Kibaha. Kijana mmoja aitwaye Rajabu Musa anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumuua baba yake mzazi, baada ya kumshambulia na kisha kumtumbukiza kwenye shimo la choo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa mtuhumiwa, Rajabu Musa, alikamatwa muda mfupi baada ya tukio hilo kugundulika, na anatarajiwa kufikishwa mahakamani mara baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa awali.
Akizungumza na Mwananchi leo, Ijumaa Julai 19, 2025, Kamanda Morcase alisema:
“Tunamshikilia kijana huyo kwa tuhuma za kumuua baba yake. Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa kulikuwapo na mgogoro wa kifamilia uliodumu kwa muda mrefu.
“Hivi sasa tunaendelea na uchunguzi ili kubaini undani wa tukio hili pamoja na sababu halisi ya kitendo hicho cha kinyama.”
Majirani wa eneo hilo walipozungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu, jana Alhamisi, Julai 17, 2025, walisema kuwa chanzo halisi cha tukio hilo bado hakijafahamika rasmi.
Hata hivyo, zipo tetesi kwamba tukio hilo lilitokana na mzozo wa kifamilia baada ya marehemu, Hamis Musa, kumkatalia mwanawe fedha alizoomba kwa matumizi binafsi, akieleza kuwa hakuwa nazo kwa wakati huo.
Inadaiwa kuwa ndipo kijana huyo alianza kumshambulia baba yake, hali iliyosababisha majeraha makubwa na hatimaye kifo chake.
“Alimkuta baba yake nyumbani akaanza kumshambulia na baadaye akambeba na kwenda kumtumbukiza kwenye shimo la choo na bahati nzuri kuna mtoto mdogo alishuhudia tukio hilo akapeleka taarifa kwa majirani,” amedai John Mvula.
Mvula ambaye pia ni msaidizi wa balozi wa eneo hilo amesema kuwa baada ya hatua hiyo mmoja wa watoto wa marehemu huyo alifika nyumbani na kwamba walisaidiana na majirani kumtoa kwenye shimo la choo na kumpeleka hospitali.
“Alipelekwa Hospital ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi na baadaye Mloganzila, lakini alifariki dunia na tumemzika leo,” amesema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa huo Jackson Msuku amesema kuwa alipata taarifa kwa njia ya simu juu ya tukio hilo na alipofika aliikuta hali hiyo.
“Nilipata taarifa kwa njia ya simu juu ya tukio hilo la kusikitisha na nilipofika nikakuta majirani wapo ndipo tulipoendelea na jitihada za kumpeleka hospitali ili kuokoa maisha yake bahati mbaya alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu,” amesema.
Wananchi wa eneo hilo wameeleza kushtushwa na tukio hilo, wakisema marehemu alikuwa mtu wa heshima na mwenye maelewano na jamii.
Wametaka vyombo vya dola kuhakikisha haki inatendeka na kutoa wito wa kuimarishwa kwa malezi na elimu ya maadili kwa vijana.
Tukio la aina hii liliwahi kutokea pia katika Manispaa ya Kibaha, mkoani Pwani Oktoba 18, 2024, ambapo mwanasheria aliyefahamika kwa jina la Riziki Majala aliripotiwa kuuawa na mwanawe wa kumzaa, Juma Majala.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, Juma anadaiwa kutenda mauaji hayo baada ya mama yake kumkatalia kumpatia fedha alizokuwa akiomba kwa ajili ya matumizi yake binafsi.
Inadaiwa kuwa baada ya kugomewa, alikasirika na kuchukua hatua ya kikatili iliyopelekea kifo cha mzazi wake huyo.