Si kila kitokacho sikioni ni ugonjwa

Baadhi ya watu hustuka wanapoingiza kijiti chenye kichungi cha pamba, unyoya au nyasi sikuoni na kutoa ute mgando wenye rangi ya kahawia, wakidhani masiko yao ni machafu sana.

Ukweli ni kwamba ute huo ni nta ya sikio, si uchafu bali ni kitu kinacholainisha, kusafisha na kulinda eneo la mfereji wa sikio.
Nta hiyo ya sikio huwa na kawaida ya kudaka vumbi, takataka na wadudu wanaoingia katika mfereji wa sikio. Huwa ni kawaida kudaka uchafu mwingi hatimaye kukakamaa.
Watalaamu wa sikio duniani wanashauri kuwa haitakiwi mara kwa mara kuondoa au kupunguza nta ya sikio, kwa kutumia kijiti pamba au njia nyingine.
Hata hivyo, kutoka maji maji sikioni kunaweza kuwa ni tatizo la kiafya hivyo kuhitaji mhusika kufika mapema katika huduma za afya kwa ajili ya ushauri na matibabu.
Uwepo wa dalili za ute au maji maji kutoka sikioni yakiwa na usaha ni muhimu kupewa kipaumbele hasa inapoambatana na hali ya maumivu na homa.
Ukiacha nta ya sikio, jambo la kwanza linalochangia kujitokeza kwa maji maji yasio ya kawaida kutoka sikioni huwa ni maambukizi ya sikio.
Maambukizi ya sikio upande wa nje, eneo la kati yanaweza kusababisha maji kumwagika kutoka sikioni, mara nyingi hufuatana na maumivu, kuwa na wekundu na mtoki.
Sababu ya pili ni kupasuka au kuraruka kwa ngoma ya sikio, hii inaweza kusababisha kutoka kwa maji maji meupe, njano au damu.
Vitu kutoka nje ya mwili vilivyopita katika sikio vinaweza kusababisha uchokozi katika tishu za sikio, ikiwamo vimelea kuvamia na kusababisha maambukizi ya sikio.
Sababu ya tatu ni ajali za kichwa au jirani na sikio, jeraha la maeneo hayo linaweza kusababisha majimaji ya uti wa mgongo kuvuja na kutoka sikioni. Hii huwa inahitaji matibabu ya haraka.
Sababu nyingine huwa ni pamoja na maji maji yanayotoka ghafla sikioni baadaye baada ya kuoga au baada ya kuogolea katika mabwawa.
Inaweza kumstua mtu aliyetokwa na maji maji haya ambayo huwa na hali kama joto joto. Haya huwa ni maji ambayo yamepenya ndani ya sikio na kukwama.
Unapofanya mijongeo kama kutembea au kurukaruka mawimbi ya mtetemo huwa kufungua njia na kuyafanya maji hayo yatoke.
Fika katika huduma za afya unapotokwa na damu, usaha, au maji maji yanayodumu zaidi ya siku chache.
Usijaribu kusafisha sikio kwa kupangusa kwa pamba au vitu vingine. Hii inaweza kusukuma nta iliyoganda zaidi ndani na kusababisha uharibifu eneo la kina la sikio.