Twiga Stars siyo mbaya, tujipange upya

TIMU yetu ya Taifa ya Wanawake, Twiga Stars imeshindwa kufua dafu katika Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2024 zinazoendelea huko Morocco.

Ilianza kwa kufungwa bao 1-0 na Mali kisha ikatoka sare ya bao 1-1 na Afrika Kusini na mchezo wa mwisho ikafungwa mabao 4-1 na Ghana na hivyo ikaumaliza mwendo ikiwa mkiani mwa kundi C.

Hapa kijiweni hatuwezi kuilaumu Twiga Stars kwa kutolewa mapema katika mashindano ya WAFCON 2024 huku ikishika nafasi ya mwisho kwenye kundi lake kwa vile hata hiyo pointi moja ambayo imepata katika fainali hizo, imejitahidi sana kwa vile imevuna dhidi ya bingwa mtetezi.

Kihistoria hiyo ndiyo pointi ya kwanza kwa Twiga Stars katika mashindano hayo kwani kabla ya hapo haikuwa imewahi angalau kupata sare iliposhiriki kwa mara ya kwanza mwaka 2010.

Isitoshe timu ambazo tulikuwa nazo kundi moja ni vigongo na zina uzoefu mkubwa wa mashindano ya kimataifa ya soka la wanawake kulinganisha na sisi na zimeshawahi kupata mafanikio kwa nyakati tofauti siku za nyuma.

Mfano Afrika Kusini mbali ya kuwahi kuchukua ubingwa wa WAFCON 2022, imewahi kufika hatua ya 16 ya mashindano ya Kombe la Dunia, wakati huo Ghana ikiwa imeshiriki Fainali hizo za Afrika mara 12, huku Mali yenyewe ikijivunia kushiriki mara saba.

Hakuna haja ya kumnyooshea kidole yeyote baada ya matokeo hayo ya Twiga Stars na badala yake turejee nyumbani na kujipanga zaidi ili Mungu akipenda tukirudi fainali zijazo tuwe imara zaidi.

Muhimu ni kuangalia wapi tulipojikwaa na kisha kufanyia kazi ili tusije kutolewa kinyonge tena kama ilivyotokea safari hii au kipindi kile mwaka 2010.

Mfano wa hayo ya kuyafanyia kazi ni nidhamu ya kiuchezaji katika kipindi cha pili na katika WAFCON 2024 imeonekana kuwa chini kiasi cha kuigharimu timu hadi imetolewa mapema mashindanoni.

Katika mechi tatu za WAFCON, Twiga Stars imeruhusu nyavu zake kutikiwa mara sita na kati ya hizo nne ni kipindi cha pili. Kuna tatizo hapo.