kuyafanya makundi kuwa pamoja na hivyo kupeleka mbele Taifa katika umoja wake.
Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Askofu Fredrick Shoo amesema amefurahishwa na maandalizi ya dira hiyo kwa kuwa imewashirikisha watu wa rika zote.
Amesema ushirikishwaji huo ni mzuri kwa kuwa kilichowekwa katika dira kitafanya Watanzania wote kuwa na mzigo wa kushughulikia na hivyo kuleta maendeleo baada ya kumaliza utekelezaji wa Dira 2025 na utakapoanza utekelezaji wa dira 2050.
“Nafuraha kubwa kwamba tunaweza kufanya kitu kama hiki cha kimaendeleo. Na kilichonifurahisha sana katika dira hii ni kwamba wameshirikishwa watu wa rika zote,” amesema.
“Hata wazee kama walivyosema wazee wameridhishwa na vijana wamepata hata nakala hizi waendelee kuona maoni yao yamejumuishwa katika dira hii,” amesema.