Mstaafu wetu amesoma moja ya vifurushi vinavyotolewa na hiki kibubu kinachomtunzia hela zake, ambacho kinadai kuwa ni mojawapo ya mikakati ya kibubu hicho kuboresha maisha ya mstaafu! Anaishia kutabasamu kwa uchungu na kuishia kuchoka kabisa.
Kifurushi hicho ni kile kilichosema kuwa, inapofika siku ile mstaafu kutakiwa kwenda mbele za haki kupitia Kinondoni, au Mahezanguu kwa marehemu mama yake Lahei, au pale Bumbuli kwa Dingi wake marehemu Fidiishi, kuna mambo ambayo kibubu kinahidi kumfanyia mstaafu ili kuboresha safari yake hiyo!
Tukumbuke kwanza, mstaafu wetu wa kima cha chini ni huyu huyu ambaye amepokea pensheni ya shilingi laki moja na elfu tano kwa mwezi kwa miaka 21, na baada ya kuomba na kuomboleza sana, hatimaye mwaka jana Oktoba, Siri-kali ikakubali kumuongeza shilingi elfu hamsini katika kile ilichosema kuwa ni kuboresha maisha ya mstaafu, ambayo akaipata miezi minne baadaye!
Kibubu kinasema kuwa, mstaafu akiishakuwa rasmi mkazi wa kudumu wa Kinondoni ama Mahezanguu, kitatoa kwanza shilingi laki tano za kusaidia gharama za mazishi ya mstaafu ambaye sasa atakuwa anaimbiwa “Ona vyema nilivyowekwa humu!”
Baada ya shughuli za mazishi kumalizika, mwenza wa mstaafu anatakiwa kuwakilisha hati ya kifo chake kwenye kibubu, ili kihakiki kwamba kweli mstaafu sasa ni historia, na sio ameamua kwenda Burundi ambako waheshimiwa wa nchi wamemshauri aende akiona tozo zinakaba koo! Kuhakiki bado kunamhusu mstaafu, ingawaje sasa hawezi tena kupanda ngazi ili kuhakikiwa!
Baada ya kuhakikiwa, mwenza au kitegemezi cha mstaafu anatakiwa asubiri mirathi isomwe ndipo apate milioni tano (milioni kumi inawezekana!) ambazo kibubu kimepanga kumpa mwenza ama mtegemezi kama “kiinua mgongo” cha mstaafu akiwa marehemu, ambacho bila shaka kitamfanya mstaafu atake kuamka huko aliko!
Atataka kuamka huko aliko, maana hiyo milioni tano ni zake alizozifanyia kazi kwa miaka 40, kibanda cha mbavu za mbwa ni chake na wategemezi wake. Haya mambo ya kusubiri mirathi yanatokea wapi tena? Yeye anajua ana ndugu zake watatu tu waliobaki kutoka wanane waliokuwepo. Waliobaki wote ni kama yeye tu na dhahiri hawatakuwa na haja ya kugawana vimilioni tano na vitegemezi vya ndugu yao!
Tatizo ni kuwa mirathi itaishia kuwa mtego wa panya wa waliomo na wasiokuwemo, na ikaibua watu watakaomwambia mwenza wa mstaafu kuwa yeye ni mtoto wa mstaafu aliyempata wakati akianza kazi akijifanya kijogoo huko Kigoma, na mstaafu alikuwa hajapata nafasi ya kumtambulisha kwa ‘mama’!
Inaweza pia kumuibua mwingine akadai kuwa naye anastahili kupata japo laki tano za mirathi, maana ni baba mdogo wa shangazi yake bibi wa upande wa babu mkubwa wa marehemu mama yangu (kama mtamwelewa!) na nilipokuwa darasa la tatu alininunulia sare za shule! Mwe.
Ni mambo kama haya yanayomfanya mstaafu ambaye amefanya kazi kubwa ya kuijenga nchi kwa miaka 40, na kiinua mgongo chake kuwa siyo zaidi ya shilingi milioni 30 tu, wakati mbunge wake aliyefanya kazi inayosemekana kuwa njema ya kupiga makofi mezani na kuunga mkono hoja kwa miaka mitano.
Rudia hapo, kwa miaka mitano tuu, akilipwa kiinua mgongo cha shilingi milioni 300! Kwa nini mgongo wake usiinuke kwa “kiinua mgongo” hicho!
Ndio maana mstaafu anaona hili la mirathi lisimhusu, isije vitegemezi wake wakaibukiwa na panya waliomo na wasiokuwemo, watu ambao hawajapata kuwaona wakati baba yao mstaafu alipokuwa hai, lakini shilingi milioni tano zimewaibua!
Kibubu kimefanya jambo jema la kuwapa vitegemezi wa mstaafu milioni tano na laki tano mstaafu atakapokuwa mkazi wa kudumu wa Mahezanguu, ama Kinondoni.
Mstaafu anadhani kibubu na Siri-kali vijiongeze na kufanya jambo jema zaidi zaidi, na kutoa hizo shilingi milioni tano, hata kumi ikiwezekana… (na inawezekana, kumbuka zile milioni 300 kwa ajira ya miaka 5!) na impe mstaafu mwenyewe akiwa hai kama kinyosha mgongo chake cha uzeeni, ili ajue mwenyewe namna ya kuwaachia vitegemezi wake, hela si yake aliyoifanyia kazi kwa miaka 40?
Msitufanye wastaafu tumuamini yule George Orwell kuwa “Binadamu wote ni sawa duniani, lakini kuna binadamu wengine wapo sawa zaidi” kuliko binadamu wengine… akina sisi wastaafu wa nchi hii!
Tuwape wastaafu hizo milioni tano wakiwa hai, msingoje wakiwa marehemu! Hela si zao?
0754 340606 / 0784 340606