Rais Mstaafu JK Ampongeza Rais Samia Kwa Dira 2050 Na Uongozi Mahiri – Video – Global Publishers



Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuongoza mchakato wa maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa umakini, uwazi na ushirikishwaji mpana.

Akizungumza mara baada ya uzinduzi rasmi wa Dira hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete (JKCC) jijini Dodoma, Dkt. Kikwete alisema mchakato huo umeonyesha mfano bora wa utawala wa kisasa unaojali maoni ya wananchi.

“Nakupongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ya kuongoza mchakato huu muhimu wa Taifa letu. Dira hii si ya serikali tu, bali ni ya Watanzania wote na uongozi wako ndio umeiwezesha kufikia hapa,” alisema Rais Mstaafu JK.

Aidha, Dkt. Kikwete alitumia nafasi hiyo kumtakia Rais Samia ushindi mkubwa na wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, akieleza kuwa ana imani na uongozi wake thabiti na maono ya mbali kwa Taifa.

“Nakuombea kila la heri katika uchaguzi mkuu ujao. Natamani ushindi mkubwa – na wa kishindo – maana kazi nzuri inaonekana,” aliongeza.

Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 inaweka mkazo kwenye uchumi jumuishi, ushirikishwaji wa vijana na wanawake, mageuzi ya kisera na maendeleo endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.