Mufindi. Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, ameagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) kushirikiana na halmashauri zote mkoani humo kuainisha maeneo yote ya uzalishaji mali na kuhakikisha yanajumuishwa katika mipango ya uboreshaji wa miundombinu ya barabara.
James amesisitiza kuwa barabara zinazoelekea katika maeneo hayo ni lazima ziweze kupitika nyakati zote za mwaka, bila kujali hali ya hewa, ili kuchochea shughuli za kiuchumi na kuwezesha wananchi kusafirisha bidhaa zao kwa urahisi.
Amesema hatua hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya mkoa na ustawi wa wananchi, hasa wakulima na wajasiriamali walioko vijijini, ambao wanategemea miundombinu bora kufikia masoko.
James ametoa kauli hiyo leo Julai 17, 2025 wakati alipokuwa akizungumza na watumishi wa halmashauri ya Mji Mafinga kwa lengo la kujitambulisha baada ya kufanya ziara kwenye halmashauri hiyo.
Aidha, mkuu huyo wa mkoa amesisitiza kuwa ni muhimu barabara hizo ziweze kupitika katika misimu yote ya mwaka, kwani changamoto ya barabara kutopitika huathiri kwa kiasi kikubwa ukusanyaji wa mapato ya halmashauri pamoja na shughuli za uzalishaji katika maeneo husika.
Amesema kukiwa na barabara ambazo zinapitika msimu mzima katika maeneo ya uzalishaji mali halmashauri zitaweza kukusanya mapato yao kwa uhakika na wananchi wataweza kupata huduma bora katika maeneo yao.
“Hali hii nimeona katika halmashauri ya Wilaya ya Mufindi yapo baadhi ya maeneo yaliathiriwa na mvua wameshindwa kwenda kukusanya mapato hali ambayo imechangia ukusanyaji wa mapato yao kushuka kutokana na changamoto hii,” amesema James.
Ameogeza kuwa ni muhimu Tarura na Tanroads kushughilika na barabara zote ambazo zinapita katika maeneo ya uzalishaji mali na kuwa na mikakati ya muda mrefu na mfupi ili barabara hizo ziweze kupitika.

“Mkoa wa Iringa uchumi wetu unabebwa na mazao ya misitu Tarura na Tanroad katika maeneo ya uzalishaji mali ikiwemo misitu, migodi na viwanda ni lazima barabara zake ziwe kipaumbele chenu katika mipango yenu ili barabara hizo ziweze kupitika,” amesisitiza James.
Meneja wa Tarura Wilaya ya Mufindi, Mhandisi Nelson Maganga, amesema wamepokea maelekezo yaliyotolewa na wanayathamini na kuyafanyia kazi kwa bidii.
Mhandisi Maganga ameongeza kuwa Tarura itashirikiana kwa karibu na taasisi nyingine, ikiwemo halmashauri, ili kuhakikisha maeneo yote ya uzalishaji pamoja na viwanda vinafikika kwa urahisi wakati wote wa mwaka.
“Sisi kama Tarura tumepokea maelekezo tupo tayari kuyafanyia kazi ili kuhakikisha mipango yetu ya muda mfupi na mrefu inajielekeza na kujikita katika maeneo ya viwanda na uzalishaji kwa kila kinachofanyika na barabara zote zinapitika kipindi cha mwaka mzima,” amesema Mhandisi Maganga.
Awali akisoma taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Fidelica Myovella amesema halmashauri hiyo ilikisia kukusanya kiasi cha Sh6.6 bilioni, lakini hadi kufikia June 30 walifanikiwa kukusanya Sh8 bilioni ambayo sawa na asilimia 120 ya makusanyo hayo.
Amesema kuwa pamoja na makusanyo hayo walibajeti kupeleka fedha katika miradi ya maendeleo kiasi cha Sh1.8 bilioni, lakini kutokana na ongezeko la makusanyo wamefanikiwa kupeleka Sh2.2 bilioni katika utekelezaji huo kupitia makusanyo ya mapato ya ndani.
“Ukusanyaji huu kama maelekezo ya Serikali ambayo yanavyosema tuhakikishe tunatatua kero za wananchi hivyo fedha hizi tulihakikisha tunapeleka kwenye miradi ya elimu na afya kwa ajili ya kumalizia maboma ambayo yalikuwa bado hayajakamilika ili kuwarahisishia wananchi kupata huduma karibu na maeneo yao,” amesema.