UONGOZI wa Dodoma Jiji unaendelea na maboresho ya nyota wapya ndani ya kikosi hicho na kwa sasa umeanza mazungumzo ya kupata saini ya mshambuliaji wa Fountain Gate, Edgar William, huku akiwa tayari amewekewa mkataba wa miaka miwili.
Nyota huyo aliyeichezea Fountain Gate kwa msimu mmoja akitokea KenGold, ni pendekezo la mabosi wa Dodoma Jiji na kwa sasa wanaamini ni mbadala sahihi wa Paul Peter Kasunda aliyejiunga na JKT Tanzania, baada ya kumkosa, Andrew Simchimba.
Chaguo la kwanza la mrithi wa Paul, Dodoma Jiji lilikuwa ni la kumpata Simchimba kutoka Geita Gold aliyemaliza kinara wa mabao wa Ligi ya Championship msimu wa 2024-2025, baada ya kufunga 18, japo dili lilibuma na kuibukia Singida Black Stars.
Baada ya dili la Simchimba kuota mbawa, mabosi wa Dodoma wamehamia kwa Edgar ambaye inaelezwa yupo katika hatua nzuri za kukamilisha uhamisho huo, ikiwa ni baada tu ya kukiwezesha kikosi cha Fountain kubakia Ligi Kuu kwa msimu mwingine ujao.
Akizungumza na Mwanaspoti, Edgar alisema baada ya msimu huu kuisha bado hajafanya uamuzi wowote wa timu atakayoichezea msimu ujao, hivyo kwa sasa ameamua kupumzika kwanza, kisha muda utakapofika mashabiki zake watajua ni wapi atapokwenda.
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Dodoma Jiji, Fortunatus Johnson, alisema wanaendelea kufanyia maboresho ya nyota wapya kwa ajili ya msimu ujao, ila kwa sasa ni mapema kuweka wazi kuhusu usajili uliofanyika, kwa sababu zingine bado ni tetesi.
Msimu huu wa 2024-2025, Edgar aliifungia Fountain mabao sita ya Ligi Kuu Bara na kuasisti mawili, huku mshambuliaji huyo akikumbukwa msimu wa 2023-2024, alipokuwa mfungaji bora wa Ligi ya Championship akiwa na KenGold baada ya kufunga mabao 21.
Mbali na ufungaji bora wa Championship, Edgar alishinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa Championship msimu wa 2023-2024, akiwashinda Casto Mhagama aliyecheza naye KenGold na Mganda Boban Zirintusa wa Biashara United aliyetua Tusker FC ya Kenya.
Anashikilia rekodi nzuri katika Ligi ya Championship kwa sababu licha ya kuibuka mchezaji bora na mfungaji bora, pia amepandisha timu mbili Ligi Kuu Bara, akianza na Mbeya Kwanza msimu wa 2021-2022, kisha KenGold msimu wa 2023-2024.