Dar es Salaam. Hatua ya Mwenyekiti wa zamani wa Chadema, Freeman Mbowe kuhudhuria hafla ya uzinduzi wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, imezidi kuwagawa makada wa chama hicho, baadhi wakimkosoa na wengine wakimtetea.
Wanaomkosoa wanajenga hoja zao wakisema, amekuwa kimya kuhusu yanayoendelea ndani ya chama chake, inawezekanaje ashiriki hafla ya kiserikali.
Kwa upande wa wanaomtetea, wanasema hatua yake ya kushiriki hafla hiyo ni haki yake ya msingi na kwamba hakuvunja sheria yoyote.
Wanaomtetea kiongozi huyo wa zamani wa Kambi Rasmi ya Upinzani (KUB), walikwenda mbali zaidi wakidai wanaomkosa Mbowe ni wenye chuki binafsi dhidi yake.
Katikati ya maoni hayo, lipo kundi linalosema alichokifanya mbunge huyo wa zamani wa Hai, ni lazima watu wamshangae kwa sababu hakuonekana kwa muda mrefu tangu kumalizika kwa uchaguzi wa ndani ya Chadema uliofanyika Januari 21, uliompa ushindi Tundu Lissu kuwa mwenyekiti wa chama hicho.
Tangu kumalizika kwa mchakato, Mbowe amekuwa mkimya, hajaongea na vyombo vya habari, mara ya mwisho alionekana Julai 6,2025 Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kijitonyama.
Kabla ya hapo, mwanasiasa huyo mkongwe alionekana hadharani Machi 25, 2025 alipohudhuria msiba wa Wilfred Joachim Ngure, ambaye ni baba mkwe wa Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba.
Mbowe amekuwa kimya na hajaonekana mahakamani wakati kesi ya Lissu anayekabiliwa na mashtaka ya uhaini inayotajwa kwa nyakati tofauti katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam na Mahakama Kuu, jambo lililotafsiriwa kwa hisia tofauti.
Hata hivyo, inaelezwa Mbowe alikwenda gerezani kumjulia halia Lissu, siku chache tangu alipopelekwa huko kutokana na kesi inayomkabili.
Katikati ya ukimya huo jana Alhamisi, Julai 17, 2025 Mbowe alishiriki uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo jijini Dodoma na kufanya mahojiano na wanahabari akitaja sababu ya ushiriki wake, kuwa amealikwa kwa kuwa ni mzalendo na ni haki yake kujua hatima ya Taifa inapangwaje.
Kuonekana kwake katika mazingira hayo umekoleza mjadala, ikizingatiwa alikuwa kimya kwa muda licha ya dhoruba inayokiandama chama chake, ikiwemo kusitishiwa ruzuku na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nashughuli zake kusimamishwa na Mahakama.
Katika tukio hilo, Mbowe la juzi aliitwa peke yake kwenda meza kuu ili kupiga picha ya ukumbusho na viongozi mbalimbali waandamizi akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Mbowe alisimama nyuma ya kiti cha Rais Samia. Baada ya hapo, Rais Samia alisimama na kiti cha Rais kikasogezwa pembeni na wawili hao (Samia na Mbowe) wakasogea mbele wakiwa wamesimama na kuibua shangwe ukumbini.
Tukio lilizidisha hisia kutoka kwa watu wanaomuunga mkono Lissu, wakidai picha hiyo itatumika kuudhihirishia ulimwengu kuwa Tanzania ina ustawi wa kisiasa, wakati mwenyekiti wa chama chake, Lissu bado anasotea gerezani.
Wakati timu Lissu ikieleza hayo kupitia mitandao ya kijamii ikiwemo makundi songezi, wanaomuunga mkono Mbowe wamejibu mapigo wakisema kiongozi huyo mstaafu ni mtu mzima, si vema kupangiwa pa kwenda au kuongea.
Baada ya tukio la uzinduzi wa dira kukamilika Mbowe alipata fursa ya kuzungumza na wanahabari akisema:“Nimekuja kushiriki kama Mtanzania mwenzenu na kuja kwangu hakuna shida, nimealikwa na nina haki ya kuja kujua kesho na hatima ya taifa langu linapangwaje sio kwamba kila kilichozungumzwa nitakikubali kwa asilimia 100.
