Serikali yatoa muda wa mwisho kusajili vituo vya malezi ya watoto mchana

Shinyanga. Mkoa wa Shinyanga una jumla ya vituo 103 vya kulelea watoto wadogo mchana, ambapo ni vituo 51 pekee ndivyo vilivyosajiliwa rasmi.

Hali hiyo imemlazimu Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, David Lyamongi, kuwataka wamiliki wa vituo vilivyosalia kuhakikisha wanasajili vituo vyao haraka iwezekanavyo.

Lyamongi amesema kutosajiliwa kwa vituo hivyo kunakiuka sheria na kanuni za uendeshaji wa huduma za malezi kwa watoto, na kunaweza kuhatarisha ustawi na usalama wa watoto wanaolelewa katika vituo hivyo visivyo rasmi.

Akifungua kikao cha wamiliki wa vituo vya kulelea watoto mchana Julai 18, 2025 Lyamongi amesema takwimu hizo ni kwa mujibu wa taarifa kutoka Halmashauri sita za Mkoa wa Shinyanga sawa na asilimia 49 ya vituo vyote vilivyo na usajili.

Lyamongi amesema katika kikao hicho cha wamiliki wa vituo vya kulea watoto mchana kimelenga kuangalia   hali ya  utekelezaji wa  Programu Jumuishi ya Taifa  ya Maendeleo ya awali ya mtoto (PJT-MMMAM) kuanzia Januari hadi Juni mwaka 2025.

Amesema makao ya watoto yatima  na wanaoishi katika mazingira hatarishi ni nane na kati ya hayo yaliyosajiliwa  ni sita  sawa na asilimia 75,ambapo amewasisitiza wamiliki wake kutumia muda uliotolewa hadi kufikia Septemba mwaka huu wawe wamesajili.

 “Vituo vyote vya kulea watoto mchana na makao ya watoto yatima na wanaoishi mazingira hatarishi wanatakiwa kusajiliwa ili kuweza kuwalinda watoto kwa mujibu wa sheria ya mtoto  Namba 21 ya mwaka 2009,” amesema Lyamongi.

Katika kikao hicho wameweka mikakati  kuhakikisha makao ya watoto na vituo vyote vinasajiliwa hadi kufikia Septemba  mwaka 2025 ili  kudhibiti vituo vinavyoibuka  na kuanza kutoa huduma pasipo kusajiliwa.

Ofisa  Ustawi wa Jamii  Mkoa wa Shinyanga, Lyidia Kwesigabo  akielezea hali halisi ya utekelezaji wa PJT-MMMAM kuanzia  Januari  hadi Juni ambapo wamefanikiwa kuzindua  mpango mkakati wa Mkoa wa kutokomeza  ukatili dhidi ya wanawake na watoto (Mtakuwwa).

Kwesigabo amesema licha ya changamoto, lakini bado kuna mafanikio ukiwemo   uandikishaji wa watoto 567  kwenye vituo  13 vya kulea watoto wadogo mchana na kutoa mafunzo ya elimu ya lishe  kwa watoa huduma ngazi ya jamii  28.

Katibu wa Umoja wa wamiliki wa   vituo vya kulea watoto mchana  Wilayani Kahama  Ediger  Walala ameiomba Serikali kuendelea kutoa elimu kwa wamiliki wa shule na kuwaeleza tofauti ya vituo vya kulea watoto na shule ili kila eneo liweze kupata huduma.