“Vilevile si kila kitakachozungumzwa nitakipinga kwa asilimia 100, ninachuja na hii ndio kwanza Dira imezinduliwa,” alisema Mbowe.
Katika mahojiano hayo na wanahabari, Mbowe alisema ili kuwa na Taifa lenye haki ni lazima ukweli utamalaki katika Taifa, unafiki uachwe, viongozi wa kiserikali na kisiasa wawe na utashi wa kisiasa kurekebisha.
Alipoulizwa kuhusu ajenda ya Chadema ‘no reforms no election’ bila mabadiliko, hakuna uchaguzi alijibu: “Mimi ni mwanachama wa chama, tuna viongozi. Sasa mimi si msemaji wa chama, tafuta viongozi watakupa msimamo na wameshatoa msimamo.
“Sasa unaniuliza mimi wakati ni mwanachama tu…mnataka kunichoma eeeh,” alisema Mbowe.
Akizungumza na Mwananchi, Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Tanzania Bara, Amani Golugwa amesema Mbowe kwenye uzinduzi wa Dira, hakwenda kuiwakilisha Chadema bali alikwenda kwa mwaliko wake binafsi.
“Amekuwa kimya tangu amemaliza nafasi yake, mara ya mwisho tulimualika kwenye ‘retreat’ ya chama Bagamoyo baada ya uchaguzi na alisema anaomba kwenda mapumziko na atakapokuwa tayari atatwambia, tangu hapo hatukuwa na mawasiliano naye.
Tuliporejea kwenye ‘retreat’ ya chama tulikuwa na uponyaji wa majeraha na aliitwa na wazee walizungumza naye na baada ya hapo hatujawahi kuwa na mazungumzo naye, amekuwa kimya,” amesema.
Golugwa amesema kwa Mbowe kuwa kimya na kutojihusisha na mambo ya chama ikiwemo suala la Lissu mahakamani na kwa Chadema hilo si tatizo.
Amesema Chadema yenyewe imenyamaza kulingana na mwenyekiti huyo mstaafu, alivyotaka mambo yawe na kushiriki kwake kwenye shughuli za Serikali hakutumwa na chama, hivyo hawezi kuwazuia watu kumshangaa.
“Haiwezekani kuwazuia watu kumshangaa ni mwanachama wa namna gani aliyekuwa mwenyekiti zaidi ya miaka 20 hawezi kufuatilia suala la mwenyekiti wa chama chake, hayo maswali Watanzania wanamshangaa ni mwanachama wa aina gani.
“Sisi kama viongozi tumemchukulia kwa jinsi ambavyo ametaka tumchukulie, amekuwa kimya, kama yeye ameamua iwe hivyo basi hatuna lolote la kumuuliza,” amesema.
Mbunge wa zamani wa Arusha Mjini, Godbless Lema yeye alitoa waraka uliosambaa mitandaoni juu ya uamuzi wa Mbowe kwenda kushiriki shughuli hiyo.
Pamoja na mambo mengine, Lema anaeleza kwamba Mbowe akiwa mwenyekiti wa chama hicho na aliposhtakiwa kwa kesi ya ugaidi na madhira mengine aliyokuwa akipitia, walikuwa wote na hawakumuacha.
“Kwa heshima na unyenyekevu wa historia, tunakuomba, usijitenganishe na damu ya mashujaa waliokuamini,” anasema Lema.
Hoja hizo ni tofauti na alichosema aliyekuwa Mratibu wa kampeni wa Mwenyekiti Mbowe, Daniel Naftali akisema kiongozi huyo hajakosea kokote kuhudhuria kwenye uzinduzi huo na hulka ya kiongozi huyo ni mtu anayependa mijadala.
“Mbowe anaamini majadiliano na hiyo ndio hulka yake wakati wote, amekuwa akiongoza Chadema kwa muelekeo huo, kama kuna mambo ya kukubaliana kama nchi tushiriki, tulishiriki, yale anayoona yanafaa kukosoana kwa staha tulikosoa na yale mambo yanayofaa kukaa mezani na kujadiliana tulikaa na kujadili,” amesema.
Naftali amesema Mbowe ameshiriki kwenye tukio linalomgusa Mtanzania yeyote na mjadala kuhusu yeye, ulipaswa kuwepo kama angeunga mkono kila jambo lililosemwa.
Amedai wanaomkosoa hawana hoja, bali wanaongozwa na chuki na makundi yaliyojitokeza ndani ya uchaguzi wa Chadema.
“Kushiriki kwa Mbowe kwenye uzinduzi wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ni dhambi kwa mujibu wa nini, hajavunja Katiba wala sheria yoyote, na Chadema hatujakubaliana kwamba wanachama wa Chadema wasiende kwenye tukio lolote linalozungumzia mipango ya nchi,” amesema.
Katika kurasa zake za mitandao ya kijamii, mwanachama wa Chadema, Yericko Nyerere katika mjadala juu ya ushiriki wa Mbowe kwenye shughuli hiyo, ameandika:
“Ukiondoa sifa kuu aliyonayo Mbowe kama kiongozi mahiri wa kisiasa na kijamii, kwa wale msiojua na wale mnaojitoa akili, Freeman Mbowe ni mwekezaji wa ndani na nje ya nchi.”
Anasema Dira iliyozinduliwa, Mbowe kama mfanyabiashara wa kimataifa, kiongozi wa kisiasa na kijamii, ni mdau muhimu, ambapo yeye tangu mchakato wa Dira hiyo alihusishwa.
“Lakini kubwa zaidi, tuwasaidie wale wenye utindio wa ubongo, Mbowe ni ‘Statesman’ pekee aliyepo Tanzania, katika nchi hii tuliwahi kuwa na watu wachache sana ambapo walikuwa ni taasisi lakini wakiwa kwenye siasa za upinzania, akiwemo Hayati Maalim Seif. Tofauti ya Maalimu Seif na Mbowe ni kuwa Mbowe ni mfanyabiashara na mwelezaji mkubwa wa kimataifa. Huyu ni package kamili ya “statesman.”
Hoja hiyo inaungwa mkono na Mchambuzi wa Masuala ya kisiasa, Dk Matrona Kabyemela aliyesema hakuna baya kwa kiongozi huyo kuhudhuria hafla hiyo, kwani ni mdau wa maendeleo kama ilivyo kwa watu wengine.
“Kama alipata fursa ya kwenda hakuna shida, ikumbukwe mambo ya maendeleo hayana chama yanamgusa mtu yeyote bila kujali itikadi yake na hata wakati wa utengenezaji wa mpango wa dira kila mtu alishirikishwa,” amesema.
Dk Kabyemela amesema wanaomkosoa Mbowe ni wale wanaoitazama dira kama mali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) jambo ambalo si sahihi.
Mchambuzi mwingine wa Siasa, Sabatho Nyamsenda amesema ushiriki wa Mbowe kwenye Dira unazua mashaka kwa sababu mwanasiasa huyo ni mjumbe wa kamati kuu ya Chadema na amewahi kushtakiwa pia.
Wakati Mbowe akiwa na kesi Chadema kilimpigania, hivyo ilitegemewa kwa sababu ni mjumbe wa kudumu wa kamati kuu ndani ya chama chake alitakiwa kutoa kauli kuhusu yanayoendelea ndani ya chama chake.
“Jambo jingine waliokuwa viongozi wakati wa utawala wake wamejiondoa ndani ya chama, hiyo imekuwa ikitengeneza minongo’no kuwa yupo nyuma ya yale yanayotokea,” amesema.
Kwa mujibu wa Nyamsenda, matukio hayo ndio yanawapa watu wakati mgumu na kuanza kuhoji umbali wa kwenda kushiriki uzinduzi wa Dira jijini Dodoma badala ya kushiriki shughuli za chama jijini Dar es Salaam.
“Ilitegemewa kauli yake baada ya kupata mwaliko angeshukuru na kutoa kauli kuwa jambo lile linahitaji umoja wa kitaifa, hivyo hawezi kushiriki, sasa ushiriki wake umeonyesha hakuna tatizo,” amesema